Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri na wataalam wote wa Wizara hii kwa juhudi kubwa wanayoifanya ya kuleta mabadiliko kwenye Wizara hii muhimu na kuinua ubora wa elimu hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilieleza Bunge kuwa wataboresha shule za umma kuanzia miundombinu, vitendea kazi, walimu na kadhalika ili ziweze kutoa elimu bora na kurejesha heshima ya shule za sekondari. Kwa muda wa mwaka unaoishia Juni, 2017 ni shule ngapi zimeboreshwa na jukumu hilo limefikia wapi kwa jumla?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilianzisha vikao na wadau wa shule binafsi ili kuweka standards za ada za shule za private ambazo ni kubwa mno na kila shule inatoa ada kwa utaratibu wake na hakuna control yoyote. Zipo shule zinatoza ada shilingi milioni tatu kwa mwanafunzi kwa mwaka bado kuna bus fee na michango mingine. Serikali ituletee hapa Bungeni taarifa ya vile vikao vimefikia wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo kubwa sana la upungufu wa miundombinu kwenye shule za msingi na sekondari. Watoto wanasoma zaidi ya 100 kwenye darasa moja, lakini wapo wanaosoma kwa shift, wanaingia saa 2.30 asubuhi wanatoka saa 6.30 mchana na wengine saa 7.00 mchana mpaka saa 10.00 jioni. Watoto hawapati muda wa kutosha kupata masomo na vipindi vya michezo, dini na mazoezi. Hakuna nyumba za walimu, wengi wanakaa kwenye nyumba za udongo huko mitaani, wengine wanakaa walimu watatu mpaka wanne kwenye nyumba moja hata ule uhuru wa kibinadamu hakuna. Walimu wanakatishwa tamaa na mazingira wanayofanyia kazi na yale wanayofundishia. Serikali itueleze mpango wa muda mrefu kuhakikisha walimu wanafundisha kwa moyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iboreshe na kuimarisha Ofisi za Ukaguzi wa shule za msingi na shule za sekondari kwa kuwapa magari ya ukaguzi kila Wilaya kwa ajili ya Mkaguzi wa Shule ya Msingi na gari lingine kwa shule za sekondari; Halmashauri za Wilaya iweke mafuta kwenye magari hayo ili muda wote wawe field na motisha uwepo kwa walimu wote hasa wale walio kwenye mazingira magumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeweka sheria ya kurejesha mikopo kwa elimu ya juu na kuweka asilimia 15 kila mwezi. Japokuwa ni sheria, lakini hii sheria inaumiza sana walimu ambao mishahara yao ni midogo. Ni vema waangalie utaratibu wa kuwasaidia walimu walipe kwa asilimia 7 kwa muda mrefu, lakini waweze pia kumudu maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madai ya walimu ni vilio na ni kero ya muda mrefu. Natumaini uhakiki umeisha na wenye vyeti fake wametambuliwa. Kuna walimu wa Kaliua waliajiriwa mwaka 2014 hawakulipwa mishahara kwa mwezi Mei na Juni, 2014 (miezi miwili) huku wamo waliolipwa mishahara yao. Pia malimbikizo ya madai yasiyokuwa ya mishahara ni mengi sana hayajalipwa kwa miaka zaidi ya saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kuwepo kwa mkanganyiko wa ubora wa vitabu vitakavyotumiwa na wanafunzi hasa primary school na zile za mchepuo wa kiingereza na uwepo upungufu mkubwa kwenye vitabu hivi vya shule za awali ambapo ndipo eneo watoto wanapata msingi wa elimu yao, Serikali itueleze mikakati iliyopo ya kuhakikisha vitabu vyote vinavyotumika mashuleni vimefanyiwa uhakiki na kuondoa changamoto iliyojitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatuambia nini kuhusu uwepo wa Mamlaka ya Udhibiti wa Vitabu (TEA) lakini wameshindwa kufanya kazi ya udhibiti wa elimu yetu hasa shule za msingi. Nashauri kuwepo na taasisi binafsi zinazotengeneza vitabu vya shule na visisambazwe mashuleni kabla ya kupitiwa na kuhakikiwa na mamlaka za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la adhabu kwa watoto wa shule ni jambo jema kwa lengo la kumrekebisha mtoto na kumweka kwenye njia nzuri. Serikali inajua kuwa walimu wanatoa adhabu kubwa sana kupita kiasi? Watoto wanavuliwa nguo zote mpaka za ndani, wanachapwa mpaka wanalazwa na wengine wanapoteza maisha. Serikali itoe tamko leo Bungeni la kupiga marufuku adhabu za aina hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo Kikuu cha Sokoine ni chuo pekee cha kilimo hapa nchini kinachotoa elimu ya juu kwa masuala ya kilimo, ufugaji wa kisasa, nutrition, misitu, mazingira, tafiti mbalimbali na fani nyingine. Serikali kwa miaka mingi haijabadilisha miundombinu ya chuo hiki pamoja na kwamba kila mwaka udahili unaongezeka na wanafunzi ni wengi. Nini mpango wa Serikali kuboresha chuo hiki tunapoelekea kwenye uchumi wa viwanda ambapo tutafika huko kwa njia ya kilimo?