Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri na watendaji wote wa Wizara hii kwa kuandaa hotuba hii na kuileta hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumelalamika sana hapa Bungeni juu ya mateso na maumivu yanayosababishwa na utendaji mbovu wa baadhi ya watendaji wako na hasa Game Rangers. Wilaya ya Kaliua na Jimbo la Kaliua imezungukwa na hifadhi, zaidi ya vijiji 30 vimesajiliwa kisheria, Serikali imepeleka huduma muhimu kama shule, zahanati na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Serikali imeunda Tume kuangalia namna ya kutatua tatizo sugu la migogoro ya ardhi na hifadhi, Askari wa Wanyamapori na Misitu wamewachomea nyumba, vyakula, mazao wananchi wa Kagome, Lumbe, Usinga, Luhembe - Iga na kuwaacha hawana chochote. Watu wa misitu kuweka beacon za mipaka kati ya wananchi na hifadhi kwenye maeneo hayo hadi kwenye nyumba za wananchi bila kuwashirikisha kwa lolote. Wanaingia, wanawapiga, wanawatupia vitu nje, wanaweka alama (beacon), wanakamata mifugo ya wananchi na kupiga mnada, wanakuja na wanunuzi wanawaacha wananchi maskini hana hata ndama wala mbuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanapora vitu vya wananchi na kwenda kuuza ikiwepo simu, solar panel, pikipiki, baiskeli, kuku, majembe ya kulimia kwa ng’ombe. Askari wa Wanyamapori wanakwenda kijiji cha Shela, kata ya Usenye, wanachukua mifugo katikati ya kijiji na kuwaswaga kupeleka hifadhini na kuwapiga faini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo cha wanyamapori kilichopo eneo la Kagome, Lumbe, kata ya Zugimlolo, askari (Games) walioko pale wote ni wezi, wanawafilisi wananchi. Mheshimiwa Waziri aeleze Bunge hawa Games wanapewa kazi ya kulinda wanyamapori au kupora mali za wananchi na kupiga minada mifugo ya wananchi, kuuza majembe, solar panel za wananchi, simu na kadhalika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vilivyosajiliwa ndani ya hifadhi vilipewa vyeti vya usajili wa vijiji vyao. Maafisa Wanyamapori walivichukua vyeti hivyo kutoka vijijini tangu mwaka 2014 na mpaka leo hawajavirudisha. Waziri aeleze vyeti hivyo viko wapi na lini vitarudishwa kwenye vijiji hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ieleze kwa nini inasuasua kurekebisha gharama za concession fee za hoteli zilizopo ndani ya hifadhi zetu ziendane na hali halisi ya sasa. Ni lini hasa fee hizo zitafanyiwa marekebisho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Sheria ya Uanzishwaji wa Hifadhi ya Ngorongoro imepitwa na wakati na inahitaji maboresho ili kuendana na hali ya sasa. Ni lini italetwa hapa Bungeni turekebishe? Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa inawahudumia wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi kwa chakula, elimu, afya na kadhalika, Serikali itaweza kufanya hilo jukumu kwa muda wote? Kwani watu wanaongezeka na huduma inaongezeka mwisho jukumu la hifadhi litapungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, misitu mingi ya asili imeteketea kwa sababu ya ukataji wa miti kwa kuchoma mkaa. Wanaokata mkaa hawapandi miti hata mmoja, pamoja na kuwa malundo ya magunia na mikaa imejaa barabarani na viongozi wanaona, hakuna juhudi za kuwaelimisha wapande miti na kuwaelimisha kuhusu mkaa endelevu. Ni mikakati gani ya Serikali inafanya kupunguza matumizi ya mkaa na kuokoa misitu yetu?