Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kuungana na Waheshimiwa Wabunge wote ambao wanasema kwamba fedha hii iongezwe ili kuweza kutoa huduma bora kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo la kushangaza sana, sisi Wabunge tumekuja hapa nia na madhumuni ni kuishauri Serikali na kuhakikisha kwamba tunaisimamia pia. Huwezi kuamini kabisa kwamba bajeti ya mwaka wa jana mpaka mwezi huu wa Aprili kulikuwa na utekelezaji wa asilimia 19.8. Hata hivyo sisi hatuoni kama hili ni janga na hatuoni kama hili ni tatizo kubwa sana, kwamba tunaweka bajeti kwa ajili ya kuhakikisha kwamba maji yanapatikana katika nchi na Watanzania wanapata maji halafu utekelezaji unakua asilimia 19.8, haya ni maajabu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli hata kama leo tunasema tunataka kuongeza hizi fedha zifikie labda za mwaka jana, lakini kama tutakuwa tunatekeleza asilimia 19 mpaka 20 haitaweza kutusaidia hata kidogo. Tatizo kubwa ni kwamba Serikali haitaki kupeleka fedha. Ninampongeza sana ndugu yangu Kitila Mkumbo ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara hii, lakini pia na watendaji wote, lakini nawaonea huruma sana kwamba wameingia katika wakati mgumu sana kwa sababu wanakwenda kufanya kazi maeneo ambayo hawapelekwi fedha, kinachoendelea ni lawama na kuonekana kwamba sio watendaji wazuri wa kazi wakati wana uwezo wa kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Serikali ihakikishe kwamba inawatimizia Watanzania mahitaji yao. Kwa sababu haiwezekani kabisa tukawa tunakaa Waheshimiwa Wabunge humu tunapanga bajeti halafu utekelezaji unakuwa asilimia 19, hii ni aibu kubwa na hii inaonyesha ni jinsi gani ambavyo Serikali ya Chama cha Mapinduzi inazidi kuwahadaa na kuwadanganya Watanzania kwa jinsi ambavyo inataka kusema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najaribu kuangalia pia katika Mji wangu wa Tunduma. Mji wa Tunduma ni Mji ambao upo mpakani mwa Zambia na Tanzania, lakini mji huu unahudumia nchi karibuni kumi. Unahudumia nchi zote za Kusini mwa Tanzania kwa mfano nchi ya Zambia, South Africa, Namibia, Angola, Congo na Botswana zote zinapita pale na mpaka wa Tunduma ni nguzo kubwa sana ya Bandari ya Dar es Salaam, asilimia 71 ya mizigo inayoshuka kwenye Bandari ya Dar es Salaam inapita kwenye mpaka wa Tunduma, lakini kuamini mpaka wa Tunduma wananchi hawana maji, wageni wanaokuja pale hawapati maji na wageni wale sasa wanakwenda kulala Zambia upande wa Nakonde, hii ni aibu kubwa sana kwa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kukuhakikishia kwamba mpaka wa Tunduma unaingiza kwa mwaka zaidi ya shilingi bilioni 80 lakini leo hakuna maji safi na salama kwenye mpaka wetu wa Tunduma. Kwa hiyo, ninaomba sana wakati Mheshimiwa Waziri anakuja hapa kuzungumza ajaribu kutueleza kwenye mpaka wa Tunduma tatizo ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hata bajeti ya mwaka wa jana tulikuwa na bajeti ya shilingi milioni 753 lakini hakuna hata shilingi iliyokwenda kwenye Mji wa Tunduma kwa ajili ya utekelezaji wa maji. Waziri anatakiwa atueleze kwanini fedha hizi hazijakwenda?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwaka jana pia kwenye bajeti kulikuwa na mradi ambao ulitaka kujengwa kwenye Mji wa Tunduma, mradi ulitaka kujengwa na kampuni ya ACCPAC International kutoka Ubelgiji; ulikuwa na thamani ya Euro milioni 100. Mradi ule mpaka leo ni hadithi na hakuna kinachoendelea, tunataka kujua na wananchi wa Mji wa Tunduma wanataka kujua ni lini mradi mkubwa huu ambao unatakiwa kutekelezwa utakwenda kutekelezwa haraka haraka iwezekanavyo kwenye Mji wa Tunduma? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka huu tunaona tena fedha zimepunguzwa. Mwaka wa jana tulikuwa tumetengewa shilingi milioni 753, mwaka huu wamepunguza mpaka kufika shilingi milioni 600; tunataka kujua pia ni kwa nini fedha zimepunguzwa ikiwa mwaka wa jana hatukupata hata shilingi moja iliyokwenda kwenye miradi ya maji kwenye Mji wa Tunduma, tatizo ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti lakini nilichoshangaa tena kwenye Mkoa wa Songwe ambako kuna Wilaya ya Ileje, Momba, Mbozi na Wilaya ya Songwe tumetengewa fedha shilingi bilioni nne katika Mkoa mzima wakati kuna Mikoa mingine wametengewa shilingi bilioni 20, ama kumi na tisa, wametengewa fedha nyingi, tatizo nini? Kwa nini Songwe tumetengewa fedha kidogo kiasi hicho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati anakuja kusema aje tu...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)