Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa mwisho leo katika Wizara hii.

Kwanza napenda kuwapongeza wachangiaji wote wa pande zote ambao wamechangia katika Wizara hii, wameonesha maeneo mbalimbali ambayo wanadhani kwamba yana haja ya kuboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niwapongeza kwa dhati kabisa Kamati ya Kilimo kwa kazi kubwa ambayo wameifanya ya uchambuzi wa bajeti hii na vilevile Waziri Kivuli wa Kilimo kwa maoni na mapendekezo ya Kambi ya Upinzani Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu nyingi zimeelezwa hapa kuhusiana na Wizara hii na takwimu hizo zinaonesha ni namna gani ambavyo Wizara hii ni muhimu sana na ingehitaji kuwekewa nguvu za kutosha katika namna ambavyo inatekelezwa. Mwaka 2009 pato la Taifa la nchi yetu lilikuwa ni dola za Kimarekani bilioni 21.4. Mwaka 2016, miaka saba baadaye, pato la Taifa la nchi yetu lilifikia dola za Kimarekani bilioni 52.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba ndani ya kipindi cha miaka saba, tuliweza ku-double na zaidi pato la Taifa, lakini viwango vya umaskini wa Watanzania vimekuwa vikiongezeka kwa maana ya idadi ya watu maskini Tanzania imekuwa ikiongezeka licha ya pato la Taifa kuongeza zaidi ya mara mbili. Sababu ni nini? Sababu ni sekta ya kilimo. Hatuwekezi vya kutosha kwenye sekta ya kilimo na ndiyo maana malalamiko ya Wabunge yamekuwa ni mengi sana katika hili eneo. Kwa sababu kama una sekta ambayo watu asilimia 65.5 kwa mujibu wa takwimu za Serikali wanaitegemea, lakini sekta hii katika fedha zake za maendeleo inapelekewa asilimia tatu tu, ni dhahiri kabisa kwamba hatuwafanyii kazi Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Wizara zote, tunaweza tukawa tunajadili na tukapitisha bajeti, lakini Wizara ambayo inawahusu Watanzania moja kwa moja ni Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi lakini mmeona dhahiri namna gani ambavyo Wizara hii bajeti yake, hata ile kidogo ambayo imetengwa, bado haiendi. Ukienda kuangalia vitabu vya maendeleo utaona kwamba katika kitabu cha maendeleo sehemu kubwa ya bajeti ambayo tuliitenga mwaka jana kwa ajili ya bajeti ya kilimo ilikuwa ni Storoge Capacity Expansion Project (Utunzaji wa Mazao yetu baada ya Uvuvi) mradi ambao ulikuwa ufadhiliwe locally na foreigners walikuwa ni Poland. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaposema kwamba ni bilioni tatu ambazo zimepelekwa kwenye Wizara hii maana yake ni kwamba mradi kama huu wote mwaka jana haukutekelezwa. Maana yake ni kwamba mwaka jana tumewalipa mishahara, tumewapa posho, tumewaweka ofisini wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo lakini hakuna kazi yoyote ya kimaendeleo ambayo ilifanyika. Hali kama hii kwa kweli inasikitisha sana na ni hali ambayo inabidi tuweze kuona ni namna gani ambavyo tutaweza kuirekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya kuangalia maeneo hayo ya bajeti ndogo ambayo inapelekwa ya Wizara ya Kilimo, lakini pili naomba tuweze kuangalia ni namna gani ambavyo mafanikio ambayo yamepatikana tunayalinda kivipi. Kwa mfano, napenda niwapongeze sana ndugu zangu wa Kusini kwa mavuno mazuri sana ya korosho na kwa fedha nyingi sana ambazo wamezipata kwenye korosho, lakini pamoja na ongezeko la mavuno ya korosho na ongezeko la bei ya korosho kwenye Soko la Dunia, sehemu kubwa ya mabadiliko haya ni ya bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwakani ikitokea kwamba bei ya korosho imeshuka, tutawafanya nini hawa wakulima na hapo ndipo inapokuja hoja ya msingi sana ya Hifadhi ya Jamii kwa Wakulima. Kuweka mfumo ambao utakuwa na fao la price stabilization ili pale ambapo bei za mazao ya kilimo zimekuwa kubwa sana, tuweze kuwa na sehemu ambayo itatunzwa, bei ikiporomoka chini ya gharama za uzalishaji kwa mkulima, mkulima yule atalipwa kumrudishia gharama za uzalishaji. Sasa hili ni eneo ambalo Waziri ameligusa, kuna paragraph moja amezungumza kuhusu Wakulima Scheme inaendeshwa na NSSF, lakini kuna haja kubwa ya kuweza kuangalia ni namna gani tutapanua hifadhi ya jamii kwa wakulima ili tuweze kuhakikisha kwamba wakulima wanakuwa na fao la bei. Siku bei zikiporomoka wakulima waweze kurudishwa katika zile bei ambazo angalau zitalinda hali yao ya uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa, naomba nirejee hoja ambayo Kambi ya Upinzani Bungeni imezungumza kuhusiana na tozo kwa wavuvi. Kuna malalamiko makubwa hasa kule kwetu upande wa Ziwa Tanganyika, SUMATRA inatoza leseni za usafiri kwa wavuvi na jana nimemsikia Waziri anasema kwamba kuna tozo ambazo zimeondolewa za kiwango fulani cha mitumbwi.

Naomba nipate ufafanuzi wa kutosha, kwa sababu SUMATRA hawatozi tozo ya leseni ya usafiri kwenye matreka, kwa sababu matrekta yanatumika kulima, lakini wanatoza tozo ya leseni ya wavuvi kwenye mitumbwi ya kuvulia. Sasa nataka nipate hapa haki inakuwa wapi, kwa sababu mvuvi hiki ndicho chombo chake cha kuzalisha, kwa nini atozwe, lakini mkulima chombo chake cha kuzalisha ambacho ni trekta yeye asiweze kutozwa? Kwa hiyo, naomba nipate maelezo haya ambayo pia Kambi ya Upinzani Bungeni imeyazungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, nawapongeza sana tena Kamati ya Kilimo na naomba ninukuu sehemu ya hotuba ya Kamati ya Kilimo ambayo nadhani inahitaji majibu ya Serikali, ambayo inasema kwamba; “Kwa mwenendo huu wa bajeti unaashiria kwamba, kilimo si moja ya vipaumbele vya Serikali; Serikali haitambui umuhimu wa sekta za kilimo katika ustawi wa sekta zingine na kilimo si sekta mama ya ustawi wa wananchi ambao wengi wanajihusisha na shughuli za kilimo.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi hoja za Kamati ya Kilimo, naomba zipate majibu ya uhakika kutoka Serikalini kwa sababu ndiyo hoja ambazo zinawahusu wakulima na wananchi wetu kwa ujumla. Nakushukuru sana.