Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nami niwe mmoja kati ya watu ambao wanapongeza maandalizi mazuri ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na Watendaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amekuwa hodari kusikiliza matatizo ya wananchi hasa tunapomwendea sisi Wabunge ni muungwana. Nina hoja zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, Wilayani kwetu tuna mbuga inaitwa Rwamfi Game Reserve, mbuga hii imepakana na vijiji kadhaa na kabla ya mbuga hii haijakuwa Serikalini ilikuwa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi. Kutokana na umuhimu wa uhifadhi tunaoujua tuliamua kuipeleka Serikalini, Serikali ikaitwaa ikaanza kuihudumia. Katika kipindi ambacho Serikali inahudumia tumeziona faida kwamba kwa kweli wanyama wameongezeka na mbuga inatunzika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo changamoto ambazo tunaziona kwa wahifadhi wenyewe, kwamba hawana vitendea kazi vya kutosha, hawana idadi ya watumishi wa kutosha na kwa maana hiyo tunaiomba Serikali iwaletee gari, maana yake naliona pale gari bovu sana la muda mrefu, kwa hiyo haliwapi nafasi ya kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia pamekuwa na migogoro baina ya mipaka na vijiji vinavyopakana. Kuna vijiji vya Kasapa, vijiji vya King’ombe, vijiji vya Mlambo, vijiji vya Ng’undwe, vijiji vya Mlalambo, Kizumbi, Kata, Namansi na vinginevyo. Vijiji hivi vimekuweko kabla hata ya kuanza kwa pori lenyewe, vijiji vya kiasili, lakini kwa sasa vinaonekana kwamba viko ndani ya pori na kwa hiyo kuna mgogoro tayari kwamba wahame nao, kwa hivyo hawana nafasi, hawana maeneo ya kulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo Kamati ya Kitaifa ambayo imeshaundwa inatembea kila mahali, kwetu haijafika naomba wafike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni nilifika hata Ofisini kwa Waziri nilimwelezea juu ya mgogoro wa Kijiji cha Kasapa ambao ulipelekea wananchi kufyekewa mazao yao kwa kiwango kikubwa, zaidi ya hekta 20, kitu ambacho kwa mwaka huu ni shida kubwa sana hakuna chakula, ingawaje Waziri alinipa ushirikiano mkubwa na kuwaambia wahifadhi kwamba ni vizuri wawe wanawasiliana kuliko kuchukua hatua kali za namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, Mheshimiwa Waziri ameshaniahidi kwamba baada ya Bunge tutaenda huko ili kwenda kuiona hii changamoto. Namshukuru sana, bila shaka ataiangalia kwa makini na kuona jinsi inavyoweza kusuluhishwa kwa vijiji vyote ni changamoto kubwa kwetu. Namna nzuri ya kuikabili changamoto ni kuangalia kama yapo maeneo ambayo yanaweza yakaachwa kwa wananchi kwa ajili ya kuendeleza shughuli za maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ambayo naiona katika Rwamfi ni mpaka wake na Kalambo ranch. Kalambo ranchi ni ranchi ya Taifa na kuna blocks ambazo wamepewa wawekezaji, wawekezaji hawa katika eneo hilo hakuna mipaka inayoonekana wazi, kwa hiyo pemekuwa na migogoro ya hapa na pale, jambo ambalo linafanya wawekezaji hawa wa-face migogoro mingi na wahifadhi. Kwa hiyo, jambo zuri hapa ni kuweka mipaka iwe wazi ili wananchi hawa ambao wanalipa kodi ya Serikali wasibughudhiwe pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni vivutio vya utalii. Wilayani kwetu hasa Jimbo la Nkasi Kusini kuna vivutio vya utalii vingi. Ukiwa kwenye mwambao mwa Ziwa Tanganyika kuna ukanda mzuri sana, kuna mawe mazuri ambayo yamepangika kwa namna yake na kuna visiwa vizuri ambavyo vikiendelezwa vinaweza vikawa ni utalii wa namna yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, naishauri Wizara itembelee maeneo hayo ione utajiri uliopo ya utalii waone utajiri uliopo wa utalii ambao ukiendelezwa unaweza ukachangia sana. Siyo tu kwetu kwa Mkoa mzima kuna maeneo kama vile ukienda Kasanga kuna Ngome ya Bismark, ikiendelezwa ile inaweza kuwa nzuri sana, kuna Kalambo falls ambayo sasa hivi nimeona kama Wizara inaizingatia, ikiiendeleza inaweza ikaleta pesa nyingi ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kama unaenda Kala kuna eneo ambalo ilikuwa ni makazi ya Zwangendaba ambaye alikuwa maarufu sana katika historia ya Tanzania kutoka Kusini. Aliuawa maeneo hayo na kuna majengo ya Mjerumani pale ambaye ndiye alimdhibiti kwenye eneo hilo na alizikwa eneo hilo. Kwa hiyo, inaweza ikasaidia sana kwa watu wanaotaka kujua mambo ya kihistoria katika suala zima la utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni muhimu sana katika maeneo ya utalii kwetu ni eneo la Kijiji karibu na Mji wa Namanyere. Kuna maji moto ambayo yanatoka kiasi kwamba yakiendelezwa pale kijijini inaweza ikasaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi niishauri Serikali, katika kuendeleza utalii nchini waangalie miji ambayo inawekeza katika ujenzi hasa ambayo ni ya kimkakati katika suala zima la utalii kama Mikoa ya Rukwa, Katavi na maeneo mengine. Majengo yanayojengwa pawepo na ushauri wa kitaalam wa kuangalia Halmashauri ambazo zinasimamia ujenzi ili angalau viwango viwe vinafikia ili changamoto ya mahali pa kufikia wageni ambao wanajielekeza kwenye utaliii isiwe ni changamoto inayokinzana na suala zima la utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba bado suala la mkaa kama wenzangu walivyolisema liangaliwe upya. Sasa hivi bado hatujawa na nishati mbadala ambayo inaweza ikakidhi mahitaji ya watu kwa sasa. Kwa hiyo, pamoja na uhifadhi na umuhimu wake, lakini pawepo na ustaarabu wa kuangalia jambo hili kwa umakini zaidi, vinginevyo tunaweza tukazua migogoro ambayo italeta shida kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante.