Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. DKT. CHRISTINA G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Kwanza kabisa nianze kwa kukushukuru wewe na pia kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais na tatu kwa kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuzungumzia kilimo. Kwa kweli asilimia 65 ya wananchi wa Tanzania wanategemea ajira kutokana na kilimo, wananchi wanategemea chakula kutoka kwenye kilimo na malighafi ya viwanda yanategemewa kutoka kwenye kilimo. Nashauri tena kilimo kiweze kupewa kipaumbele kama inavyotarajiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye upande wa bajeti; bajeti bado ni ndogo. Kuna makubaliano yaliyofanyika kwa nchi husika, makubaliano ya asilimia kumi ya Malabo pamoja na Maputo, lakini mpaka sasa hivi bado hayajatimilika. Kwa mwaka 2016/2017 ni asilimia 4.9 tu ya bajeti nzima ya Serikali ndio imepelekwa kwenye kilimo. Kwa hiyo, kwa kuwa bado Watanzania wengi wanategemea kilimo, kwa hiyo, naomba kizidi kupewa kipaumbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za maendeleo bado zinakwenda kidogo. Tumeona kuwa kwa upande wa kilimo ni asilimia 3.31 tu ndio zimekwenda kwenye fedha za maendeleo na hizo fedha za maendeleo hazitolewi kwa wakati. Kama hatupeleki hizo fedha tunategemea mipango itafanyikaje? Naishauri Serikali iweze kupeleka fedha za maendeleo tuweze kuendelea vizuri na miradi ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kuwa na kilimo bora lazima tuweze kufuata kanuni bora za kilimo na baadhi ya kanuni bora za kilimo ni pamoja na kuwa na na maji, mbegu bora, mbolea pamoja na viuatilifu ambavyo vitatuwezesha kupata mazao bora ya kilimo ambayo yatatuwezesha kupunguza utapiamlo ambao umekithiri kwenye nchi yetu; ambao umefikia takribani asilimia 34. Ili kwa pamoja tuweze kuinua kipato cha Mtanzania lazima tuweze kufuata mambo kama haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa mbegu ni asilimia 35 tu ambazo zinazalishwa Tanzania na asilimia 65 zinatoka nje na hizo asilimia 35 tukitaka kuzipeleka zina kodi, zina VAT, lakini zile za nje hazina. Kwa hiyo naomba sana Wizara, mnajitahidi sana nimewapa pongezi, kuna wanaozalisha mbegu, kuna taasisi mbalimbali kama za Magereza, JKT wanazalisha mbegu, kuna utafiti unafanyika kwenye vyuo vya utafiti na taasisi za utafiti, naomba sana tujitahidi tuweze kuzalisha mbegu zetu hapa nchini ili wananchi waache kutumia mbegu ambazo ni za kiasili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitumia mbegu za kiasili huwezi kupata mazao bora ambayo yanahitajika. Tukitumia mbegu bora pamoja na mbolea ndipo tutaweza kuzalisha mazao ambayo yanastahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa mbolea, naongelea manunuzi ya mbolea kwa pamoja. Mfumo huu tuliusubiri kwa muda mrefu, tulikuwa na mfumo ambao ulikuwa unatumia vocha, mfumo wa kutumia vocha uligubikwa na taswira za rushwa. Lakini sasa hivi tumepata mkombozi, naomba Waheshimiwa Wabunge tuweze kuupitisha mfumo huu na ninaipongeza sana Serikali na Wizara kwa kuja na mfumo huu ambao ni mzuri sana ambao utamnufaisha mwananchi na kila mwananchi ataweza kupata mbolea kwa wakati na itakuwepo kwa wakati wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nawapongeza sana Serikali kwa kuja na Mfumo huu wa Fertilizer Bulk Procurement ambao mwananchi yeyote anaweza kutumia mbolea kwa wakati wowote na ninaamini kuwa bei ya mbolea itapungua. Hata ninyi Waheshimiwa Wabunge mtaweza kutumia mbolea hii kwa sababu ule mfumo wa vocha ulikuwa unawanufaisha wakulima wachache. Kwa hiyo ni mfumo mzuri, mimi naupenda, naomba uweze kuendelea. Naipongeza Serikali kwa kuweza kuufikiria mfumo huu ambao utaanza hivi karibuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa tena pongezi sana kwa Serikali kwa kupunguza tozo nyingi sana kwa upande wa kilimo, mifugo na kwa upande wa uvuvi. Hii italeta unafuu sana kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ili waweze kuendeleza maisha yao kwa sababu tozo zilizidi na zilizidi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee NFRA ambayo inafanya kazi vizuri, naomba sana iendelee kufanya vizuri. Hata hivyo angalizo, naomba sana hayo maghala ambayo mmesema mtayajenga yaweze kujengwa kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ninashauri mnunue chakula kwa wakati, msisubiri walanguzi waanze kuingia ndipo ninyi muanze kununua na bei elekezi iweze kutolewa mapema, pamoja na mambo mengine ya mizani na magunia yasilete matatizo kwa sababu wakati mwingine huwa yanachelewa kuwafikia wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Halmashauri 55 ambazo zilikuwa na uhaba wa chakula, naomba kujua mpaka sasa hivi ni Halmashauri ngapi ambazo zinahitaji chakula? Kwa sababu najua mvua zimenyesha kwa hiyo Halmashauri nyingine ambazo zilikuwa na uhaba wa chakula sasa hivi zinavuna mazao, sasa tujue kama bado zina uhitaji wa chakula ziweze kupelekewa chakula kuliko chakula kukaa kwenye maghala. Kwa sababu chakula si vizuri kukaa kwenye maghala zaidi ya miaka mitatu, la sivyo kitaharibika, kwa hiyo, naomba sana tuangalie hali hiyo ya chakula na Halmashauri ambazo bado zinahitaji chakula ziweze kupelekewa chakula, naamini mmeanza kupeleka lakini ziweze kupelekewa chakula, nashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro ya wakulima na wafugaji. Ni kweli tulikuwa na migogoro mikubwa sana ya wakulima na wafugaji, Mkoa wangu wa Morogoro ukiwa unaongoza. Hata hivyo nashukuru kwa sababu ya hii Kamati ambayo tumeambiwa imeleta taarifa, tutaiangalia wakati ukifika. Pia ninaishukuru Serikali kwa sababu Mawaziri mbalimbali walifika huko Morogoro na walifanya kazi nzuri sana. Sasa hivi naamini migogoro imepungua. Lakini kwa nini imepungua, kwa sababu mvua inanyesha, malisho yapo, kwa hiyo inaendelea vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naishauri Serikali iweze kuangalia miundombinu ambayo ni pamoja na majosho na malambo; iangaliwe ili tusije tukarudia kwenye mgogoro huu wa wakulima na wafugaji. Pia naishukuru Serikali kwa sababu imeanza kupima ardhi kwa upande wa Ulanga pamoja na Kilombero. Ukipima ardhi na kutoa hati miliki kila mmoja atakuwa na ardhi yake na hivyo tutaendelea kupunguza migogoro ya wakulima pamoja na wafugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile naomba elimu ya malisho iendelee kutolewa ili wananchi waweze kujua kujitengenezea majani yao ya kulishia mifugo yao. Nashauri tena elimu ya kuvuna mifugo, yaani tuweze kufanya ufugaji wa kisasa na wenye tija, iendelee kutolewa na hapohapo Mheshimiwa Waziri Mwijage akituletea viwanda vya nyama.

Mhehimiwa Naibu Spika, Afisa Ugani; kuna sera inasema kuwe na Afisa Uganikwa kila kijiji, lakini mpaka sasa hivi bado hatujapata Afisa Uganikwa kila kijiji, ukimuuliza hapa Mbunge mmoja mmoja anaweza akasema hajawahi kumuona Afisa Uganikwenye kijiji chake.

Kwa hiyo, naomba mkakati wa kuendeleza na kuongeza Maafisa Ugani kwa kuomba kibali kwa Waziri mhusika aweze kutoa kibali. Maafisa Ugani wapo… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, narudia kusema Mwenyezi Mungu akubariki, naunga mkono hoja.