Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

Hon. Dr. Hussein Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu jioni ya leo ili niweze kuhitimisha hoja yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia katika hoja hii na michango ilikuwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, waliochangia kwa maandishi ni Waheshimiwa Wabunge 38 na waliochangia kwa kuzungumza ni Waheshimiwa Wabunge 21.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee naomba niishukuru kwa dhati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa Balozi Adadi Rajabu kwa ushirikiano wao mkubwa katika kutekeleza mambo ya kikanuni kama ilivyoainishwa katika kanuni za Bunge, Toleo la Januari, 2016 kupitia masuala yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza walitembelea miradi ya maendeleo chini ya Wizara yangu; pili, walifanya tathmini ya utekelezaji wa mipango ya bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, walifanya uchambuzi wa makadirio kwa mwaka wa fedha 2016/2017; na mwisho, walitoa maoni na ushauri wa Kamati ambayo yalitolewa kwa kuzingatia uchambuzi wa mambo yaliyozingatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Kamati katika maoni yake kuhusu miradi ya maendeleo kutopatiwa fedha kadri ya makadirio na hili limekuwa ni changamoto kubwa kwetu. Tunaendelea kuwasiliana na Wizara ya Fedha na Mipango ili kuona kwamba miradi hiyo inapatiwa kipaumbele kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha 2016/2017. Tatizo kubwa kwa muda mrefu limekuwa ni ufinyu wa makusanyo na kipaumbele kwa matumizi ya Serikali na vipaumbele mbalimbali vinavyoikabili nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama ilivyo ada, naomba nianze kujibu baadhi ya hoja ambazo zimetolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja ya kwamba Serikali iyapatie mafungu ya Ngome JKT na Wizara, fedha zote za maendeleo kwa mwaka wa 2016/2017. Kulingana na upatikanaji wa fedha zinazotokana hasa na mapato ya ndani, Serikali imekuwa ikitoa fedha za maendeleo kwa Wizara ili kuweza kutekeleza shughuli za maendeleo. Mfano, hadi kufikia mwezi Machi, 2017 Wizara ilikuwa imepokea jumla ya shilingi 35.9 bilioni sawa na asilimia
14.5 ya bajeti ya maendeleo. Kumekuwa na mawasiliano kati ya Wizara yangu na Hazina kuhusu Wizara kupatiwa fedha za maendeleo zilizobakia ili kukamilisha utekelezaji wa mipango yake ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni Serikali itoe shilingi bilioni 27 zilizotengwa mwaka 2016/2017 kwa ajili ya kulipia maeneo yaliyochukuliwa na Jeshi kabla ya terehe 30 Juni, 2017. Katika mwaka wa fedha 2016/2017, Wizara ilitenga shilingi bilioni 27.7 kwa ajili ya kupima na kuwalipa fidia wananchi ambao maeneo yao yalitwaliwa kwa matumizi ya Jeshi. Hata hivyo, fedha hizi bado hazijatolewa hadi kufikia mwezi Machi, 2017. Wizara imekuwa ikiwasiliana na hazina kuhusu kupatiwa fedha kwa ajili ya kutekeleza shughuli za maendeleo ikiwemo fedha kwa ajili ya fidia za ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadaye nitatolea maelezo yale maeneo yote ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyazungumza kwa uchungu kabisa kuhusu fidia kwa maeneo yaliyochukuliwa na Jeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ni kwamba Serikali ipime ardhi inayomilikiwa na Jeshi na kuimilikisha kwa Jeshi Kisheria. Kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya mwaka 1999, hakuna kipengele cha utoaji wa hatimiliki kwa Taasisi za Serikali likiwemo Jeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, mazungumzo yanaendelea kati ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa na Mamlaka husika ili hatimaye maeneo yote ya Jeshi yapewe hatimiliki bada ya kuzifanyia marekebisho Sheria hizo. Serikali kupitia Wizara husika na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, inaendelea na taratibu za kuibadilisha Sheria ya Ardhi Na. 4 na 5 ya mwaka 1999 ili kuziwezesha Taasisi za Umma likiwemo Jeshi kumilikishwa maeneo kwa hatimiliki ili kuondokana na utaratibu wa sasa wa kusajiliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la Sera na Sheria ya Ulinzi; Kamati ilitaka Serikali ikamilishe mchakato wa kufanya marekebisho katika Sheria ya Jeshi la kujenga Taifa, Sura ya 193 na Sheria ya Ulinzi wa Taifa, Sura ya192 ili iweze kuendana na wakati, mifumo ya utawala na mahitaji ya sasa ya Kisheria katika Sekta ya Ulinzi.

Mheshimiwa mwenyekiti, kwa kuwa suala la Sera ya Ulinzi wa Taifa ni la Muungano, kukamilika kwake kunategemea ridhaa ya pande zote mbili za Muungano. Hatua iliyofikiwa kwa sasa ni kupata maoni kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, marekebisho ya Sheria ya Ulinzi wa Taifa na Sheria ya JKT yatafanyika baada ya kukamilika kwa Sera ya Ulinzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili, napenda nilieleze Bunge lako Tukufu kwamba tumefikia sehemu nzuri sana, nimefanya mazungumzo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulika na vikosi vya SMZ kule Zanzibar na ameniahidi kwamba sera hii sasa inakaribia kupata maoni ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili tuweze kukamilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni Serikali ione muhimu wa suala la fidia kwa vijana wanaopata ulemavu wakiwa katika mafunzo ya JKT. Napenda kuliarifu Bunge lako kwamba malipo ya fidia hufanyika kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taifa ya mwaka 1966 ambapo mapendekezo ya marekebisho ya Sheria tajwa yatafanyika baada ya kukamilika kwa Sera ya Ulinzi wa Taifa. Kwa sasa, kijana analipwa fidia kwa kutumia kiwango cha mshahara wa Askari wa cheo cha Private kwa mwaka wa kwanza. Maana yake ni kwamba vijana wanaokwenda JKT wakiumia, siyo kwamba hawalipwi fidia, wanalipwa fidia kwa kutumia kigezo hiki cha kwamba tunawalipa sawa na aliyeajiriwa katika ngazi ya Private anapokuwa ni mwaka wake wa kwanza Jeshini. Kwa hiyo, fedha hizi huwa wanazipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni Serikali itoe kipaumbele kwa vijana waliopitia mafunzo ya JKT wakati wa kuajiri vijana kwa ajili ya shughuli za ulinzi katika Shirika la SUMA JKT. Hivi ndivyo hasa ilivyo. Napenda kutoa taarifa kwamba SUMA JKT Guard Limited linatoa kipaumbele kwa vijana waliopitia mafunzo ya JKT wakati wa kufanya ajira zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni Serikali iboreshe miundombinu ya kambi za JKT ili vijana wengi kwa mujibu wa Sheria waweze kufanya mafunzo hayo na kutenga fedha kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa mafunzo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inaendelea kuwasiliana na Mamlaka husika ili kuona uwezekano wa kuongeza fedha kwa mafunzo hayo kadri hali ya kifedha itakavyoruhusu. Sisi sote tunapenda kwamba vijana wote wanaokamilisha masomo yao ya kidato cha sita waweze kuingia Jeshini kwa mujibu wa sheria kabla hawajaendelea na elimu ya juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu eneo la madeni, Kamati imeitaka Serikali ilipe madeni ya Wazabuni na madeni ya Kimkataba. Serikali ione umuhimu wa kuongeza kasi ya kulipa madeni yote ya Wizara yaliyohakikiwa kiasi cha shilingi bilioni 212.3. Maelezo ni kwamba kiini cha madeni ya Jeshi ni ufinyu wa bajeti katika maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa majukumu ya kijeshi. Jumla ya madeni yaliyohakikiwa na ambayo yanapaswa kulipwa ni shilingi bilioni 95.6. Mpaka sasa Serikali imechukua hatua ya kuanza kulipa madeni hayo ambapo imetoa shilingi bilioni 5.16. Aidha, madeni ambayo hayajalipwa ni shilingi bilioni 90.4.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara katika mwaka wa fedha 2016/2017, imelipa shilingi milioni 61.2 kwa ajili ya malipo ya Wazabuni wa ndani ambao wametoa huduma mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa upande wa Wazabuni wa nje Wizara imelipa shilingi bilioni 30. Aidha, Wizara inadaiwa deni la kimkataba, mikataba mbalimbali kiasi cha shilingi bilioni 785.2. Kwa hiyo, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Wizara imekasimia shilingi bilioni 120.7 kwa ajili ya kulipa madeni ya kimkataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fungu 39 la JKT jumla ya madeni ya fungu hili hadi kufikia mwezi Aprili, 2017 ni shilingi bilioni 101 na madeni yaliyohakikiwa ni shilingi bilioni 79.8. Serikali imeweza kulipa shilingi bilioni 4.2, hivyo kufanya deni hilo lililohakikiwa kubaki shilingi bilioni 75.6.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kuhusu SUMA Guard ilipwe madeni yake na wale ambao wamepewa huduma naye. Tumepokea ushauri wa Kamati kuhusiana na Kampuni ya SUMA JKT Guard Limited, kampuni itaendelea kufuatilia madeni kwa washitiri wake kwa kutumia Wakala wa kukusanya madeni na kuimarisha kitengo chake cha ukusanyaji madeni kwa ajili ya kufuatilia na kuwakumbusha wateja wake kulipa madeni yao.

Mheshimiwa Mwenyeki, kuhusu Mashirika ya Jeshi; Kamati imetaka Shirika la Mzinga kumilikiwa kisheria na kuwajibika chini ya mamlaka moja. Shirika la Mzinga ni Taasisi iliyo chini ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, lakini kama taasisi nyingine za Serikali au za Umma, linawajibika kuwa kwa Msajili wa Hazina vile vile. Wizara itashughulikia ushauri uliotolewa ili Shirika hili liweze kuwajibika chini ya mamlaka moja kwa kuanza utaratibu wa kubadilisha sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Serikali itenge fedha za kutosha kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu ili kuongeza ufanisi wa utendaji wa Mashirika ya Nyumbu na Mzinga; Serikali katika mwaka wa fedha 2017/2018 imetenga shilingi bilioni 8.8 kwa ajili ya kufanya ukarabati wa miundombinu ya teknolojia ya Shirika la Nyumbu na shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya Shirika la Mzinga. Hata hivyo, mashirika haya yataendeleza juhudi za mashirika yenyewe binafsi ili waweze kuzalisha fedha zaidi ambazo zitawasaidia katika kuboresha hali ya miundombinu ya mashirika haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ilikuwa ni sehemu ya kujibu hoja zilizotolewa na Kamati na sasa naomba niingie katika hoja zilizotolewa na Kambi ya Upinzani. Kabla sijaingia kwenye hoja zenyewe naomba niseme maneno machache ya utangulizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi ni Taasisi ambayo ni tofauti sana na taasisi nyingine za kiraia hasa kutokana na majukumu yake. Kila Mwanajeshi anapoingia Jeshini anafunzwa miiko na taratibu zake ambapo kwa sehemu kubwa ni kumwezesha Mwanajeshi kutumika vyema wakati anapohitajika kutekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika kwamba sehemu kubwa ya hotuba ya Kiongozi wa Upinzani au Msemaji wa Upinzani, imetokana na hisia na baadhi ya matamshi ambayo hayana ukweli wowote au hayajafanyiwa utafiti na matokeo yake yanaweza kuzua majungu au utovu wa nidhamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kwamba Jeshi huendeshwa kwa kuzingatia mambo yafuatayo:-

(1) Katiba ya Nchi;

(2) Sheria ya Ulinzi wa Taifa;

(3) Kanuni ya Majeshi ya Ulinzi; na

(iv) ni Forces Routine Orders zinazotolewa na Mkuu wa Majeshi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rejea zote zilizotajwa hapo juu, zinatoa utaratibu kamili wa namna ya kuendesha Jeshi kama Taasisi ya Nidhamu na Utii chini ya uongozi wa Amiri Jeshi Mkuu na pia uongozi wa Kisiasa wa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa katika uhalisia wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Ulinzi wa Taifa na Kanuni za Majeshi ya Ulinzi, volume ya kwanza, ya pili na ya tatu, zinatoa maelekezo ya namna Wanajeshi watakavyotenda kazi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani inaingilia mno shughuli za uendeshaji wa jeshi. Hatari iliyopo ni kwamba Kiongozi wa Upinzani amechukua maneno kutoka kwa Askari wasiozingatia nidhamu na bila ya kufanya utafiti wa kutosha, amegeuza kuwa ndiyo taarifa yake. Ni vyema tutambue kwamba kauli kama hizi zinaweza kupelekea kuligawa jeshi bila sababu yoyote au kupandikiza mbegu za utovu wa nidhamu jeshini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanajeshi wamejiunga na jeshi kwa masharti yaliyopo na wanapaswa kuyazingatia wakati wote wa utumishi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia kusema, nimesikitishwa sana na maneno yenye lengo la kuwagombanisha wanajeshi na Serikali yao pamoja na Wanajeshi na Uongozi wao wa juu. Hili halipaswi kuvumiliwa na ni vyema Bunge lako liangalie utaratibu wa kikanuni za kumtaka Msemaji athibitishe maelezo aliyoyatoa katika wakati muafaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo ya utangulizi, sasa naomba nizijibu hoja zilizotolewa na Msemaji wa Kambi ya Upinzani kama ifuatavyo:-

Kwanza, kuongeza muda wa kufanya kazi Jeshini baada ya muda wa kawaida kwisha. Siyo sahihi kuwa Wanajeshi hawakupewa au hawakuelezwa sababu za kuendelea kufanya kazi baada ya muda wa kazi za kawaida. Wanajeshi wote walipewa taarifa na hakuna taharuki yoyote. Muda wa kazi uliongezwa kwa ajili ya michezo na mazoezi ya viungo. Aidha, ikumbukwe kuwa wanajeshi wanaandikishwa kwa masharti ya kufanya kazi masaa 24. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la usalama wao; wanajeshi wanasafirishwa kwenda na kurudi kazini kwa kutumia mabasi maalum ya usafiri. Hapa nataka kusema kwamba, baada ya saa za kazi, ili Wanajeshi hawa wawe na utimamu wa kimwili na kiafya, wanatakiwa wafanye mazoezi ya viungo na hasa wajihusishe na michezo. Ndiyo sababu ya kuongeza muda wa kutoka kazini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani, ama kuna wakati pengine ilizoeleka kwamba watu wanamaliza baada ya muda wa saa za kazi wanakwenda bar wanakunywa pombe na kadhalika. Hii haina afya kwa jeshi letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi wanapokuja kurudisha taratibu stahili hatupaswi sisi kama viongozi kuwaona wanafanya makosa, badala yake tuwapongeze kwa hatua hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ilikuwa ni kusitisha utoaji wa fedha za likizo kwa wanajeshi. Malipo ya fedha za likizo kwa wanajeshi hayajasitishwa na ni haki kwa wanajeshi wote. Aidha, siyo kweli kwamba Mnadhimu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, yaani Chief of Staff amezuia madai ya wanajeshi ya kulipwa malipo ya likizo. Mnadhimu Mkuu wa Jeshi amekuwa mstari wa mbele katika kufuatilia stahiki hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi kila mwaka wa fedha, fedha za likizo zinatengwa kutoka bajeti ya Jeshi kila mwaka wa fedha. Changamoto kubwa imekuwa ni ukomo wa bajeti, hali inayosababisha kutokidhi kuwalipa wanajeshi wote wanaostahili kwenda likizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara itaendelea kuwasiliana na Hazina iweze kusaidia kuongeza bajeti katika eneo hili ili wanajeshi wote waweze kwenda likizo. Aidha, Wizara inajaribu kubuni njia nyingine kwa kushirikiana na Hazina ili kuhakikisha kuwa wanajeshi wote wanalipwa fedha za likizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuongezea katika eneo hili; mimi binafsi wakati nikifanya ziara zangu katika Kambi za Jeshi, napata nafasi ya kuzungumza na Wanajeshi; katika kero kubwa ambayo imekuwa ikizungumzwa na Wanajeshi, ni kero ya fedha za likizo. Nimekuwa nikiwaambia kwamba hakuna mtu, siyo Wizarani wala Jeshini ambaye angependa wasipate. Sote tunapenda wapate, tunawapigania sana na tukifanikiwa katika kupata fedha hizi tutawalipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wote ambao hawajalipwa kwa kipindi ambacho walistahili, zinahesabiwa kama ni madeni. Fedha za madeni zikilipwa, watapewa fedha zao. Kwa hiyo, hatuoni sababu kwa nini kuja na dhana kwamba Chief of Staff anataka watu wasilipwe? Hili litahitaji kuthibitishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja nyingine iliyotolewa kwamba Wajumbe wa Bodi ya Manunuzi wanajipa safari za ununuzi wa zana nje ya nchi. Bodi ya Wazabuni ya JWTZ imeundwa kisheria kwa kuzingatia Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 na Kanuni zake. Bodi hiyo ina wajibu wa kutoa idhini ya manunuzi ya vifaa mbalimbali kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wajumbe wa Bodi hiyo hawana wajibu wa kununua vifaa na hakuna Mjumbe wa Bodi ya Manunuzi ambaye amesafiri kwenda nje ya nchi kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya JWTZ. Utaona kwamba hoja hii nayo inataka ithibitishwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani mtu mmoja barabarani akasema maneno ambayo kwa kweli yanaharibu taswira ya Jeshi zima, halafu tukayachukua tukayaweka kwenye hotuba halafu wengine tukanyamaza kimya. Kwa kweli hili litakuwa siyo jambo la busara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ilikuwa ni kuondolewa kwa maduka ya bei nafuu Jeshini, yaani Military Duty Free Shops. Maduka hayo yaliondolewa rasmi na Serikali tarehe 1 Julai, 2016 baada ya kuonekana kutowanufaisha Wanajeshi na pia baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kutumia mwanya wa maduka hayo kukwepa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuondoa maduka hayo, Serikali imekuwa ikiwalipa Wanajeshi fedha za ruzuku kama sehemu ya kupunguza makali ya misamaha ya kodi iliyoondolewa. Siyo kweli kwamba fedha hizo zimetolewa mara moja tu, fedha hizo bado zimeendelea kutolewa kila baada ya miezi mitatu kama Serikali ilivyoahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika, katika ziara zangu katika makambi ya Jeshi, ukiuliza matatizo ya Wanajeshi, wao wenyewe watakiri kwamba maduka haya yalikuwa yanawanufaisha wafanyabiashara siyo wao. Maduka mengi ya Jeshi, ilikuwa gharama wanazolipa wao ni sawa na kununua mtaani, wakati wao wametolewa ushuru. Kwa hiyo, aliyekuwa anafaidika ni wale wafanyabiashara. Serikali imegundua hili, sasa hivi wanatakiwa kulipwa; wameanza fitina na hili linaonekana kama vile Wanajeshi wanaonewa. Siyo kweli, waliokuwa wananufaika siyo Wanajeshi na tutaendelea kuwapa hiyo ruzuku ili kuweza kuwapunguzia makali ya maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tano, kuhusu Wanajeshi kutopandishwa vyeo. Suala la Wanajeshi kupandishwa vyeo, linazingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo bila ubaguzi wowote. Maafisa na Askari ambao wanastahili na wamekidhi vigezo, wamekuwa wakipandishwa vyeo mara kwa mara kwa kufuata taratibu zilizopo. Mara ya mwisho Maafisa na Askari wamepandishwa vyeo katika ngazi mbalimbali mwezi Aprili, 2017. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake nini? Maana yake, katika Hotuba ya Kambi ya Upinzani walitaka kuashiria kwamba, kuna Mkuu wa Majeshi mpya ameacha kupandisha watu vyeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepandisha watu vyeo. Kwanza kwa taarifa yenu, upandishwaji wa vyeo unafanywa na Kamati ya Ulinzi ya Taifa, ambayo Mwenyekiti wake ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Aprili mwezi uliopita tumekaa na tumepandisha vyeo Wanajeshi wote wanaostahili kupandishwa vyeo. Kwa hiyo, siyo kweli hata kidogo kwenda mitaani kuchukua maneno ambayo hayana chembe ya ukweli kuyaleta na kuyazungumza ndani ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, malipo ya fedha za chakula kwa Wanajeshi (Ration Allowance); fedha za chakula kwa Wanajeshi hulipwa kwa kuzingatia Sheria ya Ulinzi ya Taifa ya mwaka 1966; na Kanuni za Majeshi ya Ulinzi, Utawala ambapo chakula hutolewa kwa Wanajeshi kwa kuzingatia majukumu anayopewa Mwanajeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwanajeshi anawajibika kula chakula stahiki na mahali stahiki kwa mujibu wa kanuni na taratibu zilizopo. JWTZ kwa kushirikiana na Serikali, litaendelea kuhakikisha kuwa Wanajeshi wanapewa chakula stahili kwa kuzingatia majukumu wanayopewa. Fedha za chakula anazolipwa Mwanajeshi, siyo kwa ajili ya familia yake bali ni kwa ajili yake mwenyewe ili awe na afya imara, isiyotetereka ili aweze kutekeleza majukumu ya ulinzi wa Taifa kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niongezee kusema kwamba, wale ambao wapo kazini, wale ambao wapo kambini, wale ambao wana kazi maalum (operation), lazima wale ndiyo wakatekeleze operations. Wale ambao wapo katika maeneo mengine, wanapewa fedha zao kwenye
mishahara yao. Hakuna tatizo hapa. Kwa hiyo, haya maneno pia hayana ukweli Mheshimiwa. Naomba sana siku nyingine ukipata maelezo kama haya, nione kwanza, nitakupa taarifa kabla hujaweka kwenye hotuba yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine inahusu ufinyu wa bajeti ya umeme. Suala la ufinyu wa bajeti ya umeme, linatokana na ukomo wa bajeti unayotolewa na Serikali. Tunapenda kuishukuru Serikali kwa hatua iliyochukua ya kuweza kupunguza madeni ya umeme ili JWTZ liendelee kupata huduma ya umeme katika makambi. Wizara itaendelea kuwasiliana na Hazina ili waweze kutoa fedha za kutosha, katika eneo la umeme na maeneo mengine muhimu ambayo tunadaiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kweli kwamba Jeshi halilipi kwa kutotaka, wala siyo kweli kwamba Amiri Jeshi Mkuu ameamua hata Kambi za Jeshi zikatiwe umeme. Alichosema ni kwamba watu lazima walipe na baada ya hapo Hazina walitoa fedha na jeshi likalipa; na tutaendelea kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee na eneo lingine la utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2016/2017. Kambi ya Upinzani wanasema fedha za maendeleo zimetolewa pungufu, hili tunakiri. Fedha za Maendeleo hutolewa kila mwezi kutegemeana na mapato ya Serikali kila mwezi, Wizara inaendelea kuwasiliana na Wizara ya Fedha na Mipango ili fedha zote ambazo hazijatolewa, ziweze kutolewa katika kipindi kilichobaki ili tuweze kutimiza majukumu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu makusanyo kidogo ya maduhuli ya JKT; maduhuli ya JKT yaani Fungu 39 yanatokana na matunzo ya mazao ya shamba darasa, uuzaji wa nyaraka za zabuni na siyo kutoka katika shughuli za uzalishaji mali za SUMA JKT. Yaani kwa maana nyingine tutofautishe kati ya SUMA JKT na Fungu 39, yaani Makao Makuu ya JKT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii taarifa ya asilimia 31.8 ni maduhuli ya JKT, yaani Fungu 39 hadi kufikia Machi 2017. Aidha, hadi kufikia tarehe 15 Mei, 2017 fedha zilizokusanywa kutokana na maduhuli zimefikia asilimia 67.5 ya lengo. Kwa hiyo, tunakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika randama ya Fungu 57 subvote 1005 na subvote 2004 hazikutengewa fedha za mishahara. Je, vitengo hivi havina watendaji? Lilikuwa ni swali, ambalo jibu lake ni kwamba vitengo hivi kwa sasa havina watumishi wa umma ambao mishahara yao ingepaswa kuonekana hapo, bali kwa sasa wapo Wanajeshi ambao mishahara yao inalipwa kutoka Fungu 38 la Ngome.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni Uteuzi wa Wanajeshi katika nafasi za Kisiasa. Ndugu yangu Naibu Waziri wa Afya amenisaidia kujibu hili eneo, lakini niseme tu hivi kwamba, uteuzi wa viongozi unazingatia weledi na hitajio la uongozi katika eneo husika na kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Majukumu ya Viongozi hawa siyo ya kisiasa, bali ni kutekeleza kazi za Kiserikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, uteuzi unaofanywa siyo tafauti na majukumu ambayo Serikali imekuwa mara kwa mara ikiliagiza Jeshi kusaidia mamlaka za kiraia. Kwa maana nyingine, mara kadhaa tumeshaombwa na mamlaka za kiraia kutoa msaada hususan katika maeneo ya mipakani. Kwa hiyo, inaleta mantiki unapomweka Mwanajeshi kusimamaia pale akiwa kiongozi kwa sababu atakuwa na uharaka wa kuchukua hatua kama hizi tunazozizungumzia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo baadhi ya Wanajeshi ambao wameteuliwa na Chama Tawala katika nafasi mbalimbali za uongozi. Hata hivyo, uteuzi huo hufanyika kwa makubaliano ya Chama Tawala na Wanajeshi husika baada ya kustaafu utumishi Jeshini na siyo wanapokuwa katika utumishi wa Jeshi. Mfano, uteuzi wa Kanali Lubinga kuwa Katibu wa NEC ya Chama Tawala, ulifanyika baada ya Afisa Mkuu huyo kustaafu rasmi utumishi Jeshini. (Makofi)

Wanajeshi wanateuliwa kushika nafasi za Kiserikali na siyo za kisiasa, hivyo wanaruhusiwa kuvaa sare za Kijeshi kulingana na majukumu na matukio maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ushiriki wa Jeshi katika operation za ulinzi wa amani; napenda niseme kwamba, ushiriki wa Jeshi katika operation za Umoja wa Mataifa umekuwa na faida kubwa hususan kwa kuwawezesha Wanajeshi wetu kuongeza weledi, kuongeza uzoefu na exposure, teknolojia na kuitangaza Tanzania katika tasnia ya ulinzi na usalama duniani. Tumekuwa tukipata sifa nyingi na ni mategemeo yetu kwamba tutaendelea kutuma vijana wetu wakalinde amani katika maeneo mbalimbali duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu eneo la JKT kwamba SUMA JKT limetoa mchango gani kwa Jeshi katika kukabiliana na changamoto za bajeti? SUMA JKT linashiriki kupunguza changamoto za kibajeti kwa Jeshi kwa kuchangia katika uendeshaji wa Kambi na pia kuchangia gharama za chakula kwa vijana JKT ambapo mpaka sasa asilimia 55 ya gharama inalipwa na itaongezeka kufikia asilimia 100 siku zijazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, SUMA JKT kupitia kampuni yake ya ujenzi imekuwa ikishiriki ukarabati na ujenzi wa Kambi na miundombinu bila kutoza gharama ya kazi hizo. Mchango wa SUMA kuipunguzia Serikali gharama za uendeshaji, ni kwamba jukumu la SUMA ni kuipunguzia Serikali gharama za kuendesha JKT. Jukumu hilo limeanza kutekelezwa kwa kuchangia kulisha vijana na gharama za uendeshaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, idadi ya miradi ya uzalishaji wa mali wa SUMA JKT, iko mingi ikiwemo kilimo na mifugo, uhandisi wa ujenzi, kutoa huduma za ulinzi kwa jamii, uunganishaji na usambazaji wa matrekta na uzalishaji samani, kokoto na ushonaji wa nguo. Fedha zilizoingizwa kutokana na uzalishaji ni jumla ya Shilingi bilioni 7.8 na zinaonekana katika audit report ya SUMA JKT .

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie eneo hili la Kambi ya Upinzani kwa hoja hii ya Jeshi la Kujenga Taifa, kwamba Jeshi hili ni pamoja na kuwa na dhima ya kuwafunza vijana, kuzalisha mali ikiwemo kuzalisha chakula. Jeshi lipimwe kwa uzalishaji mali na kupunguza njaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, JKT lina program ya kuongeza uzalishaji mali na mafunzo ya uzalishaji mali hasa chakula kwa vijana wake kupitia mashamba darasa yaliyopo. Aidha, vijana waliopo kwenye makambi ya JKT wameanza kujitegemea kwa awamu katika gharama za chakula kutokana na chakula wanachokizalisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ni nyingi, sitoweza kuzimaliza zote, lakini nataka kuwahakikishia Waheshimiwa kwamba tutazitoa kwa maandishi kabla ya mwisho wa Bunge hili. Kuna eneo moja muhimu sana ambalo limechangiwa na Wabunge wengi, nalo ni migogoro ya ardhi na fidia kwa maeneo ambayo Jeshi limeyatwaa. Eneo hili limechangiwa na Waheshimiwa Wabunge wengi akiwemo Mheshimiwa Ester Matiko, Mheshimiwa Manyinyi, Mheshimiwa Mabula, Mheshimiwa Deo Sanga na wengi ambao orodha yao ninayo hapa.

Waheshimiwa Wabunge, ninachoweza kusema na naomba mnielewe vizuri kwamba nia ya kulipa ipo, tathmini katika baadhi ya maeneo imeshafanyika, upimaji umeshafanyika, kwa hiyo, kilichobaki ni kulipa tu hiyo fidia inayotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliweka katika bajeti yetu kama nilivyosema shilingi bilioni 27.7, bahati mbaya bado hatujapokea, lakini mazungumzo yanaendelea. Tuna mategemeo kwamba kabla ya mwisho wa mwaka huu wa bajeti, fedha zitakazopatikana tutaanza kulipa fidia zinazotakiwa katika maeneo ambayo nimeyazungumzia hapa. Kwa hiyo, kuna maeneo mengi mno na naweza nikaitoa ile orodha, lakini kwa sababu ya muda, naomba niendelee na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja ya pensheni ndogo kwa wastaafu waliostaafu zamani. Tunakubaliana kabisa na hoja hii na nataka niseme kwamba Serikali imeanza kulifanyia suala hili ili hatimaye tuweze kurekebisha penisheni hizo. Ila ni lazima tuelewe kwamba wastaafu wako wengi sana na fedha zitakazohitajika ni nyingi sana. Kwa hiyo, lazima zoezi hili liende awamu kwa awamu, ndiyo maana Serikali imeanza na ngazi za juu. Imeanza kutoka cheo cha Meja Jenerali hadi Jenerali kamili na tutaendelea kwa awamu hadi hapo ambapo tutaweza kutimiza jukumu hili la Serikali la kuweza kuwatazama wale ambao wamestaafu muda mrefu uliopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hoja za Mheshimiwa Fakharia, kuhusu idadi ndogo ya wanaojiunga na JKT kutoka Zanzibar. Mpaka sasa hivi wanaojiunga na JKT kwa mwaka tunapeleka nafasi 300. Kila tukiongeza idadi ya wanaoingia JKT, pia tutaongeza idadi ya wale wanaotoka Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawashauri tu Waheshimiwa Wabunge kwamba utaratibu ule wa ugawaji, siyo jukumu la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wala siyo la Jeshi. Tunazikabidhi kwa Serikali ya Zanzibar na kuwataka wao wazigawe kwa kadri watakavyoona inafaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa nilizokuwanazo, kwa sasa zinagawiwa katika Wilaya na Mikoa na kama kuna matatizo huko, likiwemo lile alilozungumzia Mheshimiwa Dau kule Mafia kwamba Mshauri wa Mgambo ndio anachukua watu kutoka nje, hapa naweza kusema kwamba zoezi hili linafanywa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya. Halipaswi kufanywa na mtu mmoja. Kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Dau kwamba kama ni kweli haya yanatokea, basi ahakikishe anakaa na DC kama Mwenyekiti ili waweze kudhibiti hii hali, kwa sababu suala hili ni jukumu la Kamati ya Ulinzi na Usalama, siyo suala la Mshauri wa Mgambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jasson Rweikiza alitaka kujua tuna-ratify lini ile Biological Weapon Treaty ambayo, tumeshaisaini? Naweza kumwambia Mheshimiwa Mbunge kwamba wakati tunaleta hoja hii kwa ajili ya ratification tulipewa ushauri, kwamba kuna treaties nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Chemical Weapons Treaty; kuna Biological Weapon Treaty kuna Nuclear Weapon Treaty; hizi zote ni weapon of mass destruction. Tukashauriwa kwamba ziwekwe kwa pamoja ili ziwe zina sheria moja. Ili ziweze kufanya hivyo, kwa hiyo, tumekubaliana kwamba zoezi hilo sasa lianze kwa haraka ili hatimaye tuweze kui-ratify treaty hii na tuweze kupitisha sheria ili tuweze ku- domesticate sheria zote hizi kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Masoud aliungana na Wabunge wengine kusema kwamba bajeti ya Wizara hii ni ndogo na tunakubaliana na hilo, lakini hiyo ndiyo hali ya uchumi wa nchi. Tuna uhakika kwamba kila uchumi ukikua na Wizara hii itaongezewa fedha kwa umuhimu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Ration Allowance kwamba isiondolewe; tunasema kwamba Ration Allowance haijaondolewa; ipo na itaendelea kuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la fidia ya maeneo yaliyochukuliwa na Jeshi, nimeshalitolea taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ujenzi wa maghala kwamba hayajakamilika na yatakwisha lini? Niseme hapa kwamba maghala yako katika hatua nzuri sana, yaliyobaki ni mambo machache sana ya kuunganisha umeme hapa na pale na kadhalika, isipokuwa lile ghala la Pemba, ambapo kumetokea mgogoro na Mkandarasi. Sasa hivi utaratibu unafanywa wa kuuvunja mkataba ule ili apewe Mkandarasi mwingine mwenye uwezo alikamilishe lile ghala na silaha zetu ziweze kukaa sehemu salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya ulinzi wa Taifa nimeshalitolea taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu eneo la Hospitali za Jeshi kuwa katika mazingira ambayo hayaridhishi na kadhalika. Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia hili. Naweza kusema hapa kwamba tuko katika mchakato wa kuanzisha Bima ya Afya kwa Wanajeshi. Sisi tuna imani kubwa kwamba huo ndiyo utakuwa mwarobaini wa matatizo yote ya kiafya Jeshini. Tutapata fedha za kutosha kuboresha vituo vyetu, kuongeza dawa kuajiri Madaktari na kuwalipa hata wale Madaktari ambao wanakuja kufanya part time. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona muda wangu umekwisha, bado nina hoja nyingi sana ambazo sijajibu; lakini kama nilivyoahidi, tutazitoa kwa maandishi ili Waheshimiwa Wabunge wote wapate majibu ambayo tulikuwa tumeyaandaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja.