Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi, napenda kumpongeza Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanayofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kusema hivi napenda kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri wanayofanya, wakati anapanga kununua ndege watu hatukuweza kuelewa alikuwa ana maana gani, lakini sasa baada ya ndege zile kuwa zimefika na zimeanza kazi tayari tumeshaona alikuwa ana maana gani. Tunamshukuru Rais hasa sisi watu wa Kigoma, ndege zile zimeongeza utalii katika Mkoa wetu wa Kigoma, kwa sababu usafiri upo mara kwa mara watalii wanaenda Kigoma, kwa hiyo watalii wanaongeza pato kwa kupitia ndege zile wanazozitumia zisingekuwepo tusingeweza kunufaika kupata watalii wanaoweza kutalii katika Hifadhi za Gombe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizugungumzie kuhusu matatizo ya mara kwa mara yanayohusiana na ongezeko la watu na ardhi kutokuongezeka. Asilimia kubwa ya Watanzania wengi ni wakulima na hasa akina mama sasa kutokana na jinsi watu wanavyoongezeka na ardhi ni ile ile kumekuwepo na matatizo mengi yanayotokea mara kwa mara. Serikali kwa kupitia watu wa TFS wanagombana na wananchi kwa sababu wananchi wanapokuwa wanaenda kulima kwenye maeneo wanafukuzwa wasilime kwenye maeneo yale kwa sababu mipaka haijaweza kuonyesha wananchi wanalima wapi na mipaka ya hifadhi ni ipi.

Kwa hiyo, nilikuwa ninamuomba Mheshimiwa Waziri kwa sababu hiki ni kilio cha muda mrefu, Mheshimiwa Waziri mimi ni Mbunge zaidi ya miaka kumi niko ndani ya Bunge hili na mara kwa mara tumekuwa tukitoa kilio chetu kuhusu Misitu ya Hifadhi kubaki haijawekewa mipaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa ninaomba kwa sababu Waziri wa Ardhi alisimama humu ndani akasema kwamba itaundwa tume na tume tayari iliishaundwa ikaanza kupitapita maeneo mbalimbali, kwanza nilitaka kujua je,majibu ya tume hiyo baada ya kuwa imezunguka maeneo mbalimbali yamefikia wapi? Kwa sababu majibu yakiishapatikana hayo sasa yatatoa majawabu ya kuweza kutenganisha ardhi ambayo wakulima watalima na ardhi ambayo itakuwa ni hifadhi kwa ajili ya Mapori Tengefu na Mapori Mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Kasulu, Kakonko na Kibondo wananchi wameendelea kupata taabu sana, kila wanapoenda kulima mashamba yao ambayo yamepakana na misitu ya Makele na Pori la Moyowosi wanapata shida sana wanafukuzwa, wanakimbizwa na hata katika maeneo mengine. Nilimsikia Mheshimiwa Sakaya akisemaa kule kwao Kaliua nyumba zimechomwa na hata wakati mwingine kule kwetu Kigoma nyumba zinachomwa, wanawake wanapata shida, watoto wanateseka, mazao yanachomwa, mavazi yanachomwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tulikuwa tunaomba Serikali iweze kutusaidia kufanya haraka na kutathmini maeneo hayo ili wananchi wapate maeneo ya kulima kwa sababu wananchi wanaongezeka, ardhi ni ile ile, lakini kwa sasa hivi wananchi wamekuwa na mwamko sana wa kuweza kutaka kulima na hata sisi Wabunge humu ndani. Wabunge walio wengi sasa hivi wameshika maeneo mengi wanataka kulima.

Kwa hiyo, tunaomba kabisa Serikali ifanye haraka iweze kupima maeneo hayo, iweze kuweka mipaka kusudi isogeze mipaka wananchi wapate maeneo ya kuweza kulima ili waweze kuinua kipato chao kwa kutumia maeneo ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumeshuhudia maeneo mengi wakulima na wafugaji wanapigana, wanauana, vifo vimekuwa vingi kwa sababu ya kugombania mipaka, tulikuwa tunaomba Serikali ifanye haraka kuweza kubaini maeneo ya wakulima na wafugaji; na itenganishe mapema kusudi matatizo haya yanayotokea mara kwa mara ya watu kuuwana, kupigana mapanga na mikuki yaweze kumalizika mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahamasisha wananchi waweze kujitegemea, watajitegemeaje kama hawana maeneo ya kulima; na ndio maana mimi eneo langu kubwa ntakalolisemea leo hii ni kilio kikubwa cha kuiomba Serikali, Wizara ya Ardhi na Wizara ya Maliasili waweze kukaa pamoja kumaliza zoezi lile ambalo tayari waliishalianza waweze kutoa majibu ili Serikali sasa iweze kubainisha maeneo haya ya wakulima yawe ni haya ya wafugaji yawe ni haya na maeneo tengefu ya Serikali na yale yanayopakana na vijiji yaweze kujulikana ili kuwaondolea usumbufu wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wetu wanateseka sana hasa wanapokwenda kulima mashambani huko. Wanaondolewa kwa kupigwa, wananyang’anywa baiskeli, mazao yakiiva wanashindwa jinsi ya kwenda kuvuna. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ninakuomba na ninakusihi sana, ninafahamu faida ya misitu lakini binadamu nao vilevile wanahitaji kunufaika kupitia misitu inayowazunguka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri tulioupokea ushauri wako uliosema kwamba tuwafundishe watu jinsi ya kufuga nyuki na kutengeneza mabwawa ya samaki. Lakini hawataishi kwa kuvua samaki tu, watahitaji kupata mahindi kwa ajili ya ugali, watahitaj kupata maharage na mboga nyingine zinazotokana na kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi ya kwangu leo yalikuwa ni hayo. Naiomba Serikali kwa mara nyingine tena, iwasaidie wananchi wa Wilaya ya Kasulu, wanaopakana na Kagera Nkandu.

MheshimiwaMwenyekiti, naunga mkono hoja.