Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa na mimi kuchangia hii hotuba ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote katika kuandaa bajeti hii. Napenda tu nimtaarifu mwanangu Mheshimiwa Halima Mdee kwamba unapokuwa unatoa pongezi ni kwamba unathamini muda na kazi ya mtu ambaye amefanya shughuli hiyo.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tuna kila sababu ya kukupongeza; na kweli katika kuandaa document kama hii siyo kitu cha mchezo. Kwa hiyo, naamini kabisa kwamba kutoa mawazo, kukubali au kukataa kitu, ni haki ya mtu yeyote. Kwa hiyo, hakuna sababu ya kukusoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna shaka kuwa kilimo ndiyo uti wa mgongo. Waheshimiwa Wabunge wengi wamelichangia hilo. Sambamba na hilo, bila kilimo, viwanda haviwezi kupata malighafi. Hivyo basi, maisha ya Watanzania hayawezi kuwa na tija bila kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirejee, Mkutano wa Maputo ambao ulikutana kuanzia tarehe 10 Julai hadi Disemba, 2003 ambapo viongozi wa Afrika walikutana kwa pamoja na walikubaliana kwamba asilimia 10 za Bajeti za Serikali katika nchi za Afrika ziende katika kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa sana, naona kwamba Serikali yetu bado haijafikia lengo hilo na hali kadhalika haijafikia nusu ya lengo hilo; kwamba hadi sasa hivi bajeti yetu ya kilimo ni 4.2% lengo ambalo kwa kweli bado lina hatihati sana. Kwa hiyo, naishauri Serikali yangu sikivu kwamba ione umuhimu wa kuweza kuongeza bajeti ya kilimo kama kweli tunataka kufika katika viwanda vya kati au uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, ili wananchi waweze kufaidika kwa kilimo, waweze kujitosheleza kwa chakula na kupata ziada ya kilimo ili wawe na maisha ambayo ni bora, lazima kilimo kitiliwe mkazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa tisa wa hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri, amebainisha kuwa Halmashauri za Wilaya 55 zina upungufu wa chakula kutokana na uhaba wa mvua, lakini hapa hali halisi ni kwamba kwa sababu zinategemea zaidi mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa sana ya wakulima wengi kutegemea mvua kwa ajili ya kilimo ndiyo imesababisha ukosefu wa chakula, mvua ambazo mtawanyiko wake hauridhishi na pengine mvua hizo huzidi na kuleta madhara makubwa ambayo hayana tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wengi wamezungumza na wamebainisha kwamba suluhisho pekee ili tuweze kupata mazao ya kutosha pamoja na usalama wa chakula katika nchi yetu, ni budi tujikite kwenye kilimo cha umwagiliaji. Kwa hiyo basi, Serikali ina kila sababu ya kuandaa miundombinu rafiki zaidi katika kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia njia mbalimbali zikiwemo kutumia mito ya kudumu, ambayo ninaamini tunayo, mito ya msimu, chemchemi za asili, mabwawa ya kuvuna maji ya mvua na miradi inayotumia visima virefu na vifupi. Naamini kabisa ikiwa Serikali itakuwa na nia ya dhati, tukitumia utaratibu wa umwagiliaji, basi suala la upungufu wa chakula litakuwa ni historia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuongelea ni suala la mbegu na pembejeo. Wenzangu wengi wamelizungumzia, taarifa zilizopo ni kwamba nchi yetu ina uwezo wa kuzalisha mbegu kwa asilimia 35 tu, kiasi ambacho ni kidogo sana. Kwa hiyo, inabidi sasa Serikali ikabuni mkakati mbadala. Hapa nchini tuna vyuo mbalimbali vya MATI, mfano tuna Chuo cha Mlingano - Tanga, tuna Chuo KT - Kilimanjaro, tuna Ukiriguru - Mwanza, Igurusi, Muhongo - Kigoma, MATI - Ifakara na vinginevyo kwa kuvitaja. Hebu Serikali ione jinsi gani itakavyovitumia vyuo hivi kwa kuzalisha mbegu ili mwisho wa siku tatizo la upungufu wa mbegu liweze kupungua?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Halmashauri za Wilaya pia zinaweza zikaanda mashamba darasa ya kutosha na hatimaye hili suala la kuagiza mbegu kutoka nje likapungua badala yake mbegu zikawa zinazalishwa humu humu nchini. Wenzetu katika Kamati walishauri kwamba uwepo utaratibu wa kulima kufuata Kanda maalum.

Kwa hiyo, nilikuwa nashauri hata pia katika mbegu, basi ingefanyika utaratibu huo ili kusudi nazo mbegu ziweze kuzalishwa kikanda, nikiamini kabisa na hiyo pia inaweza ikatusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Kuzalisha Mbegu, hawa ASA, inabidi nao wajitahidi, waweke malengo makubwa zaidi ili kusudi mbegu ziweze kupatikana kwa wakati na hatimaye suala la kupunguza ukosefu wa mbegu liwe ni historia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusu upungufu baadhi ya wataalam, Mabibi na Mabwana Shamba ambao pia imekuwa ni tatizo au kikwazo katika suala zima la kilimo; na hawa wamekuwa na tatizo kubwa sana kwa sababu hawana vitendea kazi vya kutosha. Kukosekana kwa vitendea kazi hivi kunawafanya washindwe kufanya kazi zao kwa ufanisi, hivyo hata kule vijijini ambako wangeweza kwenda kuwasimamia wale wananchi kwa kuwapa utaalamu inakuwa ni tatizo. Kwa hiyo, Serikali ione jinsi gani ya kuwapatia magari, pikipiki, mafuta na vile vifaa ambavyo vinastahiki ili kusudi waweze kufanya kazi zao kwa utaratibu unaotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nililotaka kulizungumzia ni suala la masoko, wenzangu wamelizungumza pia. Pamoja na kwamba baadhi ya wakulima wengi sana wanajitahidi kulima, lakini suala la masoko imekuwa ni tatizo, kwa mfano, katika Mkoa wa Dodoma tunalima sana zabibu, lakini bado soko la zabibu ni dogo. Kwa kweli inabidi tuone Serikali inafanya utaratibu gani kuhakikisha kwamba soko la zabibu tunapata watu wengi zaidi au wawekezaji wengi zaidi ili wawekeze kuweza kusindika mazao ambayo yanatokana na zabibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulizungumzia, najua muda unanitupa mkono, ni suala la utumiaji wa teknolojia duni. Kwa kweli bado tuna kila sababu ya kuona tunapata wataalam wengi zaidi kwa ajili ya kuwa na teknolojia ambazo ni za kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, ukosefu wa zana stadi za kilimo bado wananchi hawajaacha jembe la mkono. Kwa kweli bado jembe la mkono linaturudisha nyuma sana katika kilimo, wananchi wengi hawana uwezo wa kukopa hizi zana za kilimo. Kwa hiyo, bado tuna kila sababu na Serikali ina kila sababu ya kuhakikisha kwamba wananchi wake wana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. Ahsante sana.