Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuchangia katika hoja iliyoko katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naanza kwa kuwapongeza Mawaziri wenye dhamana; Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri ambayo wameifanya. Hili suala la tozo kwa kweli ni jambo ambalo lilikuwa linawarudisha nyuma wakulima wetu, kwa sababu hizi tozo zote zilikuwa zinakwenda kwa mkulima. Kwa hiyo, tunaamini kabisa kwamba kwa kuondoa hizi tozo zitaongeza tija pia zitaongeza uzalishaji pamoja na ari kwa wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la utafiti hasa kwenye vyuo vyetu vile kikiwemo kile cha MATI - Mlingano. Kwa dhati kabisa tunaiomba Wizara itafute namna ya kuboresha tafiti mbalimbali za mazao ya kilimo. Sasa hivi kutokana na mabadiliko ya tabianchi, mazao mengi yameanza kukataa katika baadhi ya maeneo. Kule Lushoto sisi tulikuwa ni wakulima wazuri sana wa Kahawa, lakini sasa hivi kutokana na mabadiliko ya tabianchi, Kahawa imeanza kupotea. Hali kadhalika na Kilimanjaro hali pia siyo nzuri kama ilivyokuwa mwanzo. Kwa hiyo, tuombe hivi vyuo vifanye tafiti kuona namna gani wanaweza wakabadilisha mbegu ambayo itakuwa inaendana na mazingira ya wakati huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kule katika Jimbo la Mlalo kuna scheme ya kilimo cha mpunga, kinaitwa Mng’aro Irrigation Scheme. Scheme hii imeanzishwa mwaka 1985, wakati huo ilikuwa chini ya ufadhili wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO). Linafanya vizuri sana kwa sababu tunalima mpunga lakini pia tunalima mahindi. Scheme hii ina uwezo wa kuzalisha mahindi mara tatu ndani ya msimu mmoja wa mwaka. Kwa hiyo, inasaidia sana kupunguza tatizo la upungufu wa chakula katika maeneo ya Mkoa wa Tanga, lakini na Mkoa wa Kilimanjaro kwa baadhi ya maeneo, hasa Wilaya ya Same na Mwanga. Tatizo kubwa ni mpunga. Mpunga unaolimwa katika bonde lile hauna thamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi ukaamini hivi ninavyozungumza, gunia moja la mpunga kutoka Mng’aro ni shilingi 42,000. Kwa hiyo, unakuta mwananchi anatumia gharama kubwa sana wakati wa kulima, lakini wakati anauza mpunga huu hauna thamani. Kwa hiyo, naomba Wizara itusaidie kufanya utafiti ili tupate mbegu bora zaidi ambayo inaweza ikasaidia wakulima hawa waweze kupata soko zuri la kuweza kushindana na mpunga kutoka Kyela, Shinyanga, Ifakara na maeneo mengineyo. Kwa hiyo, tunaomba sana katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la malambo na majosho ya kuosha mifugo. Katika Halmashauri ya Lushoto tuna kata tatu ni tambarare; na hizi kata ndizo ambazo zina jamii ya wafugaji. Mwaka 1954 kabla ya Tanganyika huru, wakoloni wa Kijerumani walikuwa wamejenga lambo na josho mahali fulani na mpaka sasa hivi lipo. Pamoja na tatizo hili la kuchakata vyuma chakavu, lakini lile lambo bado lipo. Kwa hiyo, naiomba Wizara, na sisi katika Halmashauri tumeshaandika mpango wa kulifufua lile lambo ili tuwasaidie wafugaji hawa wasiingize mifugo katika Hifadhi ya Mkomazi, kwa sababu wakati mwingine hii migogoro ya wafugaji na hifadhi tunaisababisha sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumsaidia Mheshimiwa Waziri kwamba tusiweke huu mzigo moja kwa moja kwake, tumeanza katika ngazi ya Halmashauri. Kwa hiyo, tunaomba mtuunge mkono ili josho lile liweze kutumika, tuwapunguzie wafugaji hawa adha ya kuingiza mifugo kwenye hifadhi na kupigwa faini ambazo ni kubwa sana. (Makofi)

Pia nataka nimwelekeze Mheshimiwa Waziri kwamba katika Kata hizi nazozingumza ambazo zina wafugaji, pia tumeanzisha kilimo cha mazao ya mchaichai. Sasa hivi mchaichai una thamani kubwa sana duniani. Tumeanza majiribio katika ekari kama nne hivi na tumepata soko zuri, lakini soko lenye liko Pemba. Baada ya kuona kwamba zao hili linaweza likawa na tija, mwekezaji mmoja wa ndani ameagiza mtambo kutoka India na sasa hivi tunaweza tukakamua mchaichai katika Tarafa hii ya Umba ambayo ina Kata karibia nne ambazo zinalima mchaichai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitoe rai kwako kwamba unaweza ukaja ukajifunza huu ubunifu ambao tumeupata kule tukausambaza maeneo mengine ya nchi kwa sababu mchaichai hahutaji sulpher, hauhitaji pembejeo mbalimbali. Ni suala tu la kupanda, kunyweshea, baada ya muda unakata. Tani moja ya mchaichai ni shilingi 250,000. Kwa hiyo, naomba aje alichukue hilo kama shamba darasa la kueneza hiki kilimo maeneo mbalimbali katika nchi yetu. (Makofi)

Suala ambalo lingine ambalo nilikuwa nalizungumzia ni suala bulk procurement ya mbolea. Hili ni jambo ambalo linakuja kutibu tatizo sugu ambalo tulikuwa tunakumbana nalo. Sisi kule Lushoto ni wakulima wa mboga mboga na matunda, lakini mara nyingi tulikuwa tunaulizwa mbona sisi wakulima wa mboga mboga hatupati ruzuku ya kilimo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaelewa kwamba ruzuku hii ilikuwa inaenda katika maeneo yale ya uzalishaji wa chakula. Sasa kwa kuanzisha bulk procurement, maana yake ni kwamba mbolea itapatikana kwa bei ya chini na nadhani kwenye bajeti ya mwaka 2016 Waziri aliyekuwa na dhamana wakati huo alituahidi kwamba lengo ni kuhakikisha kwamba mbolea inapatikana kama vocha ya simu; au akatumia lugha nyingine kwamba ipatikane kama ambavyo unanunua CocaCola dukani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naamini kwa utaratibu huu wa kununua kwa pamoja kama ambavyo tumejifunza kwenye mafuta, utaleta tija kwa sababu kutakuwa na bei maalum, lakini pia itasaidia kuhakikisha kwamba hata wale wafanyabiashara wa ndani wanaweza sasa wakaingia kwenye fair competition. Sasa hivi siyo rahisi sana kwa mwekezaji mdogo wa ndani ku-compete na makampuni yale makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutumia bulk procure- ment maana yake ni kwamba hata hawa wafanyabishara wadogo wadogo ambao ni wazawa wa ndani wanaweza sasa na wao wakaingia katika mfumo huu, wakaagiza kiasi cha tani wanazohitaji katika maeneo yao na itawasaidia pia kukuza mitaji lakini pia kukuza dhana nzima ya uchumi kwa maana ya upande wa wazawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu tangawizi. Halmashauri ya Lushoto tunalima tangawizi, Halmashauri ya Same wanalima tangawizi, kule Njombe na Madaba wanalima tangawizi na Kigoma na Rukwa nadhani pia wameanza, lakini changamoto ipo kwenye bei. Kwa sababu mara nyingi sana tangawizi inavunwa katika muda ambao unafanana bei yake huwa inashuka kutokana na suala la demand na supply. Kwa hiyo, nimsihi Mheshimiwa Waziri tuone namna ya kuwasiliana na Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji kupitia TIRDO na SIDO tupate mashine ndogo ndogo za kuweza kui-process na kuikausha kwa sababu tunauza ikiwa mbichi, hatuwezi tukaitunza muda mrefu. Hii itasaidia kuongeza tija lakini pia tukifanya hizi pro- cessing pamoja na packaging nzuri tunaweza tukaanza kuvuka kwenye masoko ya kimataifa na kuweza kuwasaidia hawa wakulima waweze kuona tija katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu ulikuwa ni huo, nitoe tu rai kwamba Wizara hii inafanya kazi kubwa, ina ma-Extension Officer mpaka kule kwenye vijiji, tunawaomba muwatumie vizuri. Hii ndiyo Wizara pekee ambayo ukifika katika ngazi ya kijiji unaikuta lakini nadhani kuna tatizo la connection kutoka kwenye Halmashauri na kuja kwenye Wizara. Hebu tuitumie nafasi hii vizuri ku- coordinate na kuhakikisha kwamba ikitokea agizo la kitaifa basi huku chini wote wanawajibika. Tunapopita katika maeneo yetu tunagundua wakati mwingine hawa Maafisa Ugani hata hajui kwa nini yuko mahali pale. Kwa hiyo, nitoe sana wito kwamba kwa sababu mnayo hii rasilimali watu ya kutosha tuitumie vizuri kuhakikisha kwamba Wizara hii tunaitendea haki kama ambavyo tunaizungumza kwamba ndiyo uti wa mgongo wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.