Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

Hon. Capt. Abbas Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Fuoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

MHE. CAPT. ABBAS ALI MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu kwa Taifa letu ambayo imeendelea kudumisha amani na utulivu kwa Taifa letu pamoja na kulinda Muungano dhidi ya maadui wa ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ufinyu wa bajeti kumekuwa na upungufu mkubwa wa makazi ya wanajeshi wetu na wale waliobahatika kupata makazi, hayapo katika hali ya kuridhisha. Upungufu huo wa makazi unapelekea baadhi ya wanajeshi kuishi nje ya Kambi za Jeshi, jambo ambalo ni hatari kwa askari wetu. Suala la askari kuchanganyika na raia kunawashushia hadhi yao kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto kubwa ya ajira kwa vijana wanaomaliza JKT Bara na Visiwani. Nashauri Wizara ya Ulinzi zishirikiane na Wizara nyingine kutoa vipaumbele vya ajira kwa vijana wanaomaliza JKT. Hii itasaidia kwa kiwango kikubwa kurudisha nidhamu ya utumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri, atakapokuja kuhitimisha (kufanya majumuisho) ananiambie nafasi za ajira zinazopelekwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ziko kwa uwiano gani ukilinganisha na Tanzania Bara?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na uwiano mdogo kati ya wanawake na wanaume kwa maafisa wa ngazi za juu wa uongozi wa JWTZ. Naomba kujua kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, anapokuja kuhitimisha, ni kwa nini hali hii inajitokeza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, hali ya ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi yetu ni shwari kwa mujibu wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Napenda kujua mgogoro wa mpaka wa Malawi na Tanzania kupitia Ziwa Nyasa ambao umechukua muda mrefu, ambao unaweza kuleta athari za uwekezaji katika nchi yetu, na hivyo kupelekea hasa Ukanda wa Nyasa kudorora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Naunga mkono hoja.