Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Antony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU – SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi hii. Kwanza kabisa napenda kuchukua fursa hii kwa sababu, ni mara yangu ya kwanza kuchangia na kusimama kutetea hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu, nichukue fursa hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kuniteuwa na kunipa dhamana ya kuhudumu katika nafasi ya Naibu Waziri Kazi, Vijana na Ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nachukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, kwa ushirikiano mkubwa na miongozo mbalimbali ambayo amekuwa akitupa katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Pia, nachukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama, pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri, Dkt. Abdallah Possi, kwa ushirikiano mkubwa ambao wamekuwa wakinipa katika utekelezaji wa majukumu yetu, lakini pia na Mawaziri wengine wote wanaounda Baraza la Mawaziri kwa miongozo yenu na ushauri wenu katika utekelezaji wa majukumu yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii pia, kipekee kabisa kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Dodoma Mjini kwa kunichagua kuwa Mwakilishi wao kwa kura nyingi sana. Nataka niwaahidi tu kwamba, kwa yale ambayo waliyatazamia kutoka kwangu nitajitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu niweze kuwatumikia vyema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni ya 99(2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 naomba sasa uniruhusu nitoe ufafanuzi wa baadhi ya hoja ambazo ziliwasilishwa na Waheshimiwa Wabunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge walichangia, moja ya mambo yaliyojitokeza wakati wa uchangiaji, lilijitokeza suala la ukaguzi wa Sera ya Uwekezaji katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) pamoja na Benki Kuu ya Tanzania ilitoa Mwongozo wa Uwekezaji wa mwaka 2015 ambao kwa mujibu wa mwongozo huo SSRA na BOT imekuwa ikifanya special inspection kwenye miradi yote ya uwekezaji ambayo inahusisha Mifuko ya Hifadhi ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, lengo kubwa sana la kaguzi hizi ni kuhakikisha kwamba Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inawekeza katika miradi ambayo itakuwa ina tija na manufaa kwa Watanzania. Pia, kupitia SSRA zimekuwa zikifanyika kaguzi za mara mbili kwa mwaka ambapo lengo lake kubwa ni kuweza kuangalia miradi hii ambayo inawekezwa na kuona namna ambavyo inaweza kuleta tija hasa katika maeneo ambayo yanawagusa Watanzania moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ilijitokeza hoja ya kuhusu Mikataba ya Wafanyakazi na vilevile wageni wasiokuwa na vibali vya kazi. Serikali imeendelea kufanya kaguzi mbalimbali kwa kutumia Maafisa Kazi waliopo nchini ili kuweza kubaini Waajiri wote ambao hawatoi mikataba kwa Wafanyakazi wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie tu fursa hii kutoa agizo kwa waajiri wote nchi nzima kuhakikisha kwamba wanatoa mikataba kwa wafanyakazi wao na Serikali haitasita kuendelea kuchukua hatua itakapobainika kwamba Waajiri hawatoi mikataba kwa Waajiriwa wao, jambo ambalo kwa mujibu wa Sheria zetu tutawachukulia hatua ili kuona ni namna gani sasa wata-comply na masharti ya Sheria zetu za Kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye suala la vibali vya ajira kwa wageni, tumeendelea kufanya kaguzi mbalimbali katika maeneo ya kazi kuweza kuwabaini wale wageni wanaofanya kazi pasipokuwa na vibali au ambao wanakiuka vibali vya kazi na hatua stahiki zimekuwa zikichukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, mtakuwa mashahidi, mmeona ziara mbalimbali ambazo zilifanywa na Mheshimiwa Waziri pamoja na mimi Naibu wake, kupitia katika maeneo tofauti tofauti ya kazi na tumekuwa tukichukua hatua stahiki kuhakikisha kwamba wale wageni wote waliokuja kufanya kazi nchini, kwa mujibu wa Sheria Na. 1 ya Mwaka 2015, wanafuata masharti ya Sheria na tunahakikisha kwamba vibali vya kazi walivyopewa wanavifanyia kazi kwa mujibu wa taratibu ambazo wameziomba. Kwa hiyo, ikibainika tofauti, tumekuwa hatusiti kuchukua hatua na wako wageni wengi ambao tumewafutia vibali na wengine kusafirishwa nje ya nchi kwa kukiuka masharti ya Sheria hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilijitokeza pia, hoja nyingine ya kuwajengea uwezo Maafisa wa Vijana katika Halmashauri na Viongozi wa SACCOS. Hoja hii ilijitokeza kama ushauri na kwa niaba tu ya Ofisi ya Waziri Mkuu, niseme kwamba ushauri huu tumeupokea, tutaufanyia kazi kwa kushirikiana na Halmashauri zote nchini. Hata hivyo, tayari Ofisi ya Waziri Mkuu imeshaanza kuwajengea uwezo Viongozi wa SACCOS na vikundi mbalimbali vya vijana na kufikia Machi mwaka huu, tayari vikundi 2,552 vilikwishakupatiwa Semina mbalimbali kuhusiana na masuala ya ujasiriamali, kilimo na masuala ya uongozi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hoja nyingine iliyojitokeza wakati Waheshimiwa Wabunge wakichangia, ilijitokeza hoja ya kuwa na idadi ndogo ya Watanzania wanaoajiriwa katika Sekta ya Viwanda. Katika hoja hii pia, ilizungumzwa kwamba asilimia kubwa ya watu wengi ambao ni wageni ambao wanafanya kazi katika maeneo haya, wamekuwa wakichukua kazi za Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasi kama Serikali, kama nilivyosema pale awali, tumeendelea kuisimamia na kuitekeleza Sheria Na. 1 ya mwaka 2015 ambayo imeweka utaratibu wa kuwaajiri wageni ndani ya nchi yetu, hasa katika maeneo ambayo yana upungufu wa wataalam. Ili kuhakikisha kwamba idadi kubwa ya vijana wanaajiriwa katika viwanda vyetu, tumeendelea kufanya kaguzi mbalimbali na lengo lake ni kuweza kubaini wale wafanyakazi wageni ambao hawakidhi masharti ya Sheria Na.1 ya mwaka 2015 kwa kufanya kazi ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nimwondolee hofu Mheshimiwa Mbunge, mama yangu Mheshimiwa Mama Vullu, ambaye katika hoja yake alisisitiza pia, kwamba ikiwezekana, basi tuongozane naye katika eneo lile la Mkuranga ambako kumekuwa kuna changamoto kubwa kwamba viwanda vingi ambavyo viko pale, wanaofanya kazi, wengi ni wageni ambao hawana sifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwahidi tu Mheshimiwa Vullu kwamba kwa sababu tumedhamiria kuwatumikia Watanzania, niko tayari muda wowote kushirikiana naye kwenda kuhakikisha kwamba tunafanya kaguzi ili kuwabaini wale wote ambao ni wageni wanaofanya kazi pasipokuwa na vibali vya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, ilizungumzwa hoja kuhusu masuala ya afya na usalama mahali pa kazi. Ni kweli nataka nikiri kwamba kumekuwepo na changamoto kubwa sana, lakini Serikali imeendelea kufuatilia kupitia OSHA na imesajili na kukagua maeneo takriban 39 katika eneo la Mkuranga na hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa kwa mujibu wa Sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua za kwanza ambazo zimekuwa zikichukuliwa tunapokwenda kufanya kaguzi na kukuta kwamba katika baadhi ya maeneo Sheria haijafuatwa kwa maana ya masuala ya afya na usalama mahali pa kazi, hatua ya kwanza imekuwa ni kutoa hati ya kumtaka Mwajiri afanye marekebisho, lakini pale inapoonekana kwamba hali hairidhishi na bado hakujafanyika hatua zozote za marekebisho, basi tumekuwa tukichukua sheria za kuwatoza fine na kuwapeleka Mahakamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilizungumzwa pia hoja ya utengaji wa maeneo kwa ajili ya shughuli za vijana na hii ilitokana na kuwa kumekuwepo na tafrani hasa baada ya Mheshimiwa Rais kuzungumza, kuwataka vijana waache kucheza pool na kwenda kufanya shughuli za uzalishaji mali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kulizingatia hilo, Serikali kupitia Wakuu wa Mikoa yote Tanzania imeelekeza Halmashauri za Wilaya na Serikali za Mikoa kutenga maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za kiuchumi za vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo haya, lengo lake kubwa ni kuhakikisha kwamba vijana wanapata maeneo ya kufanya shughuli za uzalishaji mali. Kwa hiyo, nachukua fursa hii kuendelea kuwasisitiza viongozi wote wa Halmashauri za Wilaya na viongozi wa Mikoa kuendelea kutenga maeneo maalum kwa ajili ya vijana ili wapate shughuli za kufanya; kilimo na shughuli za ujasiriamali kama ambavyo imekuwa maagizo yakitolewa mara kwa mara na Mheshimiwa Rais alivyoagiza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ilizungumzwa hoja ya fedha za mikopo ya asilimia 10 kwa ajili ya makundi ya akinamama na vijana. Ushauri huu umepokelewa na Ofisi ya Waziri Mkuu imeweka mkakati kuhakikisha kwamba fedha hizi zinawafikia walengwa kuhakikisha kwamba mapato ya ndani ya Halmashauri, zile 5% kwa makundi ya vijana na akinamama zinayafikia makundi haya. Pia, tumeweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba Halmashauri zinatoa taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo la Mheshimiwa Rais kila baada ya miezi mitatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kutoa rai kwa vijana nchi nzima kuhakikisha kwamba wanaendelea kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali ili waweze kupata fursa ya kuweza kuwezeshwa kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili, kwa kutambua kwamba tuna changamoto kubwa sana ya ukosefu wa ajira kwa vijana, tumekuwa tuna mipango mbalimbali ya kuhakikisha kwamba vijana hawa kwanza kabisa tunawatambua; pili, tunawarasimisha na hatua ya tatu tuone namna gani tunaweza tukawawezesha kiuchumi ili kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nachukua tu fursa hii kuwaomba vijana wote nchi nzima waendelee kukaa katika vikundi vya uzalishaji mali ili sisi kama Serikali sasa, tuwe katika sehemu ya kuweza kuwasaidia katika kuwawezesha kiuchumi ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, nichukue fursa hii kipekee kabisa kuwahimiza vijana wote nchi nzima kuendelea kufanya kazi kwa bidii hasa tukizingatia kwamba vijana ndiyo nguvukazi ya nchi hii. Nasi kama Serikali tutaendelea kuandaa mazingira wezeshi ya kuwafanya vijana washiriki katika uchumi wao na watumie muda wao mwingi katika kuujenga uchumi wa nchi yetu, badala ya kufanya shughuli ambazo hazina tija na zisizokuwa za uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili, nataka tu nisisitize ya kwamba takwimu zimeonesha nguvu kubwa hii ya vijana imekuwa ikitumia muda mwingi kufanya shughuli ambazo hazizalishi na zisizokuwa na tija kutokana na tafiti mbalimbali ambazo zimeelekeza. Kwa hiyo, ni vema sasa vijana wetu na sisi tukabadilisha mtazamo katika nchi yetu hii tukajielekeza katika kushiriki moja kwa moja kwenye shughuli za kiuchumi ili na sisi kama nguvu kazi ya Taifa tuwe sehemu ya ujenzi wa Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe vijana wote nchi nzima kuchukulia agizo la Mheshimiwa Rais la kufanya kazi kama ni sehemu ya kutekeleza wajibu wetu kama wananchi wema katika nchi yetu, lakini na sisi tuoneshe mchango wetu katika kuhakikisha kwamba tunatoa mchango katika nchi yetu katika kujenga uchumi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie tu kwa kufanya nukuu kutoka Kitabu cha Virgil’s Georgecs katika mashairi haya, mstari namba 146; yalisomeka pale maneno ya Kilatini ambayo yanasema, “Labor omnia vincit” ambayo tafsiri yake ni kwamba, Work conquers all, ambayo inashabihiana kabisa na falsafa ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Hapa Kazi Tu, ikituhimiza kwamba kila mmoja kwa nafasi yetu hasa vijana, tuhakikishe kwamba tunatenga muda wetu kwa ajili ya kufanya shughuli za kuzalisha, tusaidie kujenga uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kujibu hoja hizo ambazo Waheshimiwa Wabunge, walizizungumza nichukue tu fursa hii kipekee kabisa nami niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia, lakini ambao wametushauri katika namna bora ya utekelezaji wa majukumu yetu ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nasi kama Wizara tutaendelea kuhakikisha kwamba, tunatatua kero, changamoto na matatizo mbalimbali ambayo yanawakabili kundi kubwa hili la vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.