Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Silafu Jumbe Maufi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii, awali ya yote ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia afya na nguvu na vilevile nawashukuru kina mama wa Mkoa wa Rukwa kuendelea kuniamini na mimi ninawaambia ya kwamba sitawaangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kutoa shukrani za dhati na pongezi nyingi kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara hii ni pana na ni Wizara ambayo inahitaji nguvu zaidi kuiongezea ili iweze kufanya kazi yake vizuri. Napenda kutoa pongezi za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Waziri Maghembe na Naibu wake ndugu Makani, wanafanya kazi ni nzuri na kazi ni nzito, na wamejitoa kwa kuweza kuisaidia Tanzania hii katika suala zima la maliasili na utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuwapaka matope ya namna moja au nyingine ni kutokana tu na baadhi ya watumishi ndani ya Wizara hii wamekuwa si waaminifu na si waadilifu, ndiyo wanaopelekea Waziri huyu na Naibu wake kupewa matope hayo. Lakini matope hayo hayawastahili hata kidogo kwa sababu ya kwamba wanafanya kazi yao vizuri katika wakati huu mgumu. (Makofi)

Napenda kutoa shukrani na pongezi kwa Rais wetu kutokana na jinsi anavyoweza kuimudu nafasi yake na kuisaidia Wizara yetu ya Maliasili kutuletea ndege ili utalii uweze kukomaa ndani ya Wizara yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala la mkaa. Mkaa sisi sote Wabunge humu ndani tumetumia mkaa na bado tunaendelea kutumia mkaa, wananchi wa Tanzania wengi wao takribani asilimia 96 wanatumia mkaa na hata hiyo miji na majiji ambayo wanaotumia umeme na gesi lakini bado wanatumia mkaa, mathalani Dar es Salaam wanatumia mkaa wa takribani asilimia 91 pamoja na kuwepo na umeme na gesi, kwa sababu umeme na gesi ni gharama na umeme na gesi hauna uzoefu kwa wananchi wetu wa Tanzania kwa sababu ndani ya miaka yao yote hii wametumia mkaa na kuni. Kwa hiyo, ninaomba tuzungumzie suala la mkaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikiwa kama Mjumbe wa Kamati ya Maliasili, Utalii na Ardhi, nimetembelea Morogoro Wilaya ya Mvomero, Wilaya ya Kilosa na Morogoro Vijijini, upo mradi ambao unaendeshwa pale, mradi ambao unaitwa Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS). Huu mradi ni mradi mzuri ambao tunasaidiana na wenzetu wa Uswis nimeuona utakuwa ni jibu sahihi la kutunza misitu yetu na suala lile la Wizara ama suala lile la Serikali kuzuia kuchomwa mkaa halitaweza kuwepo tena, bali watu wataendelea kuwa na mkaa na kuutumia mkaa. Watautumiaje, hawa ndugu zetu wanaleta mkaa endelevu, ni kwamba wanaelezwa namna ya kukata miche ya mkaa ndani ya misitu wakiacha miche ambayo ina viota vya ndege, miche inayotumika kurina asali, na miche ya mbao. Wanaitenga, wanachukua miti inayostahili kukatwa na kutengenezwa mkaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wameoneshwa namna ya kuchoma, uko namna kuchoma, namna ya chupa na namna ya box kwa kweli utaalam huu unapelekea hawa wachomaji wa mkaa wanapata mkaa mwingi wa kutosha, takribani gunia 50 mpaka gunia 60, na hii sehemu ambayo wanakata baada ya miaka mitatu wanaacha sehemu ile na sehemu ile inakuwa inapata maoteo, na yale maoteo yanarudisha msitu mapema zaidi kulikoni ule utaratibu tunaosema wa kukata mti, panda mti. Kwa sababu tunapanda miti kwa sababu uoto wake na ukomavu wake haupo, unakuwa ni asilimia ni ndogo sana, lakini hii ya maotea inaonekana kana kwamba ule msitu unarudi kama ulivyokuwa zamani na hatimaye unaweza kuwasaidia wanachi kuendeleza mkaa endelevu katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini ushauri wangu kwa Serikali, ninaomba mradi huu kwa sababu unachukua muda mrefu, ni vyema Serikali ikaongeza mkono katika mradi huu ili mradi huu ukatawanishwe katika kanda zetu za nchi yetu. Tuna kanda nane za nchi yetu, kwa hiyo katika kanda zile nane wakapeleka utaalum huu wa mkaa endelevu. Ili huu mkaa kwa kweli ni rafiki mzuri sana wa utunzaji wa misitu yetu na mazingira yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naliomba kabisa kwamba hata mapato ya Serikali yatapatikana kwa sababu yanakuwa na hesabu kwa sababu tanuru moja ni gunia 50; kwa hiyo, watajua Wilaya inapataje, Taifa linapataje, kwa bei ambayo inakubalika. Lakini tukiacha uholela ndio maana tunapelekea kwamba, Wizara yetu inasitisha, lakini inasitisha kwa sababu ya nini, wananchi hawa wanatumia mkaa na mkaa unatumiwa sana na akina mama na hata hii biashara ya mkaa ni kina mama, tunasema kina mama tunawatua ndoo, sasa tukiziba ziba hii mikaa bila kutumia utaratibu huu ni dhahiri kusema kwamba Serikali inaleta mzigo mwingine kwa akina Mama, wa mama watabeba ndoo ya maji, na watabeba tena na mzigo wa kuni ambao kwamba sio sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tanaomba tuwasaidie kina mama kwa kuongeza nguvu katika mradi huu, ili mradi huu uwe ni endelevu na tupate mkaa endelevu kwa wananchi wa Tanzania, kwa sababu mbadala wa mkaa katika nchi hii bado haujapatikana. Kwa hiyo, ninawaomba ndugu zangu tukubaliane na wewe Waziri Maghembe najua ni makini na msikivu, ninaomba huu mradi uje utoe semina kwa Wabunge wote hapa Bungeni, kabla ya Bunge halijaisha ili tukitoka wote na uelewa tutakwenda kutoa maelekezo kwa watu wetu kule na hatimaye na wao watafuata huu mkaa endelevu na sisi tutaweza kuokoa misitu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hiyo kupanda miti itakuja kwa hiyo milima ambayo tuliyoiacha sasa hivi imeshakuwa ni kipara, lakini kwa sasa hivi kwa ile misitu tuliyokuwa nayo ni lazima tuweze kuweka utaratibu huo. Lingine ndio kusema ya kwamba mkaa ujitegemee katika maeneo yao, hao watu wa mjini Dar es Salaam watapata mkaa kutoka wapi, wakati mkaa wa Dar es Salaam unatoka Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tuweke utaratibu amabo unaweza kujibu hoja kwamba miti yote haina misitu kwa hiyo hawatakuwa na mkaa, lakini katika miji yote takribani asilimia 91 watu wa mijini wanatumia mkaa. Kwa hiyo nawaomba kwamba utaratibu uwepo, mkaa uingie mijini na iwezekane kuhakikisha kwamba akinamama hawa wanatokana na adha hiyo. Tunavyozuia tunapelekea bei ya mkaa kupanda, sasa hivi Dar es Salaam ni 73...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.