Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Deogratias Francis Ngalawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. DEO F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuchangia katika Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, najikita moja kwa moja kwenye Mradi wa Liganga na Mchuchuma. Ikumbukwe katika Bunge lako tarehe 19 mwezi wa Nne niliuliza swali Liganga na Mchuchuma, fidia kwa waliopisha maeneo itakuwa ni lini? Nikajibiwa kwamba italipwa mwezi Juni, 2016. Pia Bunge lako lilitaarifiwa kwamba Mradi wa Liganga na Mchuchuma ungeweza kuanza mwezi Machi, 2017. Sasa kitu ambacho nakiona ni kwamba, Serikali haina dhamira ya dhati juu ya Mradi wa Liganga na Mchuchuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukijaribu kufuatilia maelezo ya Mheshimiwa Waziri, naomba ninukuu kwa kusoma, Mheshimiwa Waziri anasema:-

“Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2016/ 2017 Wizara kupitia NDC iliendelea na majadiliano juu ya mauziano ya umeme kati ya Shirika la Umeme TANESCO na kampuni ubia. Mfumo uliokubalika na pande zote mbili ni mwekezaji kujenga mtambo wa kufua umeme, kumiliki na kuendesha, (build, own and operate). Mauzo ya umeme kwa TANESCO hayajumuishi gharama za uwekezaji kuhusu ujenzi wa mradi. Kamati ya Taifa ya uwekezaji imepitia kwa mara nyingine vivutio vilivyoombwa na mwekezaji kwa lengo la kutafuta manufaa zaidi kwa Taifa katika mradi huo”.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, Mradi wa Liganga na Mchuchuma umewekwa kama ni mradi kielelezo (flagship project). Hata hivyo, kitu ambacho nakuja kukiona hapa inaonekana kwamba hakuna master plan ya mradi huu kuanza. Leo hii tunauzungumzia hata fidia haijalipwa, wakati mwekezaji anasema tayari ana hela za kulipa, lakini sisi kama Serikali yenyewe inazungumza kwamba bado wanaendelea na mazungumzo juu ya power purchase agreement kati ya mbia na TANESCO. Sasa najiuliza pana tatizo gani? Kwa sababu tungepewa schedule of activities mpaka mradi ku- take over, lakini leo hii bado tunazungumzia kwamba tunaendelea na majadiliano sasa tujiulize haya majadiliano yataendelea mpaka lini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati nachangia Wizara hii mwaka wa jana tulizungumza kwamba tungepewa road map. Ifike mahali kwamba tujue kwamba mwezi huu mpaka mwezi huu, mwaka huu mpaka mwaka huu activity fulani inafanyika ili tuweze kujua kwamba itakapofika muda fulani mradi huu uwe ume-take over. Hiyo tulikuwa tunaizungumza hivyo kwa maana ya tuweze kum-pin mtu ambaye anatuletea shida hapa kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kama tunaamua kuzungumzia tu kwamba tutaendelea tu na majadiliano itafika 2020 huu mradi haujaanza, fidia haijalipwa, hayo makubaliano ya TANESCO hayapo, hizo incentives ili Serikali ije itoe GN haziatakuwepo. Kwa hiyo, napenda kusikitika kwamba huu mradi hatujauwekea kipaumbele. Inawezekana zipo incentives ambazo zinatakiwa na mwekezaji lakini vile vile lazima tuangalie multiplier effect ya mradi wenyewe upoje.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu unaleta ajira 33,000, hiyo hatujaiangalia, lakini tunaangalia zile taxation tu za mwanzo. Ifike mahali; kwa sababu Baraza la Uwekezaji Mwenyekiti wake ni Waziri Mkuu, kwa hiyo, maana yake huu mradi unafahamika vizuri. Kama kuna shida basi tujue kwamba huu mradi haufanyiki ili watu waendelee na mambo mengine. Leo hii ndugu zetu wa Ludewa kule wamepisha mradi lakini fidia hawana, maeneo yale yanashindwa kuendelezwa, yanashindwa kulimwa, lakini hakuna tamko lolote la Serikali ambalo linawapelekea sasa wananchi wale wafanye nini. Mwekezaji anasema hela anayo, kama hela ya mwekezaji inaleta shida, basi Serikali ingebeba jukumu la kulipa fidia huku ikiendelea na hayo mazungumzo ili iwafanye wale watu waendelee na shughuli nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukijaribu kuangalia licha ya ajira 33, 000 zitakazokuwa zimeletwa na mradi huu, tunatarajia kwamba huu mradi ungeweza kuleta population ya watu wasiopungua laki tatu ndani ya eneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kuja kwa mradi huu maana yake ungeweza kuanzisha viwanda vingine kwa ajili ya kuweka value addition ya mazao yanayolimwa na mikoa na wilaya jirani. Hata hivyo, inaonesha ni kwamba Serikali yenyewe ime-base tu kwenye maeneo machache, kitu ambacho na chenyewe si sawa kiuchumi. Ifike mahali kwamba hiyo tax kwa mfano tukii-wave, kuna impact nyingine kwa jamii kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumza kwamba huu mradi haupewi kipaumbele kwa sababu pia unakuta hata ile miundombinu yenyewe haijawekwa. Leo hii tuna barabara inayoenda kwenye chuma cha Liganga, barabara ya kutoka Mkiu kuelekea Madaba, mpaka leo hii tunaambiwa tunafanya rehabilitation hakuna utaratibu wowote kusema inaingia kwenye upembuzi yakinifu, iende kwenye usanifu wa kina, barabara zijengwe ili kwenda kwenye huo mradi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii nchi inazungumza haina chuma, lakini chuma kimelala pale Liganga, leo chuma tunaagiza. Kwa hiyo ikifika mahali unakuta sasa hivi vitu vinasuasua. Tumezungumzia juu ya Reli ya Mtwara kuja Mbamba Bay kutoka Mbamba Bay inakuja Mchuchuma inakwenda Liganga; sijajua utaratibu ukoje.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo unaweza kuona kwamba Serikali na yenyewe inakwepa. Kama tatizo ni mwekezaji, basi ifute huo utaratibu ili tujue kwamba huu mradi haupo tunatafuta mwekezaji mwingine ili tuweze ku- move, kwa sababu haiwezekani miaka mitano, sita tunazungumzia Liganga tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Liganga kwa mara ya kwanza imezungumziwa mwaka 1929. Sasa mwaka1929 mpaka leo tunazungumza tu Liganga, wazee wetu wanakufa, watoto wetu wanakufa sisi wote tutaenda tutakufa Liganga itaendelea kubaki palepale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unapozunguzia uchumi wa viwanda Tanzania huwezi ukaiondoa chuma cha Liganga na huwezi kuondoa makaa ya mawe Mchuchuma. Makaa ya mawe Mchuchuma yanatoa megawati 600, leo nchi inatumia megawati 1050... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. DEO F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.