Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Waziri na Naibu Waziri, kwa jitihada kubwa wanazochukua katika kuinua elimu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia hotuba ya Wizara hii katika maneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, shule ya kidato cha tano. Naipongeza sana Serikali kwa kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne. Hatua hii ni ya kupongezwa sana kwa sababu imetoa fursa kwa Watanzania wengi sasa kupata elimu bila kujali idadi, uwezo au rangi. Hata hivyo, kuna tatizo katika baadhi ya maeneo mbalimbali nchini kutokuwa na shule za kidato cha tano mfano ni Wilaya ya Kilindi. Naomba hoja yangu ipate majibu, hivi ni kweli hatuna hata shule moja katika hizi zilizopo Kilindi ambazo tunaweza kuzipandisha ziwe za kidato cha tano? Naomba majibu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni kuhusu VETA. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Wilaya ya Kilindi ilikuwa ni miongoni mwa Wilaya chache ambazo zilitengewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA. Wilaya tayari ilikwishatenga eneo kwa ajili ya ujenzi na ikumbukwe toka mwaka 2014 Wizara ilitamka itajenga chuo. Hivi ni hatua zipi zimefikiwa au kuna tatizo gani hasa?

Vyuo vya VETA vinatoa fursa kwa wananchi hususan vijana wetu ambao hawajabahatika kuendelea na kidato cha kwanza kupata fursa ya kupata ujuzi mbalimbali. Kilindi hatuna FDC, Chuo cha VETA ni hitaji muhimu kwa Wana- Kilindi, vijana wetu wa Kilindi wanahitaji la chuo hiki. Naomba Wizara iliangalie suala hili kwa jicho la ziada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, uhaba wa walimu hasa wa sayansi. Tatizo la walimu ni changamoto kubwa sana, shule nyingi zina walimu wachache kuanzia shule za msingi hadi sekondari. Katika Jimbo langu la Kilindi tuna tatizo la walimu wa masomo ya sayansi. Niipongeze Wizara kwa kutupatia walimu sita wa shule za Serikali, lakini bado uhitaji ni mkubwa sana. Naiomba Wizara itupatie walimu wa kutosha. Ili dhana ya Serikali yetu kwenda kwenye nchi ya viwanda ifanikiwe ni lazima Serikali isomeshe walimu wa kutosha wa masomo ya sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri ili tuondokane na tatizo la uhaba wa walimu wa sayansi, Wizara ione namna ya kupunguza gharama za masomo katika vyuo vyetu ili kuwapa wazazi motisha. Vilevile ajira za walimu wa sayansi zipewe kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne ni kuhusu uwiano wa ugawaji wa walimu. Bado kuna tatizo la uwiano wa ugawaji na upangaji wa walimu katika nchi yetu. Kwa mujibu wa Ukaguzi wa Ufanisi (Performance Auditing) iliyofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti wa Serikali (CAG) kuna tatizo kubwa katika eneo hili. Kuna baadhi ya mikoa mwalimu mmoja anafundisha watoto 26 wakati Mikoa mingine mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 46, hili ni tatizo kubwa, hali hii inadumaza maendeleo ya elimu. Niiombe Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na TAMISEMI, ipitie upya mgawanyo huu ili kuleta usawa wa maendeleo nchini kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuamua kujenga hosteli pamoja na maktaba, yote haya yamefanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ujenzi wa mabweni utapunguza usumbufu na kuleta utulivu kwa vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.