Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Nabu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia hotuba hii ambayo ni muhimu sana kwa sisi akina mama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais pamoja na Mawaziri wake ambao wako katika Wizara hii. Vilevile nimpongeze na kumshukuru sana Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mama Samia ambaye alikuja Iringa kwa ajili ya kukagua vyanzo vya maji. Niiombe tu Serikali iangalie yale maagizo aliyoyatoa siku zile alivyokuwa Iringa basi yazingatiwe. Tuna imani kwamba kama yatazingatiwa angalau Iringa na sisi vile vyanzo vinaweza vikawasaidia wanawake wa Iringa na wananchi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niunge mkono Wabunge wote waliochangia kuhusu Mfuko ule wa Maji uongezewe kutoka kwenye shilingi 50 mpaka shilingi 100. Nina imani kabisa ili mwanamke atuliwe ndoo kichwani ni muhimu mfuko huu ukaongezewa kiasi hicho. Pia tuangalie kwenye vyanzo vingine vya mapato kama wenzetu wengine walivyosema ili tu Mfuko wa Maji upate fedha. Kama walivyosema wenzangu na mimi nawaunga mkono kwamba maji ni kitu muhimu sana katika maisha ya binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu katika Mkoa wetu wa Iringa tumekuwa na matatizo makubwa sana, tumekuwa na vifo vingi sana vinavyosababishwa na ukosefu wa maji. Nitatoa mifano miwili ambayo imetugusa sana wananchi wa Iringa. Kwanza, kuna mwanamke ambaye alikuwa amejifungua watoto mapacha akaenda kwenye Mto Lukosi kwenda kuchota maji yule mama akauawa na mamba. Hili ni jambo ambalo kwa kweli linatuumiza, aliacha watoto wadogo sana.

La pili, juzi tu hata mwezi haujaisha, kuna mtoto wa shule ya sekondari ya Lukosi alikwenda pale kuchota maji akatokea mbakaji mmoja akamchukua yule mtoto kutaka akambakie upande wa pili. Watu walipotokeza akamtupa kwenye maji yule mtoto akafa. Kwa kweli ilitusikitisha sana kwa sababu yule binti alikuwa bado mdogo. Kwa hiyo, tunaomba sana Mkoa wa Iringa unauhitaji mkubwa sana wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika vituo vya afya vingi vilivyopo vijijini bado maji ni tatizo, inasababisha akina mama wakati wanajifungua wanapata mateso makubwa sana. Aidha, mama anaamka asubuhi kwenda kwenye shughuli ya kutafuta maji badala ya kwenda kwenye shughuli ya maendeleo. Hii pia inamkosesha mama kuendelea na miradi aliyonayo, kutwa nzima anatafuta maji, anamuacha pia hata mzee, hata ndoa nyumbani zinavunjika kwetu Iringa kwa sababu ya maji kwa sababu mama anaondoka saa
9.00 za usiku kwenda kutafuta maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nisisahau kuwazungumzia wananchi wa Mji Mdogo wa Ilula. Bahati nzuri Mheshimiwa Rais alipokuja kuomba kura alikuja kwenye Wilaya ya Kilolo, lakini kwenye Mji Mdogo wa Ilula. Ule mji kama alivyosema Mheshimiwa Mgonokulima kwa kweli maji ni tatizo kubwa sana. Siku ile wananchi walikuwa wana mabango ynayozungumzia tatizo la maji wakimwambia Rais wanavyopata shida ya maji. Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba angeweza kuleta maji baada tu ya kuchaguliwa na akatuambia kwamba Waziri atakayemchangua atakuja mara moja kuja kusikiliza tatizo la maji. Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri hebu aende Kilolo pale Ilula ukawaeleze kwa nini mpaka leo maji hayajaletwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mkoa wa Iringa hauna tatizo la maji bali ni usambazaji wa maji. Tunavyo vyanzo vingi sana vya mito kama Mto Ruaha, Mto Lukosi, Mto Mtitu na kadhalika, ni kwa nini Serikali isitumie mito hiyo kutatua tatizo hili la maji kwa sababu tumeona miradi mingi sana ya visima haifanyi kazi. Nilishauliza hata swali, tunayo mito mingi kama Mto Lukosi umezunguka maeneo mengi sana, lakini mpaka leo hii haujaweza kutumika ili uweze kuwasaidia wananchi wa Iringa kutatua tatizo la maji linalowakabili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba tu nipate majibu, katika mji huo huo wa Ilula, kulikuwa kuna wafadhili wa Austria. Je, ule mradi umefikia wapi kwa sababu tulijua kwamba ungeweza kuwasaidia wananchi wa pale Ilula?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja lakini nitaandika kwa maandishi kwa sababu mengi sana sijayazungumza. Nashukuru sana kwa kupata nafasi hii.