Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. George Mcheche Masaju

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara nyingine tena nachukua fursa hii ninapopata nafasi hii ya kuchangia, kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye kwa rehema zake anatuwezesha kushiriki kwa ufanisi mkubwa katika vikao hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naendelea kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri ambayo imesheheni taarifa katika nyanja zote, kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Taifa hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakika Mheshimiwa Waziri Mkuu unaweza, unaweza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, pia nawashukuru Waheshimiwa Wabunge ambao wamepata fursa ya kuchangia kuboresha hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambao wameitumia haki yao ya Kikatiba kwa ufanisi ipasavyo. Niseme kwamba Katiba katika Ibara ya 63 inatoa haki kwa Bunge na mojawapo ya haki ya Bunge na majukumu yake ni kuisimamia Serikali inapokuwa inatekeleza majukumu yake ya Kikatiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majukumu haya yametajwa, ni pamoja na kuuliza maswali yoyote; swali lolote kuhusu mambo ya umma katika Jamhuri ya Muungano ambayo yako katika wajibu wake, kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakati wa Mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa Bajeti, kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu na wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano na kutunga Sheria ya Kusimamia Utekelezaji wa Mpango huo. Kutunga sheria pale ambapo utekelezaji unahitaji kutunga sheria na kujadili na kuridhia mikataba yote inayohusu Jamhuri ya Muungano ambayo kwa masharti yake inahitaji kuridhiwa. Haya ni mamlaka ya Bunge ambayo yamewekwa Kikatiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ambavyo Serikali imeleta bajeti yake katika Bunge hili, Serikali kwa namna yeyote haijapoka mamlaka ya Bunge ya kuisimamia na kuishauri Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake ya kikatiba. La sivyo, isingeleta hapa hii bajeti, lakini inajua kabisa kwamba bajeti ni lazima iende iidhinishwe na Bunge. Kwa hiyo, hoja au madai kwamba Serikali imepoka madaraka ya Bunge, siyo sahihi, ni hoja ambayo haipaswi kuzingatiwa na Waheshimiwa Wabunge
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme pia kwamba Bunge hili limepewa uhuru na haki ya kujadili, haki ambayo haiwezi hata kupingwa au kuhojiwa katika Mahakama yoyote. Hivi ndivyo Ibara ya 100 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyosema. Haki hii pia imewekwa katika Sheria ya Mamlaka na Kinga na Haki za Wabunge kwenye kifungu cha (3) na kwenye Kanuni, Kanuni ambazo zinatungwa chini ya Ibara ya 89 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, haki hii haipaswi kuzuiliwa na mtu yeyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi, kifungu cha 29 cha Sheria ya Mamlaka, Kinga na Haki za Wabunge, inafanya kosa la jinai mtu yeyote kumzuia Mbunge asichangie, asitekeleze haki yake ya msingi ya kusimamia Serikali. Hilo ni la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ambalo napenda kushauri au kulitolea ufafanuzi ni suala la instrument inayotolewa na Mheshimiwa Rais baada ya kuunda Baraza lake la Mawaziri. Hati hiyo inatungwa chini ya Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Mawaziri au kwa Kiingereza inaitwa The Ministers (Discharge of Ministerial Functions Act). Hii ni sheria ambayo inaeleza majukumu ambayo Rais anabaki nayo na hayo mengine anaamua kuwagawia Mawaziri wengine.
Baada ya Mheshimiwa Rais kuunda Baraza lake la Mawaziri, Mawaziri wameendelea kutekeleza wajibu wao, bila hata migongano kwa sababu zile Wizara jinsi zilivyotajwa, kwa mfano Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Kwa hiyo, Waziri anatekeleza hayo hayo. Cha msingi tofauti na ambavyo imezungumzwa; na hili ni jambo ambalo siyo zuri sana kwa Waheshimiwa Wabunge; Kifungu kile cha (5) ambacho kimetajwa, hakimlazimishi Mheshimiwa Rais kutoa hiyo hati, kwa sababu kile kifungu kinatumia neno “may” na tafsiri za sheria kwenye Kifungu cha 43 imeeleza vizuri kwamba neno “may” ni hiari (discretion).
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana kwa mujibu wa sheria hiyo, kama kuna jambo lolote Kifungu cha 5(2) mtu anataka kujua kwamba hivi suala hili liko mamlaka ya Wizara ipi? Kule Mahakamini ataambiwa nenda kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Atakapoenda kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali atakachokisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwamba suala hili liko chini ya dhamana ya Wizara fulani, ndiyo mwisho wa hilo suala. (Makofi)
Kwa hiyo, moja, kitu chenyewe siyo cha lazima, hata kama hapa ameandika “shall,” kilichosemwa kwenye sheria ni “may.” Cha pili Mheshimiwa Rais hakupewa timeline, hakupewa masharti ndani ya muda fulani awe ameitangaza; na cha tatu, Serikali tofauti na kilichozungumzwa hapa kwamba Serikali inafanya kazi bila mwongozo, hapana. Serikali inafanya kazi kwanza kwa kuzingatia Katiba na Sheria, kwanza Katiba, Sheria na Sera za Chama ambacho kimeunda hiyo Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa sababu ni hiari, tumwachie Rais. Kwa sababu Sheria yenyewe inasema from time to time; inawezekana sisi tukawa tunazungumza hapa, huko ameshatoa, sisi hata hatujui. Kama ameshatoa, well and good kama hajatoa, tumwachie wakati wowote atakapoona inafaa kutoa atatoa. Afterall, hajavunja sheria yoyote kwa sababu sheria yenyewe hiyo, hiyo instrument anaitoa yeye mwenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, hili suala ambalo amelisema Dkt. Mpango, Waziri wa Fedha kuhusu madai ya kuvunjwa kwa Katiba, amelifafanua vizuri ila naomba kuongeza Waheshimiwa Wabunge kwamba kifungu kilichotajwa cha 41 cha Sheria ya Bajeti, hicho kifungu hakina yale maneno yaliyowekwa pale. Muisome ile sheria, hayapo hayo maneno Waheshimiwa Wabunge, isomeni hiyo sheria. Hayo maneno yaliyosemwa, hayapo na kifungu hiki cha 68 cha sheria hii ndicho kinasema sheria hii ya bajeti yenyewe ina mamlaka ya utawala dhidi ya sheria nyingine zote zinazohusu masuala ya bajeti.
Kwa hiyo, tunatambua kwamba masuala ya matumizi ya fedha pia yanaongozwa na kutawaliwa na Katiba, Sheria ya Public Finance, Appropriation Act na Budget Act na imeweka masharti. Pale ambapo ni lazima kwa masharti yale ya kutekelezwa, Serikali italeta Bungeni, lakini kwa namna ambayo Mheshimiwa Waziri wa Fedha amesema mpaka sasa. Mambo yenyewe haya Waheshimiwa Wabunge, ni ya ndani mno ya kiutendaji. Kwa Mbunge asingeweza akayajua haya. Mkitaka kuyajua haya, mtumieni Controller and Auditor General ambaye anafanya ile kazi, anasema hapa Serikali imefanya hivi. Sisi wenyewe hatuwezi kujifanya tunao watu wa ndani kuyajua yale mambo. Kama mna watu wanawajulisha yale mambo, basi wanawa-mislead. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, naomba kusema suala la uhuru wa vyombo vya habari. Hivi vinazungumzwa juu ya Kifungu cha 18 cha hii Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naomba nishauri hivi, labda nikisome kifungu hiki: “(a) kila mtu anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake; (b) anayo haki ya kutafuta kupokea na kutoa habari bila kujali mipaka ya nchi; (c) anao uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutokuingiliwa katika mawasiliano yake; (d) anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii.”
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, unapoyasoma haya, niwarejeshe kwenye haki zenu za majukumu yenu kwenye Ibara ya 63 kama nilivyosema. Sasa (d) kwanza ibara hii inachosema ni haki ya kupewa taarifa wakati wowote kuhusu matukio mbalimbali. Haki ya kupewa taarifa, siyo haki ya kutangazwa wakati wote. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana huwezi ukaenda Mahakamani popote ukaanza kusema mimi sijatangazwa. Ndiyo maana pia kuna Waandishi wa Habari na sisi tunasoma magazeti kila siku, hata juzi waliniandika Citizen na Mwananchi. Taarifa hiyo ni mambo ambayo yameshafanyika na ndiyo maana kuna taarifa za habari katika Television na katika Redio na ndiyo vipindi ambavyo vinapendwa sana duniani. Hapa kungekuwa na tatizo, kama Waandishi wa Habari wangekuwa wanazuiliwa hata kuandika chochote kinachoendelea humu ndani, naona Waandishi wa Habari wako pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku Mheshimiwa Waziri Mkuu alipowasilisha hoja yake, Mwandishi wa Citizen aliniandikia ki-note hapa, akasema Mheshimiwa AG tunaomba maoni yako kuhusiana na maoni ya Kambi ya Upinzani. Nikamwambia kwamba subiri majibu ya Serikali tutakapokuwa tunahitimisha na akaandika hivyo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa hakuna haki ya msingi na niseme tu; moja, itakuwa siyo vyema sana ni matumizi mabaya ya haki zetu sisi Wabunge kuacha kuchangia kutetea Jimbo lako, eti kwa sababu haki iliyoko hapa siyo haki ya mwonekano; haki iliyopo kwenye Bunge ni haki ya kujadiliana na kufanya maamuzi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi ya Bunge hayafanywi kwa mwonekano, yanafanywa kwa kujadiliana, kwa kuzungumza au kuandika au kwa kupiga makofi kama unaunga mkono hoja. That is how decision are made. Kwa hiyo, itakuwa siyo jambo jema, nami nimewatetea sana kwenye kesi zinazowakabili kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na kesi 52 za uchaguzi, tayari kesi 29 tumeshashinda, unatetea Wabunge waje wawakilishe wananchi wao hapa, halafu wana-abdicate majukumu yao, that is not fair. (Makofi)
Wananchi wanachotaka ni what is there kwenye Jimbo; ni kitu gani? Ni aibu sana kwa Waheshimiwa Wabunge. Nawashauri Waheshimiwa Wabunge wote, tutumie vizuri Bunge la Bajeti kwa sababu ndilo Bunge ambalo tunasimama kutetea kipato cha Taifa kwa ajili ya maslahi ya watu wetu kule Majimboni. Ni aibu kuacha kuchangia eti unadai kwamba unataka uonekane kwenye television and that is not very fair.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niseme tu kwa mara nyingine kwamba, naunga mkono hoja hii. Ahsante sana.