Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii na mimi nichangie hotuba ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoijadili Wizara ya Kilimo tunajadili wakulima namba moja, wafugaji pamoja na wavuvi. Chama cha Mapinduzi (CCM) ndiyo chama pekee ambacho kwenye bendera yake kuna nembo ya jembe na nyundo. Jembe linamwakilisha mkulima ambae ndiyo leo tunamjadili hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi wamechangia humu ndani. Wizara ya Kilimo ambayo ndiyo uti wa mgongo wa hili Taifa, Serikali kwenye bajeti zake wamepeleka asilimia tatu za miradi ya maendeleo ya kilimo. Asilimia tatu ambao wako kule ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni kwamba katika kila shilingi 100/= Serikali imepeleka shilingi 3/= kwa ajili ya kumwezesha mkulima ambaye yupo kwenye bendera ya Chama cha Mapinduzi, mkulima mnyonge. Tanzania ukizungumzia mnyonge, tunamzungumzia mkulima, hatumzungumzi mtu yeyote. Mkulima ndio tunajadili kwamba ndio mnyonge. Mpaka kwenye Chama cha Mapinduzi, ndiyo tulitumia kama silaha ya kumuondolea mkoloni, mnyonge mkulima, asilimia tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, magazeti baada ya kusoma hotuba, yalipongeza sana hotuba yakaisifu kwa kuondoa tozo, lakini hizi tozo hatujazijadili kwa kina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali imeondoa tozo, kwa mfano, tozo 80 kwenye mazao ya biashara, kwenye tumbaku wameondoa tozo kumi, kwenye Kahawa wameondoa tozo 17, kwenye sukari tozo 16, kwenye pamba tozo mbili, kwenye korosho tozo mbili na kwenye chai tozo moja. Sasa nataka tujadili tozo moja baada ya nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipitia tozo za sukari 16, zote kwenye kitabu zinamhusu mnunuzi na wala siyo mkulima moja kwa moja. Tozo zinamsaidia mtu wa kati, siyo mkulima wa kawaida wa chini. Tozo hazijadili kuhusu miundombinu ambayo wakulima wanahitaji. Wanahitaji soko la uhakika, wanahitaji miundombinu kwa maana ya umwagiliaji na wanahitaji mbolea. Hayo ndiyo mambo ambayo Wizara ya Kilimo ingekwenda kujadili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye tozo ya pamba, yenyewe inasema, wameondoa pale tozo mbili; ukija kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri anasema kwa mfano, kuna tozo ya kituo cha kununulia pamba katika ngazi ya Halmashauri ambayo Wizara ya Kilimo mpaka sasa hivi inasema tozo hii Wizara itawasiliana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ajili ya utekelezaji wa suala hili. Maana yake mpaka sasa hivi Wizara haijawasiliana na TAMISEMI. Tulitegemea nini hapa? Tulitegemea kwamba Wizara wanapokuja hapa, hili suala liwe limeshakwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tozo ya pili inasema tozo ya maendeleo ya elimu kwenye pamba inayotoza kwa kiwango cha shilingi 10/= kwa kilo katika Halmashauri ya Meatu, Halmashauri moja, wao Meatu waliweka hii tozo ili wachangie elimu wapate mapato ya ndani. Wizara ya Kilimo inasema, Wizara itawasiliana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ajili ya utekelezaji. Maana yake bado hawajatekeleza, lakini ilivyoandikwa ni kama jambo limekwisha, hiyo ni kwenye tozo ya pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija tozo ya korosho; tozo mbili zote zinahusu wanunuzi wa korosho. Hapo utaona tu kwamba tozo zinazoondolewa; gharama za magunia na kamba shilingi 56/=. Ni nani anahitaji hayo magunia na kamba? Ni mkulima wa kawaida? Ni yule anayenunua, anayepeleka huko mbele. Ada ya Leseni ya kununua korosho kwa kiwango cha dola 1000, siyo mkulima hapa. Wakulima wa korosho wanataka wahakikishiwe kwamba yale madawa kwa ajili ya mbolea pamoja na korosho ndiyo yanayotakiwa na ndicho ambacho tumekuwa tukikijadili hapa. Hapa ukiangalia, ni mtu wa kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokisema hapa ni kwamba tumesaidia watu, wale middle men kwa maana wafanyabiashara badala ya wakulima wa chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye tozo ya tumbaku, ni hivyo hivyo. Kati ya tozo kumi ni tozo mbili tu ndizo zinawahusu wakulima wa kawaida moja kwa moja. Ukienda kwenye tozo za kahawa kati ya 17 ni tozo mbili peke yake ndizo zinazohusu wakulima moja kwa moja. Sasa tunapojadili tozo, tujadili kwa kuwasaidia wakulima wa chini na ndiyo maana siku zote tumekuwa tukisema kwamba hapa Serikali ingekuja ingejadili uhakika wa mbolea kwa wakulima wa kawaida, uhakika wa masoko kwa wakulima wetu, miundombinu ya umwagiliaji kwa mwaka mzima. Hayo ndio mambo ambayo tungesema kwamba tunamyanyua mkulima wa kawaida tunampeleka juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo sukari ni kwamba baada ya kuona ime-mess up na hata ukisoma kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, inaonesha uagizaji wa mwaka huu, sukari inaonekana mazao yameongezeka kweli kweli kuliko mwaka 2016. Kwa hali halisi kwenye soko la humu humu ndani ni kwamba hali ya sukari ni mbaya kuliko hata ile ya mwaka uliokuwa umepita. Sasa ukipitia hizi takwimu, zinaji- contradict.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ndiyo mambo ambayo tunayahitaji hapa tuyajadili. Ukijadili takwimu kwa spin, magazeti yakakusifu lakini ulichokiandika ndani hakitekelezeki na wala hakitamgusa mwananchi wa kawaida na ndicho ambacho mimi baada ya kukisoma hivyo, ndiyo maana ukienda hata kwenye hotuba ya Kamati, Kamati imeeleza vizuri, kilimo siyo moja ya vipaumbele vya Serikali. Maoni ya Kamati ndiyo maoni ya Bunge zima maana yake Bunge tunaiambia Serikali kwamba kilimo mnachokifanya ni sawa sawa na kazi bure, haya ni maoni ya Bunge yaani Kamati ni Bunge, ndicho tunachokijadilia hapa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji majibu juu ya haya masuala. Moja, tunahitazi ufafanuzi juu ya tozo moja baada ya nyingine, hizi ambazo zimeandikwa. Kwenye Kamati hizi hazikupelekwa, zimeletwa tu hapa ndani ya Bunge na ndiyo maana tunahitaji ufafanuzi juu ya hili jambo. Jambo lingine tunahitaji uhakika kwamba hawa wakulima ambao tumekuwa tukiwajadili kila mwaka iliwemo kule Momba, mwaka 2016 Serikali imeshindwa kununua chakula na tishio la njaa la mwaka 2016 ndilo ambalo sasa mwaka huu lilitakiwa tunapokuja katika mwaka huu mpya wa fedha, tishio lililokuwa linaoneka mwaka wa fedha uliopita lilitakiwa mwaka huu sasa Wizara ije na bajeti ambayo tutasema kwamba tutanunua chakula ambacho kitaweza kusaidia nchi yetu kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nieleze tu, usalama wa Taifa siyo kuwa na bunduki nyingi. Usalama wa Taifa ni kuwa na chakula. Ukiwa na bunduki na mabomu, lakini mwisho wa siku watu wako wakiwa na njaa, hiyo vita huwezi kushinda. Ukisikia Marekani wanakwambia kwamba tuna uwezo wa kupigana vita tatu ama nne kwa wakati mmoja, ama mpaka vita sita, siyo kwamba kwa sababu wana mabomu ama wana teknolojia, wana uhakika wa kuweza ku-feed wanajeshi wao wakaendeleza mapambano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi uhakika wenyewe wa chakula ndani ya hili Taifa haupo, lakini ukiangalia mazingira yaani geographically position ya nchi yetu, ipo vizuri kabisa. Kwa maana, ukiangalia kama ni maziwa, yapo ya kutosha, kama ni mito ipo ya kutosha; lakini mwisho wa siku ni kwamba, miradi ya umwagiliaji haifanyi kazi vile inavyotakiwa. Miradi ambayo ilikuwa imeanziswa na Serikali, leo wananchi ndio wamekuwa wakilalamika.

Mheshimiwa Mewnyekiti, mwisho wa siku ni kwamba miradi hii ambayo ilikuwa imeanzishwa kwa mfano, miradi ya umwagiliaji badala ya kuwasaidia wananchi wa chini wa kawaida, sasa ile miradi anakuja mwekezaji mmoja anaambiwa sasa wewe huu mradi wa maji ndiyo utakaotumia. Kwamba anakuja mwekezaji, ameshaona miundombinu pale ya Serikali, anaambiwa ninyi mtatumia huu mradi na wananchi wa kawaida hawapewi ile namna ya kutumia yale maji kwa ajili ya kilimo cha mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo nilitaka kabisa lazima Serikali inapokuja itoe ufafanuzi wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba, tuelezwe, unapotaka kununua…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)