Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi siku ya leo kuweza kuchangia kwenye Wizara hii ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi leo, kwanza ninamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mheshimiwa Waziri kwa jitihada mbalimbali zinazofanyika katika kuhakikisha kwamba Tanzania ya viwanda inafikiwa. Pia ninashukuru kwa sababu dhana hii inapozidi kuzungumzwa sana, mwisho wa siku inatafsirika na watu wanaamini na wanaingia katika uwekezaji wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa sababu hiyo Mheshimiwa Waziri mimi nijielekeze, najua unajua nikisimama kuzungumzia kiwanda siwezi nikazungumza mambo mengine nikakiacha kile kilichopo pale kwangu Manonga, Manonga Ginnery. Mheshimiwa Waziri toka nimekuwa Mbunge na siku yangu ya kwanza kuzungumza ndani ya Bunge, nimezungumzia suala la Kiwanda cha Pamba ndani ya Wilaya yetu ya Igunga. Kiwanda hiki ni cha zamani sana, toka enzi za mkoloni mpaka juzijuzi kikabinafsishwa akapewa Rajan, Rajan amekiendesha mpaka na yeye akakishindwa akakiacha, amefikia hatua amefariki, amemuachia mtoto wake, mtoto wake yuko Uingereza mara sehemu mbalimbali. Tumezungumza tukakwambia wapo Igembensabo wanakitaka hiki kiwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda hiki asilimia 80 anamiliki Rajan, asilimia 20 anamiliki Igembensabo. Igembensabo anataka kukinunua hiki kiwanda, ameweka mezani shilingi milioni 500 lakini Rajan amekinunua shilingi milioni 700 anataka kukiuza shilingi 1,500,000,000, kiwanda kimesimama anataka kukiuza kama vile kinafanya kazi, kinaingiza faida na huyu ni mbia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, lakini tulikuomba uwakutanishe hawa watu wakae chini, wao wako tayari. Umetuahidi mara nyingi hawa watu utawakutanisha wakae chini wazungumze Igembensabo yuko tayari, hata wao wako tayari, issue yako kama Waziri ni kuwaita hawa ofisini kwako. Juzi juzi hapa katika majibu umesema umefanya jitihada mbalimbali, umetuambia kwamba huyu mtoto wa Rajan yuko Uingereza anakuja baada ya miezi sijui sita au saba, anachelwa. Hivi Serikali hii ya Dkt. John Pombe Magufuli ikitaka kumuita huyu kijana itashindikana kweli? Yaani akakae Uingereza na kiwanda chetu huku, kama hataki kukiendeleza si akiachie wapewe watu wengine waweze kuki-run? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi siamini kwamba Serikali hii imeshindwa kumuita, haiwezekani na siamini. Inawezekana, labda Mheshimiwa kwa sababu wewe unasema unapiga-sound inawezekana na mimi kijana wako unanipiga sound, nielewe kwamba hiyo ndiyo sehemu ya kupigana sound, lakini mimi siamini kwamba wewe zile sound unazosema unapiga unamaanisha kwamba unanipiga sound kweli. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, hebu muite huyu kijana ikiwezekana, kama inashindikana si mkitaifishe sasa, mmeshamuita amekataa. Inawezekana hamjamtafuta na wao wako tayari kuja. Mheshimiwa Waziri tunakuomba, na Mbunge mmoja wa Simiyu amesema eti zao la pamba limekufa, si kweli, halijafa, uzalishaji wake umepungua na si kufa. Maana yake ukisema kufa maana yake watu hawalimi kabisa, haiwezekani, kulima tunalima ila si katika kiwango ambacho Serikali ama nchi inataka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kweli uzalishaji wa pamba umepungua si tu katika eneo letu la Wilaya ya Igunga ama Simiyu, katika nchi yetu ya Tanzania uzalishaji wa pamba umepungua; na Serikali haijawekeza vya kutosha na kama hivyo viwanda, ginneries zipo nyingi zimetajwa, na moja wapo ya ginneries kongwe hii ya Manonga ni ginnery kongwe. Katika Mkoa wa Tabora ukizungumza Manonga hakuna ambaye hajui, hakuna Rais ambaye hajui ginnery hii, lakini sijaona Serikali ama Waziri ukiwekeza katika kuhakikisha kwamba kiwanda hiki kinafanya kazi. Waweke chini hawa watu wafanye mazungumzo, watauziana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wetu wa Tabora uangalie hizi fursa. Sisi tunalima sana maembe Mkoa wa Tabora, tuna nyuki, tumbaku, ngozi nyingi sana, hasa kwa sababu tuna ng’ombe wengi. Hivi Mheshimiwa katika makabrasha haya hauhamasishi katika uwekezaji huku kwetu? Maana kila siku ninasikia tulikuja mpaka airport wawekezaji wameondoka tena, hivi wawekezaji wa kuishia airport kweli? Hawa walikuwa wawekezaji au wasanii?

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe Mheshimiwa Waziri, hebu sukuma hili jambo ili kila mkoa uwe na fursa maana ukizungumza viwanda hapa vingi viko pwani na sisi huko kwetu Bara tunahitaji viwanda hivi vije, maana viwanda vikiwepo vitapunguza msongamano wa vijana kuwepo Dar es Salaam. Ndiyo hii unasikia kila siku Dar es Salaam vijana wanavuta bangi, wanavuta dawa za kulevya, hizi vurugu zote zipo Dar es Salaam huko na miji mingine huku kwetu haipo katika kiwango hicho. Hebu tuletee hivi viwanda huko vijana wasikimbie vijijini ama wasikimbie wilayani wakakimbilia mikoa ya pwani huko. Hii itasaidia sana kwa sababu leo hii wanabaki bibi zetu kule nyumbani kwetu wanaonekana vikongwe hawa ama wachawi. Hebu muache kuleta hii dhana, leteni hivyo viwanda ili kupunguza, vijana wawepo wawasaidie wazazi wao, waendeleze maisha na itasaidia kuokoa maisha yetu katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata hili suala la ngozi limekuwa linazungumzwa sana. Ni kweli tunataka tuwe na viwanda vya ngozi ndani ya nchi yetu, sasa ngozi imekuwa nyingi kiasi kwamba wanunuzi hawapo. Tumeweka kodi ku- discourage ku-export ngozi yetu nje ya nchi, lakini sasa hawa ambao tulionao viwanda vyetu havitoshelezi kununua ngozi, mwisho wa siku ngozi zinabaki kwenye machinjio, watu wananunua wanaacha katika maeneo yao. Hebu tupunguze kodi ama tuwa-encourage hawa watu ili kama tumeshindwa kununua ngozi yote badala ya kuharibika wai- export tupate hizo dola ambazo zinatoka nje ya nchi ziingine ndani ya nchi yetu. Mheshimiwa Waziri nafikiri hilo utakuwa umelisikia na utawasaidia hawa wafanyabiashara wa ngozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine mimi ninalotaka kulizungumzia ni hii issue ya One Stop Center. Leo tunaona mtu anapokuwa na kiwanda chake wanakuja watu wa OSHA, NEMC, madubwasha yako mengi. Kwa nini isiwe kwamba mtu yeyote anayetaka kuanzisha kiwanda aende sehemu moja, kama ni TRA alipie madubwasha yote, yeye pale apewe karatasi au sticker moja ambayo ndani yake yumo OSHA, NEMC, TRA na watu wote ili akija mtu wa NEMC iwe ni kujiridhisha tu. Sasa mtu ana kiwanda anaki-run, siku mbili anakuja OSHA anampiga faini anamwambia funga kiwanda, mtu amewekeza kwa gharama kubwa halafu anaambiwa funga kiwanda. Hebu tuwe sehemu ya ku- encourage viwanda vyetu na tuwe sehemu ya kuwasahihisha wenye viwanda ili waweze kuendelea kufanya hii kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi viwanda vinasaidia kutoa ajira kwa vijana wetu na hii inasaidia kupunguza tatizo la vijana mitaani. Unapo-discourage watu wa viwanda unasababisha hawa vijana warudi mtaani wanageuka majambazi, wanageuka vibaka na hatimaye hawa hawa wanageuka kuwa watu ambao si watu wema katika jamii. Tuombe Serikali iwasaidie wenye viwanda hata kama wana matatizo ninyi muwe sehemu ya kutatua matatizo yao na msiwe sehemu ya kuzuia kufanya miradi au kazi zao. Niombe Wizara, nafikiri mtakuwa mmelisikia hilo; naomba sana muwasaidie wafanyabiashara, maana yake tafsiri ya mfanyabiashara sijaelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninachojua, mfanyabiashara ni Mtanzania yeyote ambaye anaanza kutafuta kipato chake, mkulima ni mfanyabiashara. Kuna mkulima gani ambaye anazalisha chakula halafu asikiuze? Huyo si mfanyabiashara. Mkulima ni mfanyabiashara kwa sababu anazalisha, anauza. Mwalimu anafundisha, ama sisi Wabunge hapa, wengine tuna hoteli, tuna guest houses, tunafanya biashara, maana biashara ikiharibika mpaka kwenye hoteli zetu biashara zinaharibika huko. Humu ndani ya Bunge katika asilimia 100, asilimia 99 ni wafanyabiashara, tunatofautiana biashara gani tunafanya. Unaweza ukawa Waziri ukawa mfanyabiashara. (Makofi)

Suala lingine kabla sijafika mwisho, nafikiri muda wangu utakuwa si rafiki; kuna mtu alichangia jana hapa akasema Rais wa Kenya amepata chakula kutoka Mexico na chakula kile kinagawiwa kwa bei ya kutoka shilingi 3,000 ya Tanzania kwa maana ya Kenyan shilings 150 kupunguza kwa shilingi 90 ya Kenya sawa na 1,800 ya Tanzania. Hivi kwa saa 24 inawezekanaje Rais akatoa tangazo halafu bei ikashuka kwa kiwango hicho, inawezekana kweli au tunaleta propaganda ndani ya Bunge hili?

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba hata kule alikosema kwamba ametoa chakula kile, Mexico, kwanza tutambue, Kenya sasa hivi kuna Uchaguzi Mkuu, Uchaguzi Mkuu ni pressure kwa Rais aliyepo hata kwa wapinzani. Kwa hiyo kinachofanyika ndani ya nchi ya Kenya ni siasa, tunachozungumza leo Balozi wa Mexico amekanusha amesema kile chakula hakijatoka Mexico, kwa hiyo tusidanganyane. Mtu analeta taarifa za kutoka huko anasema kwamba eti Kenya wameshusha bei ya chakula, chakula kingi kiasi kwamba…, tuzungume ukweli pale ambapo panastahili ukweli… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja.