Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Bonnah Ladislaus Kamoli

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Segerea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami nitoe mchango wangu katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, Ofisi ya Rais (Sera, Bunge, Vijana, Kazi na Walemavu).
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu. Pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli; vile vile napongeza Baraza zima la Mawaziri kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya, lakini pia kuwapongeza kwa juhudi wanazotusaidia kwa kushirikiana na sisi Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati kabisa napenda kuwapongeza Mawaziri ambao wamekuwa wakija katika Jimbo langu la Segerea kutatua changamoto mbalimbali ambazo zinatukabili; Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Mheshimiwa Jafo na Waheshimiwa wengine ambao walifika kama Mheshimiwa Angelina Mabula. Nawapongeza sana, ahsanteni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/2017, zimezungumziwa program mbili. Program ya kwanza ni program ya kukuza ujuzi wa vijana na program ya pili ni kwa ajili ya kuwasaidia vijana ili kuweza kupata ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015/2016 iliandaliwa program na Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana ya wakati huo, ambayo ilitenga shilingi bilioni 4.1 ambayo iliweza kuwasaidia vijana waliohitimu mafunzo ya Chuo Kikuu au wahitimu wa juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hizo fedha zilizotolewa hazikuweza kukidhi au kuwasaidia vijana wote ambao waliweza kumaliza; kwa sababu tukiangalia takwimu ya vijana wetu wanaomaliza Chuo Kikuu na pesa inayotengwa, inakuwa ni ndogo sana.
Kwa hiyo, naomba Serikali pamoja na kwamba inatenga hizi fedha kwa ajili ya wahitimu wetu wa Vyuo Vikuu, naomba waangalie hili suala kwa kuangalia mifumo mingine ya taasisi za kifedha ambazo zinaweza zikashirikiana na taasisi za kijamii kuona ni jinsi gani wanaweza wakaungana nao ili kuhakikisha wanawasaidia vijana wetu ambao wanamaliza kwa wingi sana Vyuo Vikuu lakini pesa za kuwasaidia kupata ujuzi au ajira au kujiajiri wenyewe zinakuwa ni ndogo. Kwa hiyo, naomba suala hilo waliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sura ya nne, kipengele cha nne, ukurasa wa 48 - Kazi na Ajira. Katika Mpango wa Maendeleo 2016/2017, zimezungumziwa program mbili kama nilivyosema; program moja ya ajira ambayo imeweza kutolewa shilingi bilioni moja, lakini program nyingine ya kukuza ujuzi ni shilingi bilioni 15.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa hiki walichokifanya kwa ajili ya vijana wetu, kwa sababu tuna vijana wengi ambao wanahitaji kusaidiwa pamoja na kuandaliwa vizuri. Hizi fedha hazikidhi viwango vya vijana ambao wanamaliza Chuo Kikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuongelea suala la vijana wetu ambao wapo kwenye matabaka ya kati, ambao wamemaliza kidato cha nne au darasa la saba. Vijana wamekuwa wakijiajiri wenyewe. Sasa naomba Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi, iwaangalie hawa vijana kwa sababu wamekuwa wakijiajiri wenyewe, lakini pia mbali na kujiajiri wenyewe, kuna vijana wengine wana vipaji; lakini hawajawekwa kwenye huu mfumo wa kupata pesa kwa ajili ya kusaidiwa, kwa sababu huu mpango umeelezea kusaidia vijana tu ambao wamehitimu elimu ya juu. Sasa hawa vijana wa kati hatujawatengenezea mpango ni jinsi gani wanaweza wakasaidika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali ije na mpango maalum kwa ajili ya hawa vijana ambao wengine ni wasanii na wana vipaji. Kama Serikali ikiwatambua inawezekana ikawa ndiyo ajira yao ya kudumu. Pia pamoja na kuwa ajira ya kudumu, hao vijana wataweza kulipa kodi kwenye Serikali yetu. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi ambayo inaangalia watu wote kuanzia wenye elimu ya kati, lakini pia na wenye elimu ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, napenda kuzungumzia suala la bomoa bomoa katika Jimbo langu la Segerea. Kwanza nachukua nafasi hii kumshukuru Waziri ambaye aliweza kusimamisha hiyo bomoa bomoa isiendelee wakati walipokuwa wanabomoa, lakini kwa sasa hivi wananchi hawajui kinachoendelea. Tunajua kwamba kulikuwa kuna kesi sijui imetupiliwa mbali! Kwa hiyo, tunajua wananchi wengi wamejenga sehemu ambazo siyo salama, lakini wakati wanajenga, tuna Serikali ya Mtaa, pia tuna Serikali ya Kata. Hawa watu wamekuwa wakijenga, watu wanaangalia, kuna Watendaji wetu wapo kule wamekuwa wanawaruhusu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wenyewe, wanasiasa, tumekuwa tukifanya mikutano katika hayo maeneo, tukienda kwenye mikutano wanatuomba barabara, sisi tunakuja kwenye Manispaa zetu tunaomba barabara na wale watu wanapelekewa barabara. Pia wamepelekewa huduma nyingi za kijamii za kuwaonyesha kwamba sisi Serikali tunaunga mkono wenyewe waendelee kuishi pale. Sasa hivi tukisema kwamba tunawabomolea au tunawapa siku kadhaa ili waweze kutoka pale itakuwa hatujawatendea wananchi haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iangalie, ni kitu gani kitafanyika kuhusu bomoa bomoa? Watu wengi hawana elimu ya kujua kwamba mimi natakiwa nijenge mita 60 kutokea wapi? Kwa hiyo, Sheria ya Mazingira iliyokuja kwa sasa hivi, imekuja tu kuongea wananchi wengi ambao wanakaa sehemu ambazo mimi nipo, hawajui Sheria ya Mazingira. Sasa hivi ndiyo wameanza kuambiwa kwamba unatakiwa ujenge mita 60. Wananchi haelewi.
Kwa hiyo, naomba Serikali kabla hamjawabomolea inabidi kwanza mwende mkawape elimu. Pamoja na kuwapa elimu, hawa wananchi hawana kitu chochote. Kuna wengine walijengewa na watoto wao, watoto wao walishakufa, wamebaki wazee. Sasa hivi unavyokwenda unambomolea nyumba mwananchi kama yule, anakuwa hana sehemu ya kukimbilia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa mhusika aende akaangalie ni jinsi gani tunaweza tukawasaidia. Tuna Manispaa tatu Dar es Salaam, tuna viwanja ambavyo vipo waangaliwe wananchi watasaidiwaje kupata viwanja ili tutokane na hili tatizo la bomoa bomoa. Najua Serikali ya Chama cha Mapinduzi siku zote imekuwa mstari wa mbele kuwaangalia wananchi wake na hasa wananchi wa hali ya chini.
MWENYEKITI: Mheshimiwa, umemaliza muda wako, naomba ukae.
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.