Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Rose Kamili Sukum

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipatia fursa hii niweze kuchangia Wizara hii ya Kilimo ambayo ni muhimu kwa jamii nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika sana kuona kwamba Serikali haitambui umuhimu wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi. Kinachonisikitisha zaidi ni kwamba mhimili huu una maisha ya Watanzania wote. Ukiangalia kwa ndani kabisa karibu 98% wanategemea chakula kwenye Wizara hii ya Kilimo na pia 80% wanategemea ajira na 95% raw material. Ina maana kwamba hii Wizara ndiyo Wizara mama kwa sababu wategemezi wake ni wengi mno, lakini bado inaonekana kwamba hii Wizara haifai kwa kupewa 3% ya miradi ya maendeleo. Sababu ni nini, nashindwa kuelewa.

Waziri hebu atuambie, wamepigwa sindano gani ya ganzi hampati hata kufumuka? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kwenda Wizara ya Viwanda kama hukutumia Wizara ya Kilimo. Juzi Waziri wa Mambo ya Ndani amesema kiatu chake kinang’ara kwa ajili ya ngozi, kwa hiyo, wanategemea mifugo, mimi sijui kwa nini hatuoni hali halisi ya Wizara hii. Tumeona kabisa mawazo yaliyotolewa na Kamati, mawazo yaliyotolewa na Kambi ya Upinzani Bungeni, yanawaelekeza ni nini cha kufanya. Naomba sana muiangalie sana Wizara hii kwa sababu ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo ambalo linanitia wasiwasi nalo ni uwekezaji usio na tija. Sijui kama ametembelea maeneo yote ya uwekezaji, Serikali hii hii ya Awamu ya Tatu ilibinafsisha mashamba mengi sana, ikiwemo Wilaya ya Hanang mashamba ya NAFCO, naomba niyatolee mfano, yalibinafsishwa na Serikali hii lakini hakuna tija. Mashamba ya ngano, leo tunazungumza habari ya ngano inaagizwa nje, wakati kuna mashamba ya NAFCO yalikuwepo kule wamepewa wawekezaji. Matokeo yake mwekezaji huyo amepewa shamba la Gidagamowd amelima ekari 4,000 kati ya ekari 16,300. Shamba la Setchet amepewa ekari 16,330 amelima ekari 3,800. Shamba la Murujanda amepewa ekari 12,455 amelima ekari 6,000. Maana yake ekari zaidi ya 30,585 hazijalimwa, nayo ni mgogoro kwa sababu maeneo ambayo hayajalimwa wananchi wanaingia kulima, wengine wanaingia kufuga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza hawa wawekezaji ambao hawana tija kwa nini msiondoe yale mashamba kutoka kwenye mikono yao mkayarejesha kwa wananchi? Kwa nini yabaki kwao yana faida gani? Wakati wewe ndiyo Waziri wa Kilimo kwa nini asitoe kauli hiyo ya kurudisha mashamba hayo kwa wananchi? Kwa nini Waziri hakutembelea muda wote haya mashamba ya Hanang kwa ajili ya kutoa kauli? Mimi napenda kujua hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli ni vibaya sana kama mashamba yanakuwepo pale, Halmashauri haina tija, haipati hela ya mapato ya ndani, lakini Serikali nayo haipati kitu chochote, mmebinafsisha kila kitu, hakuna chochote tunachopata. Yale mashamba yalikuwa ni maeneo ya wafugaji waliyonyang’anywa na Serikali hii hii. Naomba hili liangaliwe sana kwa undani na nataka majibu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni mgogoro wa ardhi kati ya wakulima na wafugaji, pamoja na maliasili, hii ni kero kubwa. Mheshimiwa Waziri nafikiri pia naye yupo kwenye ufugaji kama sijakosea lakini Naibu Waziri alikuwa Mkurugenzi wa Pingos na mwanasheria wetu, alikuwa anatufundisha ni jinsi gani tutapata haki kwa wafugaji, mbona amejisahau au huko ndani kuna nini? Kama yeye ndiye alikuwa mwalimu wetu leo tena hakuna kinachofanyika wafugaji wanakufa, wakulima wanakufa kutokana na migogoro ya ardhi, ni nini mnachotakiwa kufanya? (Makofi)

Napenda kujua na wewe Mwenyekiti ulikuwepo Bunge la Kumi, mwezi Novemba ilitolewa hoja Bungeni Kamati ikaundwa wakaleta taarifa yao Februari, 2015 ya kwamba kuna migogoro na inatakiwa itatuliwe. Kwenye taarifa aliyoitoa Mheshimiwa Waziri nzuri sana kwamba tayari wameunda timu inafanya kazi, sasa hiyo timu tangu 2015 na 2016 haijafanya kazi halafu imetengeneza sera itawasilishwa kwenye Baraza la Mawaziri, itawasilishwa lini. Kama mwaka jana haikufanyiwa kazi na mgogoro uko watu wanakufa, hivi hiyo timu yenu ya wataalam au wanatoka nje kwamba hawakufika ndiyo wamefanya kazi sasa hivi.

Mimi naomba tuelewe, kama ni wataalam wa Tanzania muda wote huo kwa nini hawakufanya hiyo kazi na watu wanaendelea kufa. Huu mgogoro ni mkubwa sana na mnasaobabisha ni nyie Serikali kwa kweli kwa sababu watu wengine wanauawa na polisi, watu wengine wanauwawa na askari wa wanyamapori, ni mateso makubwa sana. Tunataka ardhi tengefu iwepo haraka iwezekanavyo kuondoa migogoro hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ardhi hii inatakiwa nini? Mnasema kwamba Halmshauri wakatenge watatenga wapi? Wilaya ya Hanang mmechukua heka zaidi ya laki moja, watatenga sehemu gani ili wafugaji wao wabaki pale, ni ngumu sana. Kwa hiyo, lazima muangalie ninyi wenyewe na Waziri tembea, hebu kaangalieni ninyi wenyewe siyo kutuma wataalam pekee yao, wafanye kazi kwenye eneo husika siyo kufanya kazi ya mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kulizungumzia ni taarifa inayotolewa hapa Bungeni kuhusu idadi ya mifugo waliopo Tanzania. Naomba kujua hii sensa ilifanyika lini? Mimi ni mfugaji ukiniambia ng’ombe milioni 28.4 ndiyo wako Tanzania ni kweli yaani unakubaliana na hilo? Mbuzi milioni 16, kondoo milioni tano, kuku wa asili milioni 37, hii ni taarifa ya hapa Dodoma au ni ya Tanzania nzima? Mimi sielewi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwenyewe sijaona sensa imefanyika nyumbani kwangu. Mimi ni mfugaji, sijaona aliyekuja nyumbani kwangu kufanya sensa ya ng’ombe. Sasa mtuambie hii taarifa yenu mliitoa wapi au mnaongezaongeza tu kama vile asilimia ya kuzaliwa na kadhalika, mimi nashangaa sana. Nina uhakika ng’ombe wako wengi, kondoo wako wengi, hata hao kuku ni wengi mno. Nafikiri hizi ni taarifa za mjini lakini siyo za kule ambako tunafuga mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tutakubaliana na Wizara hii maana yake sisi kila wakati tunasema jamani tuongeze bajeti halafu tukimaliza kuongea na kulalamika tukitoweka hapa ndani mkirudi mnasema hii bajeti ipite. Naomba kujua kuna matatizo gani, ni kwa nini tunashindwa kuelewana? Mawaziri ninyi mkishaacha Uwaziri mkija huku nanyi mnalia, sasa tunashindwa kuelewa, mtuambie kuna nini huko ili tusaidiane tuweze kupata manufaa kwa ajili ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala ya kusifiana, mimi leo nitamsifia sana Mheshimiwa Rais Magufuli. Mheshimiwa Rais Magufuli alipokuwa Shinyanga akasema kwamba afadhali mazao yapande bei ili wakulima tufaidike na sasa yamepanda bei mnalia nini? Wakulima tunafaidika nunueni debe kwa shilingi 30,000 ndiyo kazi hiyo maana yake yeye ndiyo kasema. Sasa tusipomsifia na yeye kwa kutupandisha sisi bei tutamsifia nani? Sasa na ninyi mnaanza kulalamika leteni mahindi bei ishuke, ishuke kwenda wapi? Mlikuwa mnatuumiza wakulima bei ya mahindi shilingi 5,000 kwa debe na shilingi 20,000 gunia sasa hivi tunapata shilingi 150,000, si raha yetu tumepata faida kuliko wafanyabiashara peke yao. Kwa hiyo, tunataka hiyo bei iendelee ili tuweze kupata manufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.