Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Mattar Ali Salum

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shaurimoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. MATTAR ALI SALUM: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Spika kwa kunipa nafasi hii kwa ajili ya kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, jina langu naitwa Mattar Ali Salum, kwa hiyo naomba kidogo tuliweke sawa ili tuweze kufahamika vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi yake nzuri ambayo anaifanya katika kushughulikia tatizo la maji katika nchi yetu, maji ni uhai.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nigusie sana katika suala la Mfuko wa Maji. Ni suala ambalo ni sensitive sana ambalo Serikali lina haki sana ya kutusikiliza kwa macho mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Maji ndio mkombozi wa nchi hii. Kwenye ziara yote ambayo tumeifanya, ukaguzi tulioufanya Kamati katika maendeleo yaliyofanywa katika miradi ya maji yote asilimia kubwa imetoka katika mfuko wa maji. Kwa hiyo niiombe sana Serikali iangalie huu mfuko wa maji ili uweze kuendelea kuweza kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali na maombi yangu haya naamini yatakuwa ni ya Waheshimiwa Wabunge wengi ambao walichangia Bunge lililopita na hata Bunge hili. Tunaiomba sana Serikali iongeze sh. 50 ili ifike sh. 100 ili Mfuko wa Maji uwe mkubwa ili uweze kutekeleza majukumu yake kwa ufasaha zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba sana Serikali suala hili la kuongeza hii sh. 50 itimie sh. 100 kwenye kila lita ya petrol na diesel hili liwe important sana. Serikali tunaiomba sana iweze kusikia tatizo hili, iweze kusikia maoni ya Waheshimiwa Wabunge na hivyo kuhakikisha maji yanapatikana kwa ufasaha.

Mheshimiwa Naibu Spika tumeiona bajeti ya Serikali ilivyo ndogo, lakini tukipata pesa katika mfuko huu, ukikaa vizuri basi tunaweza tukafika katika hatua kubwa katika kutatua tatizo la maji katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la maji bado ni sugu sana ambalo kutatulika kwake ni kazi ngumu sana, inahitaji kazi ya ziada ili tuweze kutatua tatizo hilo la maji. Tumefanya ziara katika vijiji vingi, katika Wilaya nyingi tumekuta tatizo la maji linaendelea kusumbua sana. Niiombe sana Serikali iweze kusikia kilio hiki cha kuongeza hizi sh. 50 ili iwe sh. 100 kwa lita ya petrol ili iweze kufikia hatua ya kutatua tatizo hili la maji hasa katika vijiji vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, katika uongezaji wa sh. 50 hii ikawa sh. 100, nashauri shilingi 70 iende vijijini shilingi 30 ije mijini kwa kuwa vijijini ndiko kuna kero kubwa ya maji kuliko mjini. Kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri pesa hii iweze kugawia vizuri na niiombe Serikali iweze kutukubalia suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuendelea nigusie tatizo la pesa za Benki ya India zinazokwenda Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ni zito sana. Bajeti iliyopita fedha hizi zililetwa ndani ya vitabu tukaambiwa fedha hizi za Benki ya India zinazokwenda Zanzibar zimeshakuwa tayari; lakini kitu kikubwa mpaka sasa fedha hizi hatujui zipo wapi, hatujui zimefikia vipi. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri juu ya hili suala la pesa hizi za Benki ya India zinazokwenda Zanzibar ambazo ni mkombozi wa matatizo ya maji kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar; wananchi wa Zanzibar wana matatizo makubwa sana ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, fedha hizi za Benki ya India aje atuambie zimefikia hatua gani na ni lini fedha hizi zinaweza kwenda Zanzibar ili ziweze kutatua kero Zanzibar?

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee na umwagiliaji wa maji. Hali ya hewa ya nchi yetu sio shwari, kwa hiyo tunaomba suala la umwagiliaji wa maji ni suala nyeti sana, lazima tuongeze suala la umwagiliaji kwa nguvu zetu zote angalau tufikie hekta milioni moja, tunaweza ku-save matatizo ya maji tuliyo nayo. Mheshimiwa Waziri nimwombe sana, hali ya hewa iliyokuwepo nchini kwetu si shwari na tukitengemea kilimo cha mvua hatuwezi kufika mahali ambapo tunapatarajia. Nchi yetu inaendelea na ukame na matatizo ni mengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, tuliangaliengalie kwa macho mapana suala la umwagiliaji ili tuweze kufikia hatua ya kuhakikisha wananchi wetu wanaweza kupata kilimo cha umwagiliaji kwa asilimia kubwa. Hii itawezesha nchi yetu kuwa na kilimo cha mafanikio. Kilimo cha kutegemea mvua hakiwezi kuondoa hali ya njaa katika nchi yetu; lazima tugeukie upande wa kuangalia kilimo cha umwagiliaji kwa nguvu zote na tuhakikishe kwamba wananchi wetu wameelekea katika kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nigusie na miradi ya vijijini. Hii miradi ya vjijini bado ni tatizo sugu; wananchi wetu wa vijijini wanapata miradi hii kwa gharama sana na kwamba inawasumbua sana kupatikana kwake. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri, katika hii miradi ya vijijini tuache kutumia majereta twende katika system ya solar ili tuweze kupata maji kwa urahisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanya ziara, tumeona faida ya matumizi ya solar katika miradi ya vijijni, kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri juu ya hili suala la kutumia solar katika miradi yetu hasa ya vijijini. Tuache matumizi wa majenereta kwa sababu wananchi wetu wanapata maji kwa gharama zaidi, lakini tukitumia solar watapata maji kwa urahisi, watapata maji kwa bei rahisi, watapata maji kwa uhakika. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri akisikilize kilio hiki kwa makini ili aweze kufanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nirejee tena kukazia suala la fedha...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja (Makofi).