Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Prof. Jumanne Abdallah Maghembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kuchukua fursa hii kukushukuru sana wewe binafsi na Bunge lako Tukufu kwa kupokea, kujadili na kutoa maoni na ushauri pamoja na maelekezo katika maeneo pengine kufuatia hotuba ya makadirio ya bajeti ya Wizara yangu kwa mwaka 2017/2018. Aidha, namshukuru sana Mheshimiwa Atashasta Nditiye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa uchambuzi na maoni kuhusu utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu wa fedha unaokuja na Maoni ya Kamati Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maoni na Ushauri wa Kamati umegusa maeneo ya ufinyu wa bajeti, ushirikishaji wa mamlaka nyingine za Serikali na wananchi, utangazaji wa utalii, migogoro ya ardhi kati ya maeneo yaliyohifadhiwa na wananchi, mgongano wa sheria, uwekaji wa mipaka, utatuzi wa mgogoro wa Loliondo…
udhibiti wa ujangili na masuala kuhusu maendeleo ya sekta ya utalii nchini. Ushauri na maoni haya ya Kamati utazingatiwa na wizara na tutaufanyia kazi kwa jinsi ambavyo tutaweza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nafasi hiyo hiyo namshukuru Mheshimiwa Esther Nicolas Matiko, Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kutoa maoni ya kambi yake na maoni hayo na yenyewe tumeyapokea na tutayaangalia kwa makini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba yetu imejadiliwa na Waheshimiwa Wabunge kwa undani sana; jumla ya Waheshimiwa Wabunge 142 walijadili bajeti yetu. Waliochangia kwa mdomo walikuwa Waheshimiwa Wabunge 76 na walioleta maandishi kama mchango wao ni Waheshimiwa Wabunge 66.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda ambao umenipa na michango ambayo imeletwa ukubwa wake, ubora na umuhimu wake hatutaweza kuyatendea haki mawazo yote haya yaliyotolewa katika hotuba hii ya dakika 30. Ninachowaomba na kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge ni kwamba tumepokea michango hii na tumeifurahia kwakuwa critical review ya performance ya Wizara ya Maliasili na Utalii na tutaichukua kwa hali hiyo na kushughulika nayo mpaka tupate majawabu. Tunategemea kabisa kwa ushirikiano ambao umeonyeshwa hapa, willingness ya Waheshimiwa Wabunge kushiriki na kutusaidia hakuna litakaloshindikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze kujibu masuala ambayo yamejitokeza na yamejitokeza kwa nguvu, si kwa umuhimu kwamba yale ambayo hatutayafikia siyo muhimu, ni kwa sababu tu ya muda.

Kwanza nitaongelea juu ya Kamati ya Wizara tano ambayo imeundwa kwa ajili ya kutatua migogoro ambayo inaisibu Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Kilimo, Wizara ya TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu na pengine inasibu Wizara ya Mazingira lakini ikiwa chini ya Uenyekiti wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati hii imeundwa na Kamati ilipoundwa imepitia taarifa zote za migogoro ya ardhi na migogoro mingine ambayo ni kati ya wananchi na Serikali katika maeneo mbalimbali ya nchi hii. Jumla ya ripoti 19 zimepitiwa na ni zote ambazo zimetokana na Bunge, Serikali yenyewe na kadhalika. Ripoti hizo zikaifanya Kamati ikatembelea mikoa kumi kama sampuli ya maeneo ambayo yameguswa na ripoti na ikaja na migogoro 1,246 ambayo inahitaji kutatuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ikawasilisha migogoro hiyo kwa makatibu wakuu ambao nao tarehe 8 Mei, 2017 wakaiwasilisha kwa timu ya Mawaziri wanne. Tukaipokea ripoti ile na tukaona kwamba Kamati ile iendelee na kazi ili iweke mkakati wa utekelezaji wa ripoti ambayo wameileta. Tumewakea timeframe na kwamba kabla ya tarehe 10 Juni, 2017 wataiwasilisha ripoti yao kwa Makatibu Wakuu wa Wizara sita na tarehe 10 Mawaziri wa Kilimo, Maliasili, TAMISEMI, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais tutakutana chini ya uenyekiti wa Waziri wa Ardhi kuiangalia ripoti hiyo na mkakati wake wa utekelezaji kabla hatujapeleka ripoti hiyo kwa viongozi wetu kwa kupata kibali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo,nataka niwaombe sana wale wote ambao wameongea hapa kwa hisia kubwa juu ya migogoro iliyopo kati ya hifadhi zetu na mifugo, kati ya hifadhi zetu na wakulima, kati ya hifadhi zetu na watu waliojenga katika maeneo mbalimbali kwamba wavute subira kwa sababu hili jambo linafanyiwa kazi na kazi hii inafanywa kwa nguvu sana na kwa usimamizi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutapata majawabu na hatutateteleka katika kuyatekeleza. Nimemsikiliza sana Mheshimiwa Joseph Musukuma, classmate wangu Profesa Anna Tibaijuka jana na nimewasikiliza sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu wakina Mheshimiwa Kanyasu, Mheshimiwa Joseph Kakunda na Mheshimiwa Cosato Chumi, nimewasikiliza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewasikiliza na wengine na jambo hili tunakwenda kulitekeleza, lakini wakati tulipokuwa tunasikiliza mambo haya pia tumejifunza vitu hapa maana yametolewa madarasa aina mbalimbali. Kutokana na madarasa hayo tumejifunza kwamba kuma muingiliano mkubwa sana wa shughuli za kibinadamu na uhifadhi. Hili ni jambo ambalo lazima tuanze nalo. Pili ni kwamba tunahitaji kilimo kwa ajili ya kushiba kwetu vile vile kwa ajili ya kujenga uchumi wa nchi yetu, lakini kilimo kinahitaji maji kwa ajili ya umwagiliaji. Kwa sababu hiyo kama tunataka kumwagilia maji na tunaongea na kusema kwamba hatuwezi kuwa na tija katika kilimo lazima tuhifadhi misitu kule ambako maji yanatoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji sana mifugo, na mimi ninaamini kabisa kwamba hili ni giant kubwa ambalo limelala. Mchango wa mifugo bado hatujauona. Mchango wa mifugo ule unaouona kule Uholanzi, kwenye ile cattle belt ya Marekani, hujauona hapa. Potential ya hilo giant ipo na giant hilo linahitaji maji, giant hilo linahitaji mvua, giant hilo linahitaji kutunzwa na linahitaji liepushwe na magonjwa na maambukizi mengine ya mifumo ya ikolojia ambayo inaweza kuzingatiwa na hifadhi zetu. Kwa hiyo, tunahitaji misitu itupe mvua, itupe maji, itupe hewa na itupe bidhaa nyingine zile za kiikolojia ili maisha yetu yaweze kuwa bora na vilevile ili tuweze kufanya shughuli zetu hizi za uchumi, kilimo, mifugo na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji sana wanyamapori na Mwenyezi Mungu ametupa wanyamapori hawa sisi Watanzania kwa ajili ya utalii. Kama mmejumlisha tarakimu vizuri hapa sekta hii ya utalii inachangia asilimia 21.4 ya Pato la Taifa ukijumlisha aslimia 3.9 ya misitu na asilimia 17.5 ya utalii na wanyamapori. Lakini wanyama hawa wanatusaidia pia katika kutafuta dawa kwa maisha yetu ya baadaye, ni viumbe ambavyo lazima tuwe nao ili kuhakikisha maisha yetu na longevity ya maisha yetu. Kwa hiyo, wakati umefika, kwa kweli, na amesema hapa Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati. Sisi katika kujifunza mambo yaliyopita hapa ndani tumejifunza kwamba wakati umefika sasa tusiwe na makampuni zaidi ya manne ndani ya sekta hii ya wanyamapori, tuwe na kampuni hii moja tu ambayo itapunguza gharama katika uendeshaji. Tutafundisha Jeshi la Wahifadhi na jeshi hilo tutakalolitengeneza ni jeshi moja tu ambalo litakuwa na malezi chini ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania ili kujenga nidhamu, kuheshimu haki za binadamu na kufanya kazi kama ambavyo maslahi ya Taifa yanahitaji. Kwa hiyo, jeshi hilo ambalo tunaliandaa hivi sasa (Jeshi Usu) litakuwa na chain ya command moja na litawajibika kijeshi kwa makosa ya haki za binadamu na usaliti wa Taifa au usaliti wa uchumi wa nchi yetu. Kwa hiyo, hilo ni moja ya masomo ambayo tumejifunza hapa.

Waheshimiwa Wabunge wengi wameongelea kwa uchungu juu ya utalii. Kwanza niseme kwamba tumefurahi sana kupata michango hii ya utalii, lakini nimeona katika maono yetu na definition ya utalii naona kama kuna tofauti hivi ya mawazo. Sisi tumetumia maana ya utalii kama inavyotumiwa na United Nations Tourism Organisation, hiyo ndiyo definition; ya mtu anayeondoka pale alipo kusafiri kwenda nchi za nje au kutoka pale alipo kwenda mahali pengine kwa shughuli inayozidi saa 24 lakini haifikii mwaka mzima akiondoka nyumbani kwake; hata kama anakwenda kwa biashara, anakwenda kwa vitu vingine, lakini wakati akiwa kule atakuwa anatoa huduma ambazo mtalii akifika mahali anazipata kama kukaa kwenye hoteli na kutumia huduma za aina hiyo kule anakokwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo takwimu ambazo tumezitoa ni takwimu ambazo zimekusanywa vizuri sana na timu ambayo inaundwa na Wizara yangu ya Maliasili na Utalii, Jeshi la Uhamiaji, Benki Kuu ya Tanzania, Kamishna wa Utalii kule Zanzibar na huduma zetu za kiuchumi wa ndani ya nchi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Msemaji wa Kambi ya Upinzani wakati ukiwa na nafasi nitakupa hizi takwimu ili uweze kuona ni jinsi gani tumezikokotoa na ni jinsi gani ambavyo ile thought process imekwenda na kwamba zile takwimu ambazo umetupa hapa si za kweli. Tumepata mawazo, na ni kweli kwamba utangazaji wetu wa vivutio vya utalii bado ni mdogo kwa sababu ya fedha ambazo tunazo. Hata hivyo Serikali imeondoa hatua ya kwanza na inakwenda mbele na mwelekeo ambao tunao na mipango ambayo tunayo inatuwezesha sasa tupige hatua kubwa katika kuujulisha ulimwengu kwamba yule giant wa utalii anayeitwa Tanzania sasa ameanza kutembea. Kama mnavyokumbuka, sisi kwa tathmini ya World Economic Forum ya mwaka 2014, sisi ni wa pili baada ya Brazil kwa kuwa na vivutio vizuri, hasa vile vya nature, tukifuatia Brazil huku duniani, hakuna nchi nyingine tena. Lakini kuanzia mwaka 2014, tukafika mwishoni mwa 2015, tumeanza kushuka kwa sababu tumekuwa na maono tofauti kwa jinsi ambavyo tunaviona hivi vivutio vya utalii. Wengine kati yetu wanayaona ni maeneo mazuri ya kuchunga ng’ombe, wengine wanaona ni maeneo mazuri ya kupeleka utalii, wengine wanaona ni maeneo mazuri ya kulima, na kwa sababu ya vitendo hivi mbalimbali tumefika mahali sasa tumefika Taifa la nane katika mataifa ya duniani katika ubora wa vivutio vyetu vile ambavyo ni natural.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka niwaombe ndugu zangu, tuvilinde hivi vivutio vyetu vya utalii kama tunavyoweza kuweka mboni na kulinda macho yetu, na hatujachelewa. Hatujachelewa kwa sababu nina imani kabisa hii Kamati yetu itaweka matumizi mengine hapa, matumizi mengine hapa na utalii na uhifadhi hapa na tutarudi kule ambapo tulikuwa. Katika Bara la Afrika kuna vivutio vya kimataifa, vya kidunia 50, kati ya hivyo 50, vivutio vya kwanza nane vinatoka Tanzania. Tusiharibu jambo hili zuri namna hii kwa kuwa tu tunataka tuoneshe kwamba sisi we are on top of the world and we can use it for anything, tusifanye hivyo. Tulinde na tuangalie ni kitu gani kinaleta ugali ndani ya midomo yetu, na kule kwingine tuangalie ni namna gani ambavyo sasa tutaboresha kilimo. Hatuwezi kulima sasa mashamba kwa kukimbilia kulima hekta 200 ili tupate magunia 200 ya mahindi, lazima tulime hekta 10 tupate magunia 200. Lazima tufuge vizuri tupate maziwa, tupate nyama na mazao ya kufuga mazuri ili tufurahie nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo changamoto katika utalii. Moja ya changamoto iliyotajwa hapa ni leseni. Ndugu zangu nawaomba mnielewe, leseni za biashara zinatolewa kwenye categories mbalimbali. Leseni ni kibali cha kufanya biashara, sio kodi. Mtu mwenye kaduka kwenye mtaa tunapoishi anakata kodi lakini kodi ya mtu mwenye duka la mtaani ni tofauti na kodi ya Kampuni ya Mabasi ya Shabiby, ni tofauti na kampuni ya ndege na ni tofauti na kampuni za aina nyingine. Katika utalii, tangu mwaka 1992 leseni ya kufanya utalii ni dola 2000. Nimewawekea kwenye bag sheria zote ambazo zinaongoza maliasili na Sheria ya Utalii nimewawekea mule ndani na zile kanuni za leseni na namna ya kufanya hiyo biashara nimewawekea kwenye lile bag; naomba mzisome na mzielewe vizuri. Mtu anayepandisha watu Mlima Kilimanjaro akapandisha kundi la watu kumi, kila mtu mmoja kwa bei ya sasa analipa dola 4,000. Kama wako kumi watalipa 4,000 mara kumi na mtu yule anaweza kupandisha makundi matano mpaka sita ya watu hao kwa mwaka. Mimi nina rekodi kule kwenye Wizara kwa hiyo najua. Kwa hiyo huwezi kusema kwamba ni mdogo asilipe leseni ya dola 2,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nadhani interpretation hapa na udogo na ukubwa una tofauti. Udogo na ukubwa unaangaliwa kwenye kulipa corperate tax, wakati wa kulipa kodi ile asilimia 30 ndiyo unaangalia mdogo kwa sababu ya biashara yake ilivyo ndogo na mkubwa kwa sababu biashara yake ni kubwa. Lakini katika kukata leseni, ni lazima tuangalie biashara kama biashara ya kawaida na tumeanza kupanua utalii katika zones mbalimbali, katika kanda mbalimbali. Upande wa Kusini, tunaboresha miundombinu katika mbuga za wanyama za Ruaha, Selous, Mikumi na Ruangwa pamoja na Kitulo. Serikali pia kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imekwenda ikakagua barabara kutoka Iringa mpaka kwenye lango la Hifadhi ya Ruaha. Kwa hiyo, tuko njiani kuboresha maeneo yale, lakini kikubwa ni kwamba kuboreshwa kwa ATCL kumesaidia sana na kutasaidia sana kupunguza gharama za ndege za kwenda kutembelea Hifadhi za Ruaha, Ruangwa na Kitulo na kwa hiyo, kufungua lango la Kusini mwa Tanzania. Hivyo hivyo, tumefanya kazi kubwa sana ya kupeleka zile Kampuni za Utalii za Kimataifa katika mbuga yetu ya Katavi, kwenye ufukwe wa Ziwa Tanganyika na katika Hifadhi yetu ya Gombe kule Kigoma, na kuanzia mwezi Aprili, 2017 tumeanza kupata watalii kutoka Uyahudi kwenye sekta hiyo ya Magharibi, na Air Tanzania imetusaidia sana kupokea wageni wanapofika Dar es Salaam na kuwarusha kwenda Kigoma na kutoka Kigoma kwenda Mpanda. Kwa hiyo, kazi inaendelea, naomba mtuunge mkono. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge nimesikia sana malalamiko makubwa kuhusu mkaa. Ndugu zangu, mkaa unasababisha ukataji wa asilimia 80 ya miti yote inayokatwa hapa Tanzania. Sisi tunaelewa kabisa kwamba bado tunahitaji wananchi wetu watumie mkaa katika vijiji, watumie kuni na katika miji midogo hii watumie mkaa kwa ajili ya maisha yao. Lakini huu mkaa unaokatwa unatengeneza tani milioni 2.3 za mkaa kila mwaka na zaidi ya nusu ya mkaa huu unaingia Dar es Salaam. Kiini macho tu. Maana kutoka Dar es Salaam mwingine unakwenda Zanzibar na kutoka Zanzibar unakwenda Oman na unakwenda Mombasa. Mkaa unakatwa kwenye hifadhi zetu za Magharibi za Burigi, kule Moyowosi, Kigosi, unakatwa unachomwa kule unakwenda nchi jirani za DRC, Burundi na mataifa ya kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ambacho ninataka niwaambie ndugu zangu ni kwamba hatuwezi kukubali miti yetu ikatwe kwa ajili ya kupeleka mkaa Kenya na majirani wengine. Tunataka mkaa ukikatwa utumike hapa Tanzania. Kwa hiyo, hatujakataza kuchoma na kuuza mkaa ndani ya Tanzania na mtu ambaye anafanya hivyo anavunja sheria na ninataka niseme, kuzungusha mkaa ndani ya mji au ndani ya vijiji au maeneo ambayo watu wanaishi kwa baiskeli au kwa pikipiki, hakuna mtu aliyekataza. Kinachokatazwa ni wale ambao wana-smuggle mkaa kutoka misituni kwa ajili ya kupeleka nchi za nje na kupeleka kuuza kwenye maeneo ambayo haina kibali cha kuuza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka kwanza tuanze vizuri, cha kwanza, nimeambiwa wapo watu wengi sana wamekamata baiskeli za watu, zipo baiskeli malundo na malundo. Nimeambiwa kuhusu malundo yaliyopo Kasulu, nimeambiwa kuhusu malundo yaliyopo Geita, nimeambiwa kuhusu malundo yaliyopo Ushirombo na maeneo mengine. Kuanzia leo, Maafisa wa Misitu wote wa maliasili wanaagizwa warudishe baiskeli za watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaagiza kwamba Maafisa Maliasili, Maafisa Misitu, Maafisa Wanyamapori walioshika pikipiki za watu, baiskeli za watu na vifaa vya wananchi ambavyo havina kesi mahakamani, waviachie mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo watu ambao wanasaidia sana nchi hii kwa kupanda miti katika maeneo yao na mashamba yao, na mimi nataka niwape pongezi kubwa kwa kufanya kazi hii kwa niaba ya Taifa. Watu hawa wengi wapo katika Wilaya za Njombe, Wanging’ombe, Mufindi, Mafinga, Kilombero na Morogoro. Nataka niseme hivi, Wizara na Serikali hatuna tatizo na watu hawa kuchagua matumizi ya miti yao.

Aidha, hatuna tatizo na watu hawa kukata miti yao wakati wanapotaka. Lakini tungependa kuwashauri, kwamba kama ni miti ambayo inatakiwa kutumika kwa ujenzi au kutengeneza vifaa kama hiki ambacho ninaongelea hapa, ni vizuri miti ili iachwe ikomae ili vifaa vile viweze kuwa vya kudumu na miti yao iweze kuwa na faida kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa sababu wapo watu wengi sana wanaofanya biashara ya magogo na mazao mengine ya miti, ni muhimu Maafisa Misitu waweze kuhakikisha kwamba hii inatoka kwenye mashamba yao na kwa sababu hiyo wasiwabugudhi, lakini wote ambao wanatoa kwenye mashamba ya Serikali, katika Misitu ya Serikali, Misitu ya Vijiji na Misitu ya Halmashauri ni lazima wapate vibali na leseni za kuvuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti viko vitu vingine hapa ambavyo vilisemwa kwa hisia kubwa sana nami najisikia kwamba labda nipate muda niviseme tu hata kwa sentensi mbili. Hapa kimesemwa Chuo cha Nyuki cha kule Tabora kwamba chuo kimefungwa, kama Kituo cha Utafiti kimehamishiwa Arusha. Sasa nataka kusema, hii siyo kweli. Chuo cha Tabora kipo na Chuo cha Utafiti wa Nyuki Tabora kipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo kile ni muhimu sana kwa sababu kulikuwa na uvumi wakati fulani kwamba asali inayotokana na miombo kule Tabora ina nicotine, kwa hiyo, haifai kuuza nchi za nje. Kituo kile ndiyo kimechukua sampuli za aina mbalimbali za asali kutoka maeneo yote ya Tabora; maeneo yanayolimwa tumbaku na yale ambayo hayalimwi tumbaku na hakuna tofauti ya kihesabu yaani statistical kati ya uwepo wa nicotine kwenye asali inayotoka ndani ya misitu ambapo hakuna kabisa tumbaku na ile ambayo inayotoka katika maeneo ambayo yako karibu na tumbaku. Nyuki wenyewe wana uwezo wa kuchagua na kutengeneza zao zuri. Kwa hiyo, nataka kile chuo kiendelee kukaa pale na tutashirikiana na Waheshimiwa Wabunge wa Tabora kuhakikisha kwamba tunakijenga na kukiendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliambiwa computer ziliondolewa, computer hazijaondolewa. Kama wameondoa watazirudisha, kesho ukifika pale utazikuta. Gari halijaondolewa limepelekwa kutengenezwa. Gari ni la mwaka 1989 na ni Land Rover ile ya zamami. Kwa hiyo, nimewaagiza kwamba wawaletee gari nyingine ili waweze kufanya utafiti vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limesemwa hapa likanigusa sana ni akina mama kuliwa na mamba wakati wanachota maji kwenye Mto Ruvuma. Hili limeletwa hapa na Mheshimiwa Bwanausi ambaye amelieleza kwa uchungu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuwahakikishia tu akina mama wa Lulindi kwamba tuko pamoja, tumetuma wataalam wa kupima maeneo ambayo yana maji ya chini ya visima ili kuhakikisha kwamba hakuna mwana mama anakwenda kuchota maji kule kwenye mto. Nasi tutatoa fedha ili visima hivyo viweze kujengwa na kuhakikisha kwamba akina mama hawaliwi na mamba wakienda kuchota maji. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo hapa ambayo bado nilikuwa nataka niyaseme, lakini kwa kweli muda tu ndiyo unanishika mkono na mimi nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba tutawapa majibu mazuri kwa maswali yenu yote ambayo mmeuliza na tutaomba msaada wenu katika kuendeleza sekta hii ya maliasili na utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo naomba ushirikiano wenu katika kupitisha bajeti ya Wizara ili tuweze kwenda kufanya kazi. Naomba kutoa hoja.