Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Allan Joseph Kiula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuweza kunipatia nafasi nami nichangie hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa nachukue nafasi hii kumpongeza Waziri Mkuu kwa hotuba yake. Hotuba hii imekaa vizuri kwa sababu imegusa maeneo yote ya utendaji kazi na maeneo yote ambayo ni matarajio ya nchi. Pia nampongeza Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa utendaji kazi wake mzuri. Wanasema unakunywa chai ya moto na andazi moto. Maana yake nini? Maana yake unatoa ahadi, unaanza kutekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, elimu bila malipo imeanza kutekelezwa, changamoto zipo, inabidi sisi sasa tuziboreshe. Hotuba hii imejengwa katika msingi mzima wa Mipango ya Miaka Mitano. Kwa maana hiyo, imezingatia na ni hotuba ambayo ina tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo habari ya mapato. Ili kuweza kufanikisha utekelezaji wa mipango mbalimbali ambayo tunapanga ndani ya Bunge hili, ni lazima suala la mapato liangaliwe kwa kina. Ninapozungumzia mapato, maana yake ni nini? Maana yake ni lazima tupanue wigo wa mapato, tutafute vyanzo vipya vya mapato, tuachane na ule utamaduni wa kupandisha gharama kodi kwenye sigara, pombe lakini pia na kodi ya wafanyakazi. Lazima tupanue wigo wa mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kuna sekta isiyo rasmi. Sekta isiyo rasmi ni kubwa lazima tuirasimishe. Tukiirasimisha, wigo utapanuliwa, lakini pia wawekezaji wanaokuja kuwekeza ndani ya nchi yetu, inatakiwa tuziangalie kodi wanazostahiki kulipa. Kodi hizo zikiwekwa vizuri, tutapata mapato. Pia liko jambo ambalo na lenyewe sisi kama Wabunge inabidi tuliangalie. Yako mambo kwa sababu Sheria za Ukusanyaji wa Mapato zinatungwa na Bunge hili lakini imeshafikia mahali sisi Wabunge ndiyo tunazihoji. Sasa tunapozihoji, inakuwa ni changamoto kubwa.
Kwa hiyo, naomba Waziri anayehusika aje atuelimishe upya, hizi sheria zinazopitishwa hapa na zinazotumika. Kwa mfano, Sheria ya Uondoaji wa Mizigo Bandarini kwenda nje ya nchi, hizi transit goods; uamuzi ulifikiwa wa taratibu za kuondoa na ulipaji kodi, lakini wako watu ambao wanahoji na zilipita humu humu ndani. Sasa ni muhimu jambo hilo na sisi tukalielewa kwa sababu sisi kama Wabunge tunatakiwa tuwe Walimu na ndio tuwaelekeze watu wetu. Kwa sababu mtu wa kijijini hawezi kujua hayo mambo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa eneo hilo limeanza kuendeshwa na Clearing and Forwading, hao Mawakala wa Forodha. Haiwezekani! Kama sisi ni Wawakilishi wa wananchi lazima tulisimamie, kama sisi ni Wabunge, lazima tulisimamie na tuisaidie Serikali katika kutoa mwongozo na kuwaambia watu jambo lipi linatakiwa kufanyika. (Makofi)
Cha pili, nizungumzie ajira. Nitajikita zaidi kwenye maeneo ya vijijini. Zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wetu ni wakulima. Sasa tunapozungumza ajira na kilimo, ina maana kilimo kinatoa ajira kubwa kwa watu wetu wa vijijini na kwa wananchi wetu wa vijijini. Jambo la muhimu ni nini? Wananchi wetu wanatakiwa wapate mbegu bora kwa bei rahisi, wapate pembejeo kwa bei rahisi. Mambo hayo yakifanyika, tunaweza kuchangia kupanua wigo wa ajira badala ya kutegemea hizi wanaita white colour job au Ajira za kuajiriwa maofisini. Kilimo ni sekta kubwa ambayo inaweza ikatoa ajira. Ukiangalia ukurasa wa 28 suala hilo limezungumziwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 32 kuna suala la viwanda na kilimo. Ukienda kwa mfano Wilaya ya Mkalama, tunalima sana alizeti, vitunguu, mahindi na mazao mengine. Sasa lazima kuwe na muunganiko kati ya hii malighafi ambayo itakwenda viwandani. Kwa hiyo, kitu cha msingi zaidi ni kusisitiza suala la kilimo ambacho kitatoa malighafi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kilimo, kuna suala la masoko. Wananchi wetu lazima tuwatafutie masoko. Tunawatafutia masoko vipi? Kwa kutengeneza masoko ya kukukusanyia mazao, kwa sababu mwananchi ananyonywa sasa hivi. Kwa mfano, kule Mkalama, kuna mtu anatembea na debe linaitwa Msumbiji; debe nane kwa debe sita. Sasa mkulima anapunjwa. Kwa hiyo, tukiwa na sehemu za kukusanyia mazao, kwa Mfano Kibaigwa kuna soko la Kimataifa na sehemu kama Iguguno kunaweza kukawa na soko la Kimataifa la kuuza mazao tukawasaidi wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la ardhi. Maeneo mengi yamekuwa na migogoro ya ardhi ikiwemo Mkalama. Ipo migogoro mingi ya ardhi. Pia hao watu wanaokuja kupewa ardhi kubwa kubwa; kuna mtu anapewa ekari 700 na anapewa ndani ya kijiji, maana zinapimwa mpaka zinaingia ndani ya kijiji. Sasa hao wataalam wetu wanaona jambo hilo? Hilo ni jambo ambalo inabidi likemewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wilaya zinaanzishwa, hakuna Afisa Ardhi Mteule. Nalo ni changamoto kubwa. Kwa hiyo, naomba Ofisi hii iangalie, kuwe na Maafisa Ardhi Wateule. Wilaya inapoanzishwa, ateluliwe Afisa Ardhi Mteule na Hakimu wa Wilaya ili mambo yaweze kusonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la barabara. Hapa ndiyo ipo changamoto kubwa. Maana tunapozungumza suala la barabara, mimi huwa naangalia, wenzetu wa Dar es Salaam barabara zote ni lami, lakini ukienda Mkalama na maeneo mengine ya pembezoni barabara zote ni vumbi; na uwezo wa Halmashauri zetu wa kukusanya mapato ni mdogo sana. Kupandisha hadhi barabara ya Halmashauri yenyewe ni changamoto, acha kupandisha iwe barabara ya TANROAD.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala hilo linatakiwa liangaliwe kwa makini. Zipo barabara kwa mfano kutoka Mwangeza mpaka Endasiku, zipo barabara za kwenda Iramoto, zile hazipo kabisa kule ni mapalio tu, lakini maeneo hayo ndiyo yanayozalisha mazao kwa wingi kama alizeti na mahindi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nachukua nafasi hii kwa kuipongeza Serikali kwa kutoa pesa daraja la Sibiti kuanza kujengwa. Hapo ndipo sera ya kuunganisha Mkoa kwa Mkoa wa Singida na Simiyu, tutapata unafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona wamesema maji vijijini yamesambazwa kwa asilimia 72, lakini nikiangalia vijiji vyangu vyote havina maji, halafu asilimia 72 imetokea vipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Waziri mhusika anatakiwa angalie jambo hili, iko miradi ambayo imefadhiliwa na Benki ya Dunia, haijamaliza; lakini inahesabika kwamba mradi upo na unafanya kazi. Wahandisi ni wa aina gani? Bomba za maji zinapita mtoni. Mto unakuja unazoa maji pale Iguguno, unasema mradi wa World Bank. Mradi wa World Bank lazima uwe na hadhi ya World Bank, siyo unakuwa mradi kama wa kimachinga tena. Kwa hiyo, Waziri wa Maji anatakiwa aangalie matumizi ya pesa na watu wapate maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya mpya zina changamoto kubwa; Hospitali za Wilaya hazipo! Kama hazipo, Halmashauri ikijitahidi hata ikiweka kwenye mpango haiwezi, kwa sababu kipato ni kidogo. Wilaya hizi ziangaliwe kwa jicho la karibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ulinzi na usalama. Jeshi la Polisi na wengine lazima waangaliwe kwa karibu. Sisi tunaokaa porini kule, amezungumza Mheshimiwa Musukuma huko, watu wanakatwa mapanga tu! Kwetu, vijana wa bodaboda wanatekwa tu! Suala la ulinzi lazima liangaliwe, magari na mafuta yapelekwe ili tuweze kupiga hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Wilaya mpya na wenyewe ni changamoto. Kwa mfano, Wilaya ya Mkalama, mwaka 2014 ilitengewa shilingi bilioni moja ikapewa Shilingi milioni 450; mwaka huu ilitengewa shilingi bilioni moja, haijapelekwa hata senti tano! Hiyo Wilaya mpya itakwisha lini? Hiyo na yenyewe ni changamoto kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya machache, niipongeze tena hotuba ya Waziri Mkuu, naunga hoja mkono, tushikamane. Watu walikuwa wanataka maamuzi magumu, haya ndiyo maamuzi magumu. Ukiangalia maeneo yote yaliyotumbuliwa, yameguswa maeneo ambayo hayajawahi kuguswa. Sasa maeneo hayo yaliyoguswa, wameguswa ndugu zetu, kaka zetu; tuvumilie! Tunataka kujenga Tanzania mpya. Utajengaje Tanzania mpya kama huchukui hatua? Nashukuru sana, naunga mkono hoja.