Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Oliver Daniel Semuguruka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona na kunipati nafasi niweze kuchangia katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayozidi kufanya katika Taifa letu. Mimi binafsi namuombea kwa Mwenyezi Mungu azidi kumtia nguvu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa kazi nzuri wanazozidi kuzifanya kwa kulitumikia Taifa letu kwa moyo wa dhati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijielekeze moja kwa moja kutoa mchango wangu katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambayo ni Wizara nyeti inayotegemewa na Taifa letu. Mkoa wa Kagera tumebarikiwa kuwa na ardhi nzuri yenye rutuba na hali ya hewa nzuri yenye mvua nyingi za kutosha. Mkoa wa Kagera kilimo kimekuwa cha kusuasua kutokana na changamoto mbalimbali. Kwanza kabisa kuwa na teknolojia duni na pembejeo kutokufika kwa wakati. Mkoa wa Kagera tuna ardhi nzuri sana na tunapata mazao ya kila aina lakini pembejeo zimekuwa za shida sana kutufikia kwa wakati na pia teknolojia duni, bado hatujapata teknolojia za kisasa kuweza kulima kwa kutumia teknolojia hizo. (Makofi)

Katika Mkoa wa Kagera kuna miundombinu mibovu ya kusafirisha mazao toka shambani hadi kwenye masoko. Wakulima wanapata shida sana kutoka shambani hadi kufikia masoko, miundombinu ni mibovu, barabara ni mbovu. Namwomba Mheshimiwa Waziri aweze kuwasiliana na Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ili waweze kutengeneza barabara wakulima wetu waweze kufika kwenye masoko bila tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Kagera magonjwa ya mimea na mazao ya chakula kama zao la migomba linalolimwa na kutegemewa na wakazi wa Kagera linashambuliwa na ugonjwa wa mnyauko. Ugonjwa wa mnyauko umetushambulia sana katika Mkoa wetu wa Kagera ambapo migomba ndiyo tunayoitegemea kama chakula chetu kikuu. Naiomba Wizara ya Kilimo pamoja na Waziri waweze kutusaidia ili kuweza kupata tiba ya huu ugonjwa wa mnyauko kwa sababu ndilo zao kuu tunalolitegemea kwa Mkoa wa Kagera. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wangu wa Kagera umebarikiwa kuwa na mazao ya biashara ya kahawa na miwa lakini kahawa imekuwa haipati soko zuri sana yaani hatupati bei nzuri hadi inapelekea wakulima kwenda nje ya nchi, kwa mfano, wanapeleka Uganda ili waweze kupata bei nzuri. Naomba Serikali na Wizara husika waweze kuangalia zao letu la kahawa (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna zao la miwa, kwa upande wa zao hili napenda kuishauri Serikali kuweka mashamba darasa kwa wakulima wadogo wadogo ili waweze kuungana na wakulima wakubwa waweze kupata utaalamu wa kulima kwa kisasa zaidi. Naishauri Wizara ya Kilimo waweze kutuletea Maafisa Ugani, ikiwezekana kila kijiji, ili wakulima waweze kujifunza zaidi katika zao letu hili la miwa. Miwa ni zao kubwa sana ambalo linatupatia sukari, kwa mfano kwa sasa hivi sukari imekuwa tatizo katika nchi yetu, lakini tungekuwa na wakulima ambao wanaelewa vizuri hili tatizo lisingekuwepo, tungeweza ku-supply katika mikoa yote kutoka Mkoa wa Kagera. Kwa hiyo, naomba sana Wizara ya Kilimo iweze kufikiria kuweka mashamba darasa ili wakulima waweze kupata elimu ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuongelea kuhusu mawakala wa pembejeo za kilimo, mpaka sasa wameendelea kupigwa danadana kwa kutokulipwa fedha zao. Tukumbuke mawakala wengi walichukua fedha za mikopo katika benki, wengi wamepoteza hadi maisha yaani mtu akiwaza nyumba yake inapigwa mnada, hakuna mtu ambaye anaweza kumsaidia ili aweze kulipa lile deni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wameshasema kwamba wanafanya uhakiki wa mawakala wanaodai Wizara, mawakala wote nchi nzima wanadai Wizara ya Kilimo shilingi bilioni 64.4 ambapo Wizara inawapiga danadana na hawajui hatma ya deni lao, japo Wizara ya Kilimo inasema bado inafanya uhakiki wa deni hilo. Sasa itafanywa uhakiki mpaka lini na watu wanazidi kupoteza maisha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hebu fikiria hivi tunavyokuja Bungeni, mtu usipopata posho yako, tunalalamika kutokupata posho, sasa endapo umechukua mkopo wa benki na ume-supply hizo mbegu sehemu yako na bado hujaweza kulipwa, kweli hii inaumiza sana kwa sababu watu wanapoteza maisha, wanaacha familia zao zikihangaika. Naiomba sana Serikali na Wizara husika iweze kuwafikiria hawa watu ambao wali-supply hizi mbegu kwa wakulima. Basi ni vyema ikaanza kuwalipa wale iliyojiridhisha kuwa wanastahili kulipwa na wale ambao bado hawajiridhisha Wizara iangalie namna ya kuwasaidia watu hawa hata kwa mawazo. Kwa sababu mtu kama ameshatoa hela yake, inatakiwa kwa kweli apate counseling ili vifo visiendelee kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwenye uvuvi. Wavuvi hawako salama, kuna wavuvi wanakwenda kuvua usiku, wanatekwa na majambazi na wananyang’anywa samaki wao. Kwa hiyo, naomba angalau kuwepo na doria mle ziwani au baharini wanapokwenda kuvua samaki. Naomba Serikali waangalie kwa jicho la huruma suala hili. Pia leseni wasitoze zaidi ya mara moja, unaweza ukakuta mvuvi anatozwa leseni zaidi ya mara mbili, tunaomba Serikali iliangalie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuongelea pia nyavu wanazotumia zinazosemekana kwamba ni mbovu. Hivi, hizo nyavu ambazo hazitakiwi mpaka zinaingia nchini Serikali inakuwa inaangalia wapi mpaka waweze kumuonea huyu anayekwenda kuvua samaki au hawa wavuvi wanawachomea nyavu zao. Kabla hawajafika hiyo hatua, naomba Serikali ifanye uchunguzi wa hizo nyavu zisiweze kuuzwa hata madukani kwa sababu wanawapa hasara wananchi wetu. Kwa kweli inatia uchungu sana katika upande wa uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niongelee sekta ya mifugo. Mkoa wa Kagera wafugaji wamenyanyasika sana, wamehamishwa kupelekwa huku na huku na wengine wamepoteza ng’ombe wao wengi. Huku wanasema kwamba hakuna sehemu ya kufugia na wakulima vilevile wanasema hakuna sehemu ya kulima, lakini naomba Serikali iwaangalie kwa jicho la huruma hawa wafugaji na wakulima pia, itenge sehemu ya kwamba hawa wafugaji wanatakiwa wafugie sehemu fulani na hawa wakulima wapate sehemu ya kulima lakini imekuwa ni tatizo kubwa. Wafugaji wa Mkoa wa Kagera wanalia, wamenyang’anywa ng’ombe wao, wamepotea na kwa upande wa wakulima ng’ombe wanaenda kula mazao ya wakulima vilevile, yaani kote kote ni shida. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Dkt. Tizeba uliangalie hili kwa uso wa huruma. Mimi mwenyewe ni mfugaji, hata wewe najua ni mfugaji, kwa hiyo, naomba uangalie jinsi ya kusaidia hawa wafugaji waweze kupata sehemu ya kufugia ng’ombe wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishie hapa, naunga mkono hoja ya Wizara yetu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Ahsante.