Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Sixtus Raphael Mapunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya mwisho ya kufunga dimba kwenye siku hii ya leo. Ibara ya 100 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi kusema, Mheshimiwa Komu alitumia Ibara hii kutoa mawazo yake, yanaheshimika; akasema, Hotuba ya Waziri ni hewa, the same alichokifanya Mheshimiwa Kingu kutoa uhuru wake wa mawazo aliposema haina alternative. Katika mazingira kama haya tuvumiliane tu. Ukijua kucheka, lazima ujue na kulia. Sindano inapoingilia, ndiyo pale pale inapotoka. Kwa hiyo, tuvumiliane tu, tuendelee. Kwa hiyo, ili isinipotezee muda, niende kwenye hoja yangu ya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, toka Awamu ya Kwanza, Awamu ya Pili, Awamu ya Tatu, Awamu ya Nne na Awamu ya Tano, tuliona mkakati wa kukuza viwanda kwenye Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Nyerere. Ikaenda ikakuza viwanda ikatuachia viwanda vikubwa sana na viwanda vidogo vidogo. Katikati hapa viwanda vikafa na vingine vikauzwa. Hatukuwahi kupata matumaini mpaka ilipofika Awamu ya Tano. Ilipokuwa kwa kauli yake ya kusema sasa Tanzania inakwenda kwenye nchi ya viwanda ili twende sambamba na mpango wetu wa maendeleo ifikapo mwaka 2025 angalau tufike kwenye uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nayasema haya? Nayasema haya kwa sababu tunaona kabisa kuna dhamira ya dhati ya kwenda kule. Kusema ni neno moja na kutenda ni neno lingine. Tukumbuke tunakuja kwenye mkakati huu mkubwa. Kipindi tukiwa na miaka zaidi ya 20 ya kusuasua kwa viwanda, kwa namna yoyote ile ni lazima tuanze popote, aidha, tumeanza kwa usahihi sana au kwa kukosea, lakini tulipoanza tumeanza sehemu sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hadithi moja inaitwa hadithi ya jongoo na mwana jongoo. Jongoo alizaa jongoo mwana, sasa alipomwona mama yake akitembea, jongoo mwana akamwuliza mama, nina miguu mingi sana nitatembeaje? Jongoo mama akamwambia mwana, anza na wowote. Jongoo mwana alipoanza na wowote akatembea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takribani miaka 20 tumekwama kwenye viwanda, tunauliza tutoke na mguu gani? Mheshimiwa Mwijage, aanze na mguu wowote, mwisho wa siku tutatembea. Tukisema tulie kwenye mkakati, tulie kianze kipi, in process tutajua jinsi ya kwenda, lakini ni lazima tuanze na tulipoanza tumeanza sehemu sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema ni sehemu sahihi? Kwa hoja zote za kiuchumi zinafsirika. Hoja ya input, out put zinatafsirika vizuri tu. Ndani ya mwaka mmoja, Julai, 2016 mpaka Machi, 2017 vimesajiliwa viwanda 170. Kati ya hivyo, viwanda 54 vipo kwenye hatua ya ujenzi na viwanda 17 vimeanza kufanya kazi ndani ya mwaka mmoja. Huko ndiko tunakosema jongoo anza na mguu wowote, mbeleni huko tutapata njia ya kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo yote, niseme mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, niliwahi kusema na nitarudia tena kusema. Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, tunapotaka kutengeneza viwanda aidha vimekuwa viwanda vikubwa au vidogo, ni commitment kubwa ambayo tunaifanya kwenye uchumi wa nchi yetu. Factors nne hizi lazima siku zote zituongoze na zituelekeze kwenye kujenga Tanzania ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ni jambo la umeme (power), jambo la pili ni watu (manpower), jambo la tatu ni raw materials na la nne ni mtaji. Haya mambo yote ukiyaangalia ndiyo yanaweza yakatuhakikishia kwamba ndani ya miaka hii mitatu au minne tutakwenda kwenye Tanzania ya viwanda kwa kiasi gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, tumejiuliza ni kwa kiasi gani kwa viwanda hivi vidogo vidogo ambavyo nchi karibu zote zilizoendelea kama Malaysia, Ujerumani, China, walianza? Walianza na zile asilimia 89 mpaka asilimia 99 viwanda vidogo vidogo (small scale industry). Kule majumbani, mtu anaweza akakamua maziwa yake ya ng’ombe akatengeneza siagi, akaenda akauza, ndiko tunakoongelea. Hivi in process huko mbele ndivyo vitapelekea kukua kwa viwanda vingine vikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wanabeza hivi viwanda vidogo. Niseme, tumeanza sawa sawa, ila inabidi tufanye marekebisho kwenye vitu vifuatavyo: tuna viwanda vidogo vidogo vya SIDO ambavyo vinatengeneza mashine ambazo zinaweza zikawasaidia hawa watu wanaoendesha viwanda vidogo vidogo. Vile vile tuna Shule za VETA; naomba Serikali i-link hizi sekta mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu anayesoma VETA akifuzu mafunzo yake aunganishwe na SIDO kwa kile alichokuwa amejifunza ili SIDO impatie vitendea kazi kwa mkopo. Anapozidi kuendeleza ile sekta ya ufundi wake ataleta tija na viwanda vidogo vidogo vitakua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, tutaimba mpaka jua litakuchwa na kucha kama hatujaona agriculture ndiyo sehemu pekee itakayokuza viwanda, hatutatoka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuitengeneze ramani ya nchi yetu kwa zone. Sehemu wanayolima pamba, sasa tufikirie kuwa na kiwanda cha spinning kwenye maeneo ya pamba. Sehemu wanayolima mahindi, sasa tuwe na mills kubwa ya kutengeneza sembe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii watu wa Rukwa, watu wa Songea, watu wa Mbeya na Iringa wanauza gunia moja la mahindi kwa shilingi 40,000 mpaka shilingi 60,000. Likienda kwenye yale makampuni yanayonunua mahindi, pumba ili ulishe ng’ombe wako na mifugo yako, gunia moja la pumba ambalo tunaita makapi ni shilingi 200,000. Tukitengeneza hizi mills kwenye haya maeneo, tutakuwa tumewasaidia wakulima na Tanzania ya viwanda tutaiona bila shida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna maeneo wanalima alizeti. Leo hii mafuta ya Korie yanauzwa bei chini, lakini mafuta ya alizeti ya Singida, ya Dodoma mpaka Kibaigwa, unapata shilingi 18,000 mpaka shilingi 20,000 kwa ile galoni la lita tatu. Kwa nini tufike huko? Kuna gharama zinakwenda kwa yule mkulima mdogo ambazo Serikali iki-intervene; nilipoongea kwenye eneo la power, kwenye kuwakopesha mashine ili waweze kukamua, tutatoka. Ndiyo hiyo hoja tunayoiongea ya import na export kwa nini vinakuja? Kwa sababu tunavyozalisha kwanza havitutoshelezi na hata kama tunazalisha gharama yake inakuwa kubwa, automatic kutokana na hali yetu ya uchumi, tunalazimika kuingiza vitu vya nje kuja hapa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho niseme kuhusu Mchuchuma na Liganga; hapa ndipo kwenye moyo wetu. Ukiuangalia vizuri mradi wa Mchuchuma na Liganga, ndiyo mradi pekee unaoifanya Dar es Salaam na Mtwara, Mtwara na Ruvuma, Ruvuma, Njombe, Iringa, Mbeya kuja Morogoro itoke katika maana ya reli ya uhakika, chuma cha uhakika na madini mengine. Tunaongelea mwaka huu wa 17, tatizo liko wapi? Kila tukifika tunaongelea Mchuchuma na Liganga, Mchuchuma na Liganga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu tunaomba, najua kuna sehemu ataweza kuijibia Mheshimiwa Waziri Mwijage, lakini nyingine atakuja kujibu Waziri mwenye dhamana. Nawaomba kabisa, suala la Mchuchuma na Liganga, mwaka huu tufunge huu mjadala au halipo; na kama lipo tujue tunatoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho tena la mwisho kabisa, nimalizie na la matrekta. Ilikuwa SUMA JKT, ilikuja na vitu vinaitwa power tiller na wakulima wakakopeshwa matrekta kwamba sasa tutaondokana na jembe la mkono hatutainamisha tena viuno. Kilichotokea wote tunakijua.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili tufanikiwe vizuri, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kwenye sekta hiyo ya merchanization, yaani ya kumtoa mkulima kwenye jembe la mkono...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante sana na naunga mkono hoja.