Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora kwa mwaka wa fedha 2016/2017

Hon. Anna Joram Gidarya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora kwa mwaka wa fedha 2016/2017

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kabisa, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia lakini pia ni mara yangu ya kwanza kuingia katika jengo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, ndugu zangu naomba nitangulize neno la utangulizi. Naomba tujifahamu kwamba sisi ni Wabunge lakini utumishi wetu unalenga nini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie maeneo machache na kwanza naomba nianze na afya. Katika hili kabrasha nimesoma pesa zilizowekwa kwa ajili ya on call hasa kwa Mkoa wangu wa Manyara, Babati TC hazitoshi kabisa. Pesa hizi ni kidogo sana ukizingatia idadi ya madaktari waliopo. Babati TC ina daktari mmoja wa anesthesia, sidhani kama huyu daktari mmoja anajitosheleza na hii on call.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni eneo la elimu. Babati TC ina takribani shule za sekondari zisizopungua 36 lakini tuna walimu wa masomo ya sayansi wachache mno. Shule moja ina mwalimu mmoja wa masomo ya sanyansi, kwa wiki ana vipindi 49, sijui mwalimu huyu anajigawaje katika maandalio ya somo na mpaka hatua ya kukamilisha hii kazi ya kuwafundisha wanafunzi. Tuna upungufu mkubwa sana wa walimu, kuna shule zilizopo maeneo ya mijini walimu wamerundikana humo kwa kigezo cha afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Waziri mwenye dhamana ya Wizara ya Afya walimu hao wapimwe. Walimu wengine wa vijijini wanapiga mizigo, siku nzima mwalimu halali mpaka saa kumi na mbili lakini muda wa kazi uliopangwa unajulikana. Kwa nini wengine wawe wana kula bata mjini na wengine wapo vijijini wanakula mzigo, haiwezekani! Namshauri Waziri mwenye dhamana hii walimu hao wapimwe. Mfano mzuri ni shule ya Babati Day, kuna walimu zaidi ya 22 wamerundikana pale lakini shule za pembezoni hazina walimu na tunasema elimu bora, tutaipataje?
Mheshimiwa Naibu Spika, niende sasa kwenye utawala bora. Mkoa wa Manyara kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi ambayo chanzo chake ni watawala wakuu wa maeneo hayo husika. Kwa nini nasema hivyo? Eneo lenye migogoro mikubwa ya ardhi ni maeneo yenye hifadhi mfano Galapo. Eneo hili watawala wana maeneo, imagine Mkuu wa Mkoa ana hekari 400 halafu Mkuu huyo huyo wa Mkoa ndiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, anasuluhisha nini? Anaendaje kwanza ku-face wale wananchi wenye matatizo? Mkuu wa TANROAD ana heka 500, RPC ana heka 300, leo hii mnawahamisha wale watu mnawapeleka wapi, inawezekanaje? Tumejibeba mno kuliko wale wadhaifu ambao wametuweka sisi tuwatawale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba Waziri wa Ardhi aende Galapo, akinihitaji mimi anitafute nitampeleka na nitamuonyesha hayo mashamba. Mwezi wa pili tulienda na Naibu Waziri wa Maliasili kuangalia mipaka ya watu wa Ayamango, wanampeleka sehemu ile ambayo haitakiwi, kisa wanajificha. Waziri wa TAMISEMI, nakuomba baba yangu kawamulike Wakuu wa Mikoa. Iweje mimi niteuliwe kuwa Mkuu wa Mkoa halafu miezi mitatu, minne tayari nina heka 200, nimepewa kwa sababu nimefanya kazi gani, lazima tujiulize. Mnasema migogoro haiishi, migogoro ya Manyara ni ya muda mrefu ni kwa sababu watawala wakija wametanguliza mikono. Unachukua hapa, unapeleka pale halafu wewe ndiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama. Waziri akija anapapaswa huko anaambiwa maneno mengi, ndiyo imeshatoka hivyo. Tunaomba twende kwa wale wadau wa ngazi ya chini tujue matatizo yao yako vipi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende eneo lingine la kilimo. Kumekuwa na Maafisa Kilimo na Maafisa Mifugo kazi yao wanayojua ni pembe za ng‟ombe zikiota akakate, hakuna kutoa elimu, hakuna kuhangaika watu wake wafuge vipi. Hapa mmeandika mafunzo, haya mafunzo kwa nini msiyafute kama wao hawataki kujituma? Tumekuwa wavivu wa kufikiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna huu mradi wa ng‟ombe wa TASAF hawaelekezwi hata nini wafanye. Kazi yao ni kuwaambia jenga banda, lakini kuna mifumo mingi ya ufugaji, sisi wengine ni wajasiriamali tumetoka huko. Kuna mfumo wa kufuga kisasa huhangaiki na malisho ya ng‟ombe wala huhangaiki kumtafuta kijana wa ngo‟mbe. Unafunga vyombo vya kisasa ng‟ombe wako anakula, anakunywa maji na kwa kiwango. Watu hawa wamekaa kazi yao ni kuomba vibustani huko kwenye mashamba ya watu. Wako watu kule Magugu wamekaa ni Maafisa Kilimo na wao wana mashamba kawamulike Afisa Ardhi nakuomba.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine la mwisho ni barabara. Miundombinu yetu ni michafu. Tuna kilio cha muda mrefu, tuna barabara inayotoka Mbuyuni – Magara, tuna eneo linalohitaji daraja. Rais wa Awamu ya Nne, huyu aliyemaliza muda wake alituahidi mwaka 2010, sasa sielewi daraja lile linafanyiwa uchunguzi wa aina gani miaka kumi iliyopita? Mpaka sasa daraja hilo limekuwa kikwazo kwa watu wanaotoka Mbulu kuja Arusha, kuja Babati na maeneo yale ya Magara. Mheshimiwa Waziri, tunakuomba utusaidie lile daraja ni muhimu kwa watu wa Mbulu Mjini na Babati Vijijini. Tunaomba miundombinu hii ya daraja ikamalike kwa sababu ni ahadi ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema, ndugu zangu utawala siyo kutawala kwa mabavu, tunatakiwa tutawale kwa hekima. Tujiulize kwa nini watu kwenye Majimbo yao wakulete wewe hapa uwe Mbunge, uwawakilishe, una nini hasa wewe, una nini ulichowazidi, una elimu au, hapana, ni Mungu amekupanga uwe mtawala wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tusitumie utawala wetu vibaya. Wako waliotumia utawala vibaya na wameanguka. Hatuhitaji tuanguke kwa sababu utawala unatoka kwa Mwenyezi Mungu, tutawale kwa hekima. Tumegeuza huu ukumbi kama chumba cha ku-debate, kila siku ni debate hapa, ni taarabu hapa sasa haieleweki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ndugu yangu Mheshimiwa Nape mimi nakujua wewe ni kaka yangu, tumefanya kazi sana nikiwa CCM, kwa hiyo, nakuomba wakati mwingine kuna uhuru, huu uhuru uuachie, hautakukwaza wewe, cha msingi ni kutengeneza sheria ya huu uhuru unatumikaje lakini tuki-debate humu ndani hatutasogea. Huu siyo utawala, kwanza turudi tujiridhishe katika maandiko, maandiko yanasema aliyeteuliwa kuwa mtawala ni Mwenyezi Mungu mwenye ametaka awe mtawala, sasa tusitumie hivi vipaji vibaya. Hakuna aliye zaidi ya mwenzake hapa, wote tumetokana na Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba kaka yangu Mheshimiwa Nape suala la vyombo vya habari uliachie. Siyo kwa maslahi ya hawa Wabunge wa Upinzani ni kwa maslahi ya Watanzania na kwake pia ili tuwe na mbio ambazo zinaelezeka. Tusikimbie mbio ambazo sio zetu, ukichagua mbio ukimbie mbio zako mwenyewe, hizo mbio kaka yangu siyo za kwako zitakudondosha njiani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema ahsante.