Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Prof. Norman Adamson Sigalla King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. PROF. NORMAN A. S. KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kabla sijaendelea nichukue nafasi hii angalau kwa dakika moja kuendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayofanya ya kuiendeleza Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie mambo machache kwa haraka haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Waziri afahamu kwamba ili uendeleze kilimo na ufugaji ni vizuri Hazina (treasurers) za Serikali na hasa mashamba maalumu yaliyotengwa kwa ajil ya ufugaji ya Serikali yatumike ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wetu mstaafu baba wa Taifa hili Mwalimu Nyerere pamoja na mzee Karume mwaka 1965 walikaa kutafakari na kuona ni jinsi gani wataondoa ugomvi kati ya wakulima na wafugaji, ndipo wakaja na wazo la kusema ni lazima mashamba ya mifugo yaanzishwe ili wanaochunga ngo’mbe wajifunze kufuga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana hawa wazee, wameshalala wametangulia mbele za haki, lakini bado hekima zao na akili zao zinaonekana ziko juu sana ya upeo wetu leo. Kwa mfano Shamba la Kitulo ambalo liko Makete uwezo wake ni kuchukua ng’ombe 4,500 sasa hivi wako ng’ombe 750 tutawezaje, tutawezeshaje wananchi wa Tanzania kufuga ng’ombe na kupata maziwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Mifugo aliyepita Mheshimiwa Mwigulu Nchemba alitembelea Wilaya ya Makete akabaini hazina kubwa iliyopo pale, akaridhika kwamba ni muhimu sana zitafutwe bilioni 7.6 ili shamba lile liweze kufufuliwa ili Watanzania kutoka kaskazini na pande zote za Tanzania waweze kujifunza namna ya kufuga, tuondoe ugomvi wa kuswaga ng’ombe. Mpaka leo hivi ninavyoongea Waziri hajaenda tena kuweza kujibu hoja hii ya wananchi wa Makete kwamba ni lini hao ng’ombe watakwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji aliposimama hapa kwenye mada yake alisisitiza kwamba ng’ombe 3,000 wameagizwa kutoka nje, mpaka leo hao ng’ombe hawajaenda Kitulo. Kwa hiyo hazina ile inapotea wakati ingeweza kujibu haja ya migogoro ya wakulima lakini pia ingeweza kuboresha uchumi wa Watanzania wala si Makate peke yake, ni Watanzania wote; maana wangejifunza kule namna ya kufuga wangepata maziwa, wangepata ajira, afya zingeboreshwa na uchumi ungeboreshwa pia. Ni muhimu sana Wizara izingatie hili ili kuendeleza uchumi wetu lakini pia kuboresha mifugo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko shida ya kufasili namna bora ya kuboresha kilimo chetu. Soko limeachwa kwa wakulima ambao weledi wao uko kwenye kulima na hauko kwenye masoko. Niiombe sana Wizara, Mheshimiwa Waziri Wizara yake ni muhimu kabisa ijikite kwenye kutafuta, la kwanza masoko, ili mkulima anapolima awe na uhakika wa bei atakayouza, siyo ilimradi kuuza lakini bei atakayouza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili, ni vizuri Mheshimiwa Waziri ajikite kwenye kutafuta mbegu bora. Pale Makete na Njombe nzima tunalima sana viazi, lakini leo viazi tunavyolima havina soko kwa sababu viazi vinavyozalishwa nchi jirani ya Kenya vinauzwa kwa bei ndogo Sh.50,000/=, wakati sisi uzalishaji bei ya chini ya uzalishaji ni Sh.80,000/=. Kwa sababu hiyo kwa vyote vile tukitaka kuuza hivyo lazima tuuze kwa bei ya hasara. Tatizo haliko Kenya, tatizo liko kwetu, kwamba Wizara inafanya nini kutoa majibu ya mbegu bora ili wakulima wetu wa viazi, watumie mbegu bora hatimaye wapate viazi vingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifurahi sana rafiki yangu Mhandisi Tizeba alipoteuliwa kushika Wizara hii. Nilifurahi kwa sababu kwanza yeye ni mkulima, hata kama yeye ana fani ya uhandisi lakini ni mkulima, naamini ataitendea haki Wizara hii; kwa sababu hatusemi vitu ambavyo ni vya nadharia kwake yeye anavi-practice, analima, anajua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana rafiki yangu Mheshimiwa Tizeba apeleke nguvu kwenye kutafuta mbegu bora za viazi, pareto na mazao mengineyo, tukifanya hivi tutaharakisha maendeleo ya nchi yetu na hasa kwenye eneo la ukulima bora; vinginevyo wakulima wetu wataendelea kulaumu sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi, watadhani kwamba tunazembea. Sasa mtu mmoja akizembea ni vizuri sana ajue kwamba ni yeye aliyezembea. Nami naamini

Mheshimiwa Waziri si mzembe, kwa vyovyote vile atafanya jitihada ili kuhakikisha kwamba analigeuza hili jambo ili kwamba mbegu bora zipatikane na wakulima wapate kulima vizuri na twende mbele zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la pareto ni moja ya mazao ambayo miaka ya 80 Wilaya ya Makete ilikuwa inaongoza kwa zao la pareto. Likapoteza mwelekeo kwa hiyo bei yake ikashuka. Sasa hivi angalau bei ya pareto inarudi, niombe sana Wizara, kama nilivyosema awali isipuuze soko kuachia wakulima, hawa ni wakulima wa kawaida weledi wao ni wa kawaida, hawana weledi wa kutafuta masoko. Niombe sana Mheshimiwa Waziri aichungulie Makete ili aweze kuona ni jinsi gani ataharakisha kazi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihitimishe mchango wangu mfupi kwa kusema kwamba kama Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hatasema neno kuhusu jinsi ya kulifufua shamba la Kitulo ili wananchi wale waone faida ya kuachia hekta 12,000, kama asipokuja na majibu hakika nitashika shilingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, anafahamu rafiki yangu, sina jinsi ya kushawishika isipokuwa atoe majibu jinsi ya kuwafanya wananchi wa Makete ambao wamenituma kwenye Bunge hili waone faida ya kutunza eneo hilo na waone faida ya ng’ombe hao kuwa wamesambaa kwenye kata zote 23 za Wilaya ya Makete.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, Mungu Ibariki sana Serikali ya CCM, siungi mkono hoja mpaka atakapotoa majibu. Ahsante sana.