Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Zubeda Hassan Sakuru

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. ZUBEDA H. SAKURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha mchango wangu katika mjadala wa Maliasili na Utalii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Tunduru ni mojawapo ya Wilaya kongwe nchini ambazo zimekuwa na matukio ya muingiliano wa shughuli za binadamu na wanyamapori hasa tembo. Baadhi ya matukio yamepelekea kuwepo na mauaji ya tembo hao na kisha wananchi kuwaondoa pembe na kugawana nyama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni zaidi ya tembo 20 walivamia vijiji vya Wenje vilivyo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji wakitokea Msumbiji (Aprili, 2017) na wananchi waliwaua na kisha kuondoa meno yao na kugawana nyama. Vilevile wengine walivamia kijiji cha Jakika wakitokea Pori la Akiba la Selous na kuharibu zaidi ya ekari 50 za mazao mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika tukio hilo, zaidi ya watu watano walikamatwa. Pamoja na kuwa kuna muingiliano wa vijiji zaidi ya vitano na Pori la Selous na tembo hao wamekuwa wakisumbua zaidi, ipo haja kuweka mikakati madhubuti itakayoweza kuwadhibiti tembo kuingia katika vijiji hivyo na pia kuwashirikisha kwa karibu wananchi ili kupunguza mauaji ya tembo pale wanapoingilia maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu shehena ya meno ya tembo; Tanzania inaonekana mbele ya Jumuiya ya Kimataifa kama Taifa ambalo halitambui kwamba kushamiri kwa vitendo vya ujangili ni pamoja na kutaka kuuza shehena ya meno ya tembo. Ikumbukwe kuwa kadri siku zinavyoenda idadi ya tembo nchini inapungua huku ikichochewa pia na kutokuwa na mbinu na mikakati madhubuti ya kukomesha vitendo vya ujangili. Mkoa wa Ruvuma ni moja ya mikoa inayoongoza kwa matukio ya kukamatwa kwa shehena za meno ya tembo na nyara za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Serikali ya Tanzania bado imeshikwa na kigugumizi licha ya kuwa na idadi kubwa ya matukio 11,000 ya mauaji ya tembo kila mwaka, kutekeleza ahadi yake ya kuteketeza tani zipatazo 90 za shehena ya meno yaliyohifadhiwa katika maghala yake baada ya kuzikamata. CITES iliweka msimamo wa nchi zenye shehena kuteketeza shehena pamoja na kulifunga soko la China ili ku-discourage ujangili. Kwa masikitiko makubwa, Tanzania bado inashikilia kuuzwa shehena hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais Mstaafu, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete aliwahi kusema katika kongamano nchini Uingereza kuwa imesitisha na kufuta msimamo wake wa kuuza shehena ya meno ya tembo. Muda mrefu sasa umepita tangu ahadi hiyo itolewe. Je, Serikali inatueleza ni lini itateketeza shehena hiyo kama walivyofanya majirani zetu Kenya? Pamoja na hayo, ipo haja ya Serikali pia kupinga kwa vitendo uuzaji wa meno na pembe za ndovu waliokufa naturally ili kuua kabisa soko la ndovu duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa utangazaji wa vivutio vya utalii; Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vya utalii lakini havijatangazwa vya kutosha ili kuwavutia watalii wa ndani na nje ya nchi. Nimeona msanii wa kike Vanessa Mdee ni mmoja wa wasanii ambao wametumiwa na Afrika Kusini kutangaza vivutio vya nchi hiyo. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwatumia wasanii maarufu/mashuhuri na Watanzania kama mabalozi wa kutangaza vivutio vya utalii nchini? Pia ni lazima kuhakikisha Balozi zetu katika mataifa mbalimbali zinaandaa utaratibu wa economic diplomacy ili kuhuisha sekta ya utalii katika kukuza uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuongeza ajira kupitia sekta ya maliasili na utalii; vijana wengi hawana ajira nchini na hii imetokana na mwenendo wa dunia katika ajira lakini hii isisababishe Tanzania kupoteza lengo la kukuza ajira hasa kupitia sekta hii muhimu. Leo sekta ya utalii inakua lakini ajira zinazopatikana katika sekta hii ni chache sana. Hata vyuo vinavyotoa kozi za utalii nchini havikidhi hitaji kubwa la watu kwenye sekta ya utalii. Ipo haja ya kuwa na integration of national plans katika kutatua tatizo la ukosefu wa ajira nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa utunzaji wa mali kale katika kukuza utalii; ipo haja ya Serikali kuwekeza ipasavyo katika kutunza mali kale ili kukuza sekta ya utalii. Mji Mkongwe Zanzibar, Isimani, Bagamoyo na maeneo mengine ni mojawapo ya maeneo yenye malikale lakini havijatunzwa na ku-maintain status zake (hadhi zake) ili kuvutia watalii wengi zaidi kutokana na historia za maeneo hayo. Miji hiyo ni ya kihistoria, Wizara ishirikiane na Wizara ya Utamaduni ili kuhakikisha maeneo hayo yanatunzwa ili kuongeza Pato la Taifa kutokana na utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu biashara ya vinyago na utalii; ipo haja ya Wizara kuhakikisha kuwa wachongaji na wasanii wa vinyago hasa katika maeneo ya utalii wananufaika na kazi zao. Ni namna gani Wizara hii inahakikisha kuwa vinyago vinavyochongwa nchini vinanufaisha wachongaji wake na pia Serikali inanufaikaje na uuzaji wa vinyago hivyo? Iwapo Serikali itawekeza vya kutosha kuwasaidia wachongaji hawa itaweza kukusanya kodi na kuongeza ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.