Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Raphael Michael Japhary

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia kwenye Wizara ya Viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuna hoja ambayo imekuwa-raised kwamba inawezekana ndoto yetu ya kufikia Tanzania ya viwanda ina mashaka makubwa. Lakini imeonekana kama vile ni uchokozi ambao upande mwingine haukuutaka. Lengo la Kambi ya Upinzani kuonyesha wasiwasi wetu kwa dhana hii kufikiwa, ni vizuri Serikali ikalichukulia hili kama changamoto na isiwe ni sababu ya kuanza kuleta malumbano yasiyo ya lazima.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1967 Tanzania ilishaanza hatua hizo za kujijenga katika dhana mzima ya Industrial Revolution na bahati mbaya tulienda na dhana hiyo tukiwa na mtu ambaye ni dedicated ambaye alikuwa Rais wetu wa Kwanza wa nchi hii. Hata hivyo mwaka 1996 dhana ile tuliiua wenyewe. Na bahati nzuri mwaka 1996 kwa lengo hilo la ubinafsishaji tulikuwa na dhamira kwamba tunaweza tuka-develop zaidi kama tutakuwa tume-adopt vizuri dhana ya ubinafshaji ambayo bahati mbaya hatukuweza kuifanyia kazi vizuri. Sasa wasiwasi wetu ni kwamba kama Sustainable Industrial Development Policy ya tangu mwaka 1996 mpaka leo haijaweza kufanya kazi vizuri, nini miujiza ya kuifanya kwa miaka mitano? Ndio wasiwasi wetu. Sasa nafiki ni vizuri tungeichukua kama changomoto muhimu sana Serikali ilituweze kuifanyiakazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa kipindi hicho vikwazo vilivyokuwa vinakabili sekta ya viwanda ndiyo ambavyo viko sasa, tangu 1996. Wachambuzi waliokuwa wanatunga hii Sera ya Sustainable Industrial Development Policy waliona kwamba tuna vikwazo vya unfavorable legal and regulatory framework ambazo zilikuwa ni kikwazo kimojawapo, limited access of SMEs to finance, cha pili; cha tatu kilikuwa infective and poor coordinated institutional support framework; vitu ambavyo mpaka leo tunavizungumza kwamba ni tatizo katika nchi hii.

Sasa lazima tuone kwamba tuna mahali ambapo panatukwamisha na kwa pamoja tufikiri namna gani tunatoka hapa kwenda mbele ili tufikie hiyo ndoto ya Tanzania ya viwanda. Kwa hiyo ni vizuri mkaichukua kwa uzito wake hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la pili ambalo linafanya tuone mashaka ya viwanda ni soko letu la ndani. Tuna soko la ndani la kiwango gani. Nini uwezo wa watu wetu kununua katika soko letu la ndani, purchasing power yetu. Ukizingatia kwamba viwanda anavyovihubiri Mheshimiwa Waziri ni viwanda vidogo sana vyenye kuajiri mtu mmoja mpaka watu watano; viwanda vidogo vinavyofuatia vyenye kuajiri watu watano mpaka watu 49 na viwanda vya kati vyenye kuajiri watu 49 mpaka 99.

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda hivi vinatengemea sana soko la ndani, soko ambalo hatuna kwa sababu Serikali ya Awamu ya Tano imechukua fedha zote ambazo zilikuwa za Serikali ikaziamishia Benki Kuu na ni sawa tu na hadithi ile ya mtu aliyechukua rupia akaifukia chini ya ardhi. Haiwezekani uchukue fedha zile ambazo zilikuwa kwenye mzunguko uzipeleke benki ukiamini ndio uwekezaji.

Kwa hiyo, matokeo yake tumepunguza sana mzunguko wa fedha katika uchumi wetu, tumepungusa uwezo wa uwekezaji katika uchumi wetu na kwa misingi hiyo purchasing power ya watu imepungua, sasa kwa hawa watu wanaozalisha wanakwenda kumuuzia nani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndio leo tunaambiwa kwamba kuna hata soko la kuuzia bidhaa za kiwanda cha bidhaa za kupambana na malaria zimekosa soko kwa sababu hatuna soko la ndani. Sasa tunafikiaje haya malengo? Hili ndilo suala la msingi la kujadili kwa pamoja ili tuone tunavyoweza kufikia lengo la kuwa na Tanzania ya viwanda. Kwa hiyo ni vizuri tukayachukua haya masuala kwa uzito wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara wa ndani kama wengi walivyosema hawana mazingira rafiki ya kibiashara, kuna vitu vingi vya kuwakwaza, ni lazima tuviangalie, tuwapende wafanyabiashara wa ndani. Wafanyabiashara wa ndani tunawaumiza, tunaonekana kama hatuna haja nao, tunaonekana kuvutia zaidi wafanyabiashara wa nje ambao hata wenyewe hatuna vivutio vya kutosha vya kuwavutia.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni vizuri tuone namna gani tunajiweka vizuri katika maeneo hayo ili tufikie katika dhana ya Tanzania ya Viwanda. Kila mtu anaona uthubutu wa kufikia hiyo dhamira ya kuwa na Tanzania ya Viwanda iliyoonyeshwa na Serikali hii, lakini lazima sasa tuone tunafikaje katika hatua hiyo kwa pamoja wote kama Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la Mkoa wa Kilimanjaro. Mkoa wa Kilimanjaro ulikuwa na viwanda zaidi ya 15, leo hakuna kiwanda kinachofanya kazi ukiondoa Kiwanda cha Bonite peke yake. Sasa nataka Mheshimiwa Waziri aniambie ni lini atahakikisha Kiwanda cha Madawa ya Mimea kinafanya kazi? Kiwanda kile kimewekeza fedha za Watanzania nyingi mno za mikopo lakini kiwanda kile hakuna siku kimefanya kazi na Watanzania wanadaiwa madeni kutokana na fedha ambazo Serikali hii ilikopa lakini kiwanda kimekuwa pale ni white elephant haifanyi kazi yoyote mpaka leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri aniasaidie ni lini kiwanda kile kitafanya kazi? Ni lini Kiwanda cha Machine Tools kitafanya kazi? Kiwanda ambacho katika zama za Mwalimu Nyerere kilikuwa ni kiwanda mama kama vilivyokuwa viwanda vya chuma vya Tanga. Kama ninavyozungumzia Liganga na Mchuchuma, lakini leo kiwanda kile hakifanyi kazi, na ni kiwanda ambacho kilikuwa ni cha tatu katika Afrika, lakini leo hakifanyi kazi; na mnaimba Tanzania ya viwanda, mnafikiaje hilo lengo la kufika Tanzania ya viwanda kama kiwanda mama hamuwezi kukifanya kikafanya kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nilikuwa najiuliza kiwanda cha magunia Mheshimiwa Waziri umeorodhesha kwenye hotuba yako Kilimanjaro viwanda vimebinafsishwa havifanyi kazi. Bahati nzuri Mheshimiwa Rais ameonesha dhamira kwamba anataka Tanzania ya viwanda, kuna kigugumizi gani cha kuwanyang’anya wale watu viwanda ambao hawavifanyii kazi? Nini kigugumizi cha Serikali? Kwa nini hapo mnakosa uthubutu wa kufanya maamuzi magumu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama watu wamechukua viwanda tangu mwaka 1996 mpaka leo hawavifanyii kazi, ni kwa nini mnapata vigugumizi ya kuchukua vile viwanda? Kiwanda cha Magunia kilichokuwa kikiajiri watu wa Kilimanjaro leo hakifanyi kazi, kimekuwa godown la kuwekea bidhaa, kwanini tunawalea hawa watu na nyie mnaona ni jambo la kawaida. Bahati mbaya kuliko vitu vyote Serikali yenu haifanyi kazi kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa Moshi tumegundua kwamba hamtaki kufufua vile viwanda. Tumeanzisha mipango yetu ya kujiendeleza wenyewe, tumetaka kujenga stendi ya kisasa pale ya kushindana na soko letu lakini mpaka leo Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI hataki kutupa kibali, kwa nini? Kwa sababu ni eneo la upinzani ama sababu ni nini? Tumeomba kwamba Moshi iwe Jiji ina sifa zote, lakini leo tunanyimwa kwa nini? Sasa mtakuzaje huu uchumi na mnafikaje Tanzania ya viwanda? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilikuwa nafikiri ni vizuri kama kuna lengo la kufikia Tanzania ya viwanda tuone tunafikaje huko, lakini kuanza kuhujumiana kwa sababu za kisiasa ni jambo la ajabu sana. Kama hamtaki huu mfumo wa vyama vingi vya siasa futeni ili wengine tukafanye biashara zetu zingine kwa sababu hatuwezi kuja hapa kuwawakilisha wananchi, tujenge mawazo ambayo ni constructive halafu myakatae unnecessary bila sababu yoyote ya kimsingi, kwa nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa natamani sana nione mlivyo-link katika suala la kufikia Tanzania ya viwanda, namna gani mnamsaidia Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Bashe amewaambia na Mheshimiwa Zitto amewaambia; namna gani mnamsaidia Rais ili ndoto yake itimie. Otherwise mtazungumza kama ilivyozungumzwa tangu mwaka 1967, mtazungumza kama ilivyozungumzwa tangu 1996 mpaka leo na mtazungumza mpaka miaka mingine 40 ijayo mbele hamuwezi kufikia Tanzania ya viwanda. Hatutaki kwamba mfike hapo, hii nchi ya kwetu wote, tunataka tu-achieve lengo la kuwa na Tanzania ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lazima na nyie mheshimu mawazo ya watu wengine muone kwamba wanaweza wakafanya. Lengo la viongozi ni kuwa wabunifu, ziacheni Halmashauri Madiwani wabuni mipango yao na muwape support Madiwani. Acheni kule chini wafanyabiashara wafanye biashara zao vizuri, waacheni wamachinga wa-develop ili dhana ya SME ifanyike. Sasa msipoyafanya haya mnaifikiaje Tanzania ya viwanda? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimependa kuyaonesha haya kwamba Kilimanjaro tuna shida. Kiwanda cha Ngozi leo kinazalisha kidogo; Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira itusaidie kuhakikisha kwamba kile kiwanda kinatumia teknolojia ya kisasa; watu pale wanaumia kwa harufu ya kile kiwanda. Sasa hatutaki kifungwe kwa sababu hatuna viwanda, lakini tunataka kilazimishwe kuzalishwa ka teknolojia ya kisasa ili kulinda afya za watu wa Moshi maana kuna watu pale wanapata maradhi, mtawalipa na nini na mtawafidia kwa kitu gani kwa roho za? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilikuwa naomba sana ichukuliwe kwamba lengo letu ni jema na ni la msingi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunakuwa na Tanzania ya Viwanda kweli.