Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora kwa mwaka wa fedha 2016/2017

Hon. Esther Lukago Midimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora kwa mwaka wa fedha 2016/2017

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anazozifanya. Vile vile nampongeza Waziri Mkuu kwa kazi nzuri anazozifanya, wananchi wote wanaziaminia. Pili, nawapongeza akinamama wa Mkoa wa Simiyu kwa kunipa kura ili niweze kuwawakilisha katika Bunge lako Tukufu na nawaahidi utumishi uliotukuka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawapongeza sana Mawaziri wote wawili kwa hotuba yao nzuri. Naanza na uboreshaji wa maslahi ya Madiwani. Madiwani wanafanya kazi katika mazingira magumu sana hawana hata usafiri. Naiomba Serikali yangu sikivu iweze kuwapatia hata pikipiki ili waweze kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la afya Wilaya ya Maswa; hospitali ya Wilaya ya Maswa ina tatizo la umeme, umeme siyo wa uhakika unasuasua, miundombinu imekuwa ya kizamani. Naiomba Serikali yangu iweze kuboresha miundombinu ya hospitali ya Wilaya ya Maswa. Vile vile hospitali ya Wilaya ya Maswa ina majengo ambayo yameshakamilika, jengo la OPD, theater na wodi ya wazazi, lakini hayajaanza kutumika. Naomba Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi hayo majengo yaanze kutumika yaweze kuhudumia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika Wilaya hospitali ya Maswa ina tatizo la maji. Jambo la kusikitisha Maswa Mjini kuna maji na hospitali ya Maswa na Maswa Mjini ni pua na mdomo, lakini hospitalini hakuna maji. Naiomba Serikali yangu ifanye haraka ivute maji kutoka pale Maswa Mjini ipeleke hospitali ya Maswa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu afya katika Wilaya ya Itilima, Wilaya ya Itilima tunayo zahanati kubwa sana Kata ya Luguru. Hiyo zahanati ina majengo mengi sana. Tunaomba kibali kwa zahanati hiyo ili iweze kupandishwa hadhi iwe kituo cha afya. Tuna jengo kubwa la upasuaji limejengwa na Mfuko wa Mkapa Foundation na vifaa tiba tayari vipo, tatizo hatuna wataalam wa upasuaji. Naiomba Serikali yangu itupelekee Madaktari Bingwa wa upasuaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kituo cha afya Zagayu. Kituo cha afya cha Zagayu kina wafanyakazi watano ambapo mahitaji ni wafanyakazi 32. Tunaomba mtupelekee watumishi 32 ili waweze kuhudumia vizuri. Tunacho kituo cha afya Kata ya Nkoma, tunaiomba Serikali itupatie kibali kama kuna uwezekano tukipandishe hadhi kwa Wilaya ya Itilima tuwe na Hospitali ya Wilaya, kwa sababu wananchi wa Itilima wanahangaika sana, wakipata matatizo wanaenda kutibiwa Bariadi, Somanda. Tukikipandisha hadhi kile kituo cha afya cha Itilima, nina imani hata msongamano wa wagonjwa Somanda utapungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya maji; naipongeza sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kuahidi kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria kuleta Mkoani Simiyu kupitia Wilaya zake za Busega, Bariadi, Maswa, Itilima na Meatu. Naiomba Serikali yangu ihakikishe hayo maji itakapovuta, maji yapitie kwenye shule zote za Mkoa wa Simiyu za Sekondari, vituo vya afya vyote na zahanati ili yaweze kusaidia kwa sababu maji ni muhimu kwenye vituo vya afya na hospitali, ukizingatia na sera yetu ya sasa hivi ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kila Kijiji kutakuwa na zahanati na kila Kata kutakuwa na kituo cha afya. Naomba na maji yafike huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna vijiji katika Wilaya ya Maswa havina maji kabisa ambavyo ni Gudekwa, Masanwa, Mwabalatulu na Isegenge, akinamama wa vijiji vile wanahangaika sana. Naiomba Serikali yangu iweze kuchimba visima virefu kwa hivyo vijiji nilivyovitaja ili mradi akinamama waweze kupata maji. Wameshindwa kufanya kazi zao za ujasiriamali na mambo mengine ya maendeleo wamebaki kutafuta maji, wanasafiri kilometa nane mpaka kilometa 10. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekta ya elimu; naishukuru sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kujenga shule nyingi za Kata, naipongeza sana. Naiomba Serikali yangu kama kuna uwezekano kwa Mkoa wetu wa Simiyu iweze kutenga kila Wilaya shule ya bweni kwa watoto wa kike, kwa sababu watoto wa kike wanahangaika sana, watoto wa kike tukijenga shule za bweni tutawaepusha na vishawishi vya chipsi na bodaboda wakiwa wanarudi makwao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Bariadi tuna Chuo cha Ufundi, Bunamhala, chuo kile naomba kiboreshwe, vijana wengi wapate ujuzi ili waweze kujiajiri wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mkoa wetu una changamoto, una upungufu wa nyumba za Walimu 1,471, madarasa 563 na matundu ya vyoo 2,107. Tunaiomba Serikali iweze kutuletea pesa kupitia TAMISEMI ili tuweze kukamilisha ujenzi huu. Vile vile naomba Serikali iweze kuweka Chuo cha VETA Mkoani Simiyu na iweze kutuletea pesa haraka sana tuweze kujenga hospitali ya Mkoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi, naunga mkono hotuba ya Waziri Mkuu kwa asilimia mia moja.