Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii muhimu iliyopo mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijalia uzima na afya njema na hatimaye kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Nampongeza Rais wangu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Mawaziri wote kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuliongoza Taifa hili na kuhakikisha maendeleo ya haraka na yenye tija yanapatikana kwa Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha mapinduzi kwenye uchumi wa viwanda yanapatikana na hii itafanikiwa tu iwapo tutakuwa na mikakati thabiti ya kilimo chenye tija. Asilimia 80 ya wakazi wa Mkoa wa Singida wanajishughulisha na kilimo, hulima mazao ya mahindi, uwele, mtama, viazi vitamu na muhogo kama mazao ya chakula. Pia hulima mazao ya biashara kama alizeti, vitunguu, pamba, karanga pamoja na choroko lakini wanakabiliwa na changamoto nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto hizo ni pamoja na pembejeo zisizokuwa na viwango, bei kubwa za pembejeo za zana za kilimo, ruzuku ndogo inayotolewa na Serikali, uhaba wa wataalam na mashamba darasa pamoja na uhaba wa mitaji na mikopo kwa wakulima. Hii inawakatisha tamaa sana vijana na wanawake ambao wengi wana hamasa kubwa ya kujikita katika kilimo cha kisasa lakini hukimbilia mijini ambapo hudhani ndiko kuna maisha bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mkoa wa Singida unakabiliwa na uhaba mkubwa sana wa Maafisa Ugani ambao ni watu muhimu sana katika kilimo na hasa kwa wale wananchi waliopo maeneo ya vijijini. Ukiangalia tu Wilaya ya Iramba, wapo Maafisa Ugani 79 lakini mahitaji ni 324, Wilaya ya Singida Vijijini mahitaji ya Maafisa Ugani ni 188 lakini waliopo ni 45 tu, Wilaya ya Mkalama mahitaji ni 185 lakini waliopo ni 38. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya uwepo wa Maafisa Ugani hao wachache, bado wanakabiliwa na ukosefu wa vitendea kazi kama pikipiki na hivyo kushindwa kuwafikia wananchi waliopo maeneo ya vijijini. Ni vema sasa Serikali ikaangalia jambo hili kwa kina kwa kuongeza Maafisa Ugani wa kutosha katika Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nielezee masikitiko yangu juu ya mgao mdogo wa ruzuku ya pembejeo kwa Mkoa wa Singida. Kwa msimu wa mwaka uliopita, 2016/2017, Serikali iliweza kutupatia tani 20 tu za mbegu za mpunga, tani 20 za mbegu za mahindi na tani 100 ya mbolea ya kukuzia ambayo ni sawa na asilimia 0.29 ya mbolea kwa mahitaji ya mkoa mzima. Kiwango hiki ni kidogo sana, mahitaji yetu ni kuanzia tani 33,000 mpaka 44,000 kwa mkoa mzima. Singida tumekuwa tukiachwa nyuma kwa kila jambo. Wakati ufike sasa wauangalie Mkoa wa Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Singida ni miongoni mwa mikoa inayolima mazao ya mafuta. Kwa Mkoa wa Pwani ni nazi, kwa Mkoa wa Kigoma ni mawese na Mikoa ya Singida na Dodoma ni alizeti. Hata hivyo, Serikali haijalitilia mkazo zao hili na haijalitaja kama ni zao la kimkakati, hata Mpango wa ASPD II haujatilia mkazo kabisa zao hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msimu uliopita takribani tani 58,000 ziliuzwa nchini Kongo ambazo ziliingiza zaidi ya shilingi bilioni sita. Iwapo zao hili litatiliwa mkazo uzalishaji utaweza kuongezeka lakini pia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana kwa mchango wako.