Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia sekta hii ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu, ukizingatia zaidi ya Watanzania asilimia 80 ni wakulima na wafugaji na ukizingatia kauli mbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kilimo chenye tija hatutapata malighafi kwa ajili ya viwanda bila kuboresha sekta ya mifugo hakuna njia tutakuwa na viwanda vya kuchakata nyama, ngozi, kwato, pembe na kutoa bidhaa za ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni sekta ya uvuvi, Tanzania ni kati ya nchi iliyojaliwa maziwa, bahari, mito na mabwawa ambayo tukiwekeza basi uchumi wa nchi yetu utakuwa ni wenye tija. Kama nchi tunahitaji kuwekeza kwenye uvuvi wa kisasa, kuna teknolojia za ku-fence maeneo muhimu kwenye ziwa au bahari ambapo baada ya muda huwezi vuna samaki wengi na kuweza kuwachakata na kutoa mazao mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumzie issue ya mnada wa Magena ambao ulifungwa bila sababu za msingi zaidi ya kisiasa. Nashukuru niliweza kuuliza swali humu ndani ambalo lilisababisha aliyekuwa Waziri Mheshimiwa Mwigulu Nchemba pamoja na Watendaji wake wa Wizara waliweza kufika Tarime na tukawa na vikao pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ambapo baadaye tulienda eneo la mnada na wakaongea na wananchi na kuwaahidi kuwa ule mnada utafunguliwa, maana hauhitaji gharama kuufungua, miundombinu yote ipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni takriban mwaka sasa tunaomba ule mnada ufunguliwe ili kuokoa pato la bure linalopotea kwa njia za panya ambapo ng’ombe wengi hupelekwa ng’ambo ya pili upande wa Kenya kwa maelfu. Tulikumbushana kuwa mnada wa Butiama/Kinesi uwepo lakini ule ambao upo mpakani ni wa muhimu sana, utatoa ajira nyingi kwa wananchi wa Tarime na hivyo kukuza uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wakati wa kuhitimisha niweze kupata jibu la hili, yale maazimio walioelezwa wananchi juu ya ufunguzi wa ule mnada yatatimia, wananchi wana imani na Serikali ya Awamu ya Tano, watatimiza hayo ya kukuza uchumi wa viwanda kwa kufungua ajira mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu ni kuhusiana na Chuo cha Kilimo kilichopo Tarime (Tarime Extensions Centre) kimetelekezwa kabisa wakati ni chuo ambacho kama Serikali ingewekeza tungekuwa tunatoa si tu wataalam bali Mabwana Shamba wengi ambao wangeweza kutembelea na kutoa elimu juu ya kilimo cha kisasa na ukizingatia Wilaya ya Tarime ina udongo ambao unastawi mahindi, ndizi, mihogo, mtama, alizeti, tikitimaji, ulezi, viazi vitamu, viazi mbatata, kahawa, chai zao linalochipukia, vitunguu na kadhalika. Tukiwekeza vema kwenye kilimo chenye tija Tarime tutakuza uchumi imara na viwanda vingi vitajengwa kwa ajili ya kusindika mazao haya na kuongeza thamani, viwanda vya biscuits na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba Serikali ione ni muhimu wakafanya tafiti za kina juu ya zao la bangi na kuona kama inaweza kuwa zao la biashara kwani kuna nchi hununua na kutengeneza bidhaa zinazotumika hospitalini. Pia hivi karibuni tuliona ndugu Keluch wa nchini Kenya aliweza tumia marijuana (mirungi) na kugeuza toka dawa ya kulevya na kutengeneza vinywaji mbalimbali kama wines (mvinyo), juice, maziwa ya mtindi (yoghurt) na kadhalika. Hivyo wataalam wa madawa ya kulevya pamoja na chakula na wale wa dawa za binadamu wafanye tafiti ya kina ili kuona madhara ambayo kama zao hili likiwa processed hayana direct effect, maana hili ni moja ya zao lenye uchumi mkubwa kuliko hata tumbaku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni kuhusiana na zao la kahawa na kushuka kwa bei ya kahawa jambo ambalo linakatisha tamaa wakulima. Vilevile usimamizi juu ya kilimo cha miwa huko Jimbo la Tarime Vijijini.