Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Rhoda Edward Kunchela

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Katavi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ubadhirifu wa shamba zaidi ya heka 1000 kwa ajili ya uwekezaji katika Kata ya Kakese, Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi. Shamba hili la kulima mpunga lipo katika Kata ya Kakese, Kijiji cha Mbungani na linamilikiwa na Charles Dofu na Lucas Busanda. Lilimilikiwa 1985, mwaka 1987 walianza kilimo cha biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la kuchukua eneo hili ilikuwa ni kwa ajili ya uwekezaji ambapo awali lilikuwa la wananchi. Wawekezaji hawa wanachukua mikopo benki na kuilipa kwa kuwachangisha wananchi, wanajipatia fedha kwa kupitia kundi kubwa la zaidi ya wananchi 5000.

Mheshimiwa Naibu Spika, je ni kwa nini Serikali imemuacha mwekezaji huyu fake kuendelea kuwalaghai wananchi na kujipatia mikopo mikubwa ikiwepo NBC na wanaposhindwa kulipa mkopo wanataka wananchi walipe mkopo huo?

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanalipishwa gharama kubwa wanapokodi mashamba. Kwa heka wanakodishwa kwa zaidi ya Sh.500,000/= kwa sababu ni eneo lenye udongo mzuri. Wananchi wanapiga kelele shamba lirudi kwa wananchi na Serikali ya Kijiji ili walime kwa bei ya chini na hivyo wajikwamue kiuchumi. Wananchi hawa wanatishia kuchoma moto shamba hili ambalo lina zaidi ya wakazi 8000. Hatua ya dharura inahitajika kuchukuliwa ili kuvunja Mkataba wa kujipatia maeneo kupitia kuwalaghai wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanataka kuandamana mpaka kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waziri husika; kuna hali ya tafrani katika eneo hili. Ili kunusuru vurugu zisitokee naomba Serikali itatue huu mgogoro mkubwa katika Kata hii ya Kakese. Serikali imekuwa ikitatua kero nyingi katika nchi hii kwa maslahi ya Taifa na amani; mimi nimewazuia wananchi kuja Dodoma kwa maandamano nikiamini kwamba Serikali italifanyia kazi tatizo hili kwa haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi walifunguliwa kesi na hawa wamiliki wakatumia rushwa kuhonga polisi. Wananchi wakapigwa ili kuondoka ilihali lilipatikana kutoka kwa wananchi. Je hamuoni kwamba Serikali inaibiwa kupitia wawekezaji hawa wahuni kwa umma? Tunahitaji majibu kuhusu shamba hili; lirudi kwa wananchi, hali ni mbaya, ni mwizi huyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile niipongeze hatua ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa kutoa mwelekeo wa bajeti mbadala kwa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hii ya CCM haina mapenzi mema na wananchi wake katika kuwasaidia vijana kupata ajira kupitia viwanda vidogo vidogo. Tuna wimbi kubwa la vijana waliokosa kazi vijijini kwa takwimu hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Uanzishwaji wa Mradi wa Viwanda Vidogo Vidogo Vijijini 2016/2017. Serikali imeanzisha viwanda vipya 161 vidogo vijijini Tanzania nzima na kufanikiwa kuajiri vijana 1,098. Ajira hizi ni chache ukizingatia vijana wengi wako vijijini na hawana elimu. Tulitegemea vijana hawa wangewekewa mkakati wa kuwapatia ajira na si kuwadidimiza kiuchumi vijana wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuboresha mazingira ya uwekezaji ni jukumu la Serikali ili kuhakikisha sheria kanuni na utendaji wa sekta ya umma unakuwa rafiki kwa wawekezaji ili kutoa ajira, kuwalipa vijana kwa wakati, kuacha unyanyasaji kwa vijana wanaofanya kazi migodini katika Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mgodi wa Isulamilomo (Nsimbo Katavi), kuna mwekezaji mchimbaji yuko pale na hana leseni; amepora eneo kubwa na vijana wamebaki hawana maeneo. Huyu bwana (Mbogo) Simon Mdandila anazua tafrani na uvunjifu wa amani kwa kuwanyima fursa vijana kupitia kujiajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, vijana zaidi ya 450 wanashindwa kuchimba katika maeneo yao kwa rushwa iliyofanywa na huyu bwana Mbogo. Je Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha inawazuia wawekezaji wa aina hii wanaotumia rushwa kuhodhi maeneo katika eneo la uchimbaji na huku vijana wakihangaika kupata ajira? Uwekezaji huu wa aina hii wenye lengo la kuwatesa wananchi pamoja na hali ngumu waliyo nayo usimamiwe ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ubadhirifu wa Kiwanda cha Kukoboa na Kusaga. Mashine hii ilinunuliwa na Halmashauri ikayeyuka, ilikuwa na thamani ya milioni mia moja lakini leo hii wananchi wakihoji hawapati majibu ya wizi huu wa wazi kabisa. Je Serikali hii kwa kuendelea kuwalea wezi wanaokula fedha za viwanda vya uwekezaji katika Manispaa ya Mpanda kwa kutochukua hatua yoyote hamuoni kwamba mnapoteza fursa za vijana kwa kuwalea wabadhirifu hawa bila kuwachukulia hatua?

Mheshimiwa Naibu Spika, uchumi wa viwanda uendane sambamba na ukuaji wa sekta ya nishati na umeme. Je ni mkakati gani wa haraka wa kuuhakikishia uchumi wa viwanda upatikanaji wa umeme unaoenda sambamba na mazingira ya uwekezaji sawia nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya CCM bado haijajipanga pia kujiendeleza kiuchumi kupitia viwanda. Bajeti yenye asilimia 0.36 ya pato hili, je, Wizara hii imejipanga kweli kuwasaidia wananchi au utani?