Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya. Pili, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mwijage, kwa kweli anafanya kazi nzuri sana, ameonyesha umahiri wake kwa kujitahidi kuanzisha hivi viwanda ambavyo ametusomea kwenye hotuba yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niongee machache kuhusu Mkoa wangu wa Morogoro. Nianze kwa kupongeza. Naishukuru Serikali yetu kwa jinsi inavyowezesha Mkoa wetu wa Morogoro kwa viwanda ambavyo vinatarajiwa kujengwa. Ni viwanda vingi kiasi. Nikianza na viwanda vya Nyama, Matunda, Kiwanda cha Sukari ambacho kipo Mkulazi watajenga na Kiwanda cha Mbigili Sukari, watajenga; pamoja na Kiwanda cha Sigara ambacho na chenyewe kitajengwa Morogoro; na bila kusahau Morogoro Star City ambapo vitajengwa viwanda mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana hivi viwanda viweze kujengwa kwa wakati ili viweze kuajiri hasa vijana pamoja na wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikimaliza kusema hivyo, kwa Mkoa wangu wa Morogoro kuna viwanda ambavyo vilibinafsishwa na havifanyi kazi. Kwa mfano, Kiwanda cha Canvas, Kiwanda cha Ngozi, Kiwanda cha Ceramic, MOPROCO na Kiwanda cha Juice ambacho kipo Kingorwila. Naomba sana Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake amesema kuwa viwanda hivi hasa MOPROCO pamoja na Canvas viko karibu kuanza. Naomba viweze kuanza kusudi viweze kutoa ajira hasa kwa vijana pamoja na akinamama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, naomba kuvipongeza na kuwapongeza wale wawekezaji wa viwanda vya Morogoro ambavyo mpaka sasa hivi vinafanya kazi na vinaajiri sana akinamama na hasa vijana, wasichana na wengine. Nikianza na Kiwanda cha Tumbaku; kiwanda hiki kinaajiri akinamama wengi na kinafanya kazi masaa 24. Kwa hiyo, nawapongeza kwa kazi hiyo nzuri wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Mtibwa Sukari kinafanya kazi, Kiwanda cha Kilombero K1 na K2 vinafanya kazi; Kiwanda cha Maji ya Udzungwa kinafanya kazi vizuri na Kiwanda cha Nguo kinafanya kazi. Bila kusahau Mazava, ingawa Mheshimiwa Waziri amesema hakifanyi kazi, lakini kinafanya kazi ambapo kuna vijana wengi hasa wa kike, wanafanya kazi kwenye kiwanda hicho. Kwa hiyo, nawapongeza kwa sababu wanasaidia vijana, akinababa na akinamama hasa wa Mkoa wa Morogoro kwa kupata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa kilimo hapa, wananchi wengi Tanzania asilimia 75 wanategemea kilimo, lakini viwanda vya mbolea ni matatizo bado. Naomba kuuliza Mheshimiwa Waziri, Kiwanda Mbolea cha Kilwa – Lindi ni lini kitaanzishwa? Pia hapo hapo, Mheshimiwa Waziri alisema kuwa kuna kiwanda cha Pwani, nacho naomba aelezee kidogo kama ni cha mbolea. (Makofi)

Pia namwomba Mheshimiwa Waziri na Serikali ya Mheshimiwa Rais, pia waweze kupanua wigo kwa upande wa viwanda vya kilimo pamoja na pembejeo kwa sababu asilimia 75 ya wananchi wanategemea kilimo na kwenye kilimo ndiyo tunategemea uchumi wa mwananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukisema viwanda tunamaanisha mambo mengi. Hatuwezi kuwa Tanzania ya viwanda kama hatuna umeme na hatuwezi kuwa Tanzania ya viwanda bila kutegemea kilimo. Ni lazima tuwe na umeme kwa upande wa nishati na kilimo kwa upande wa malighafi. Pia ni lazima tuwe na maji; huwezi kuwa na kiwanda bila ya maji. Vile vile ni lazima tuwe na ardhi na miundombinu muhimu ikiwepo barabara, reli na viwanja vya ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri aweze kushirikiana na hizi sekta kusudi tuweze kuanzisha hivi viwanda na Tanzania iweze kuwa Tanzania ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu fedha za miradi. Kutokana na hotuba ya Mheshimiwa Waziri tumeona kuwa mpaka Machi mwaka huu fedha za maendeleo ilikuwa ni asilimia 18.92. Ikiwa fedha za maendeleo hazitoki, ni shida sana kufanya maendeleo ya viwanda. Kwa hiyo, nashauri kuwa fedha tunazozipitisha hapa Bungeni ikiwezekana ziweze kutoka na kupelekwa kwa wakati kwenye miradi husika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siwezi nikamaliza bila kuongelea wanawake. Wanawake wa Kitanzania wamejitoa sana kwenye biashara. Wanafanya biashara ndogo, za kati na biashara za Kimataifa, matatizo yaliyopo ni masoko. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iwajengee mazingira mazuri waweze kupata masoko na kuuza bidhaa zao. Pia hapo hapo, naomba waweze kuunganishwa na TBS pamoja na TFDA kusudi mazao yao na bidhaa zao ziweze kuwa na thamani ya kuweza kuuzwa ndani na nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wangu wa Morogoro bado una ardhi kubwa. Bado tunaomba zaidi na zaidi wawekezaji hasa kwenye viwanda vya maziwa, kwa sababu bado tunazo ng’ombe na kwenye kilimo bado tuna sehemu kubwa ambayo tunaweza kulima matunda, kuendelea kulima mpunga ingawa kuna wawekezaji, lakini hawatoshi. Kwa hiyo, naomba sana tuweze kupata hao wawekezaji na madawa ya kilimo pamoja na mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa SIDO; huwezi kufanya viwanda hasa viwanda vidogo vidogo bila ya SIDO. Kwa hiyo, naomba sana kuwepo mkakati maalum ambao unaweza ukawaunganisha hawa wafanyabiashara pamoja na SIDO.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii na Mwenyezi Mungu akubariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Ahsante sana.