Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Capt. (Mst). George Huruma Mkuchika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. KEPT. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nikushukuru kwa kunipa nafasi hii kuweza kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Napenda kuchukua nafasi hii kwanza kumpongeza Rais wetu John Pombe Magufuli anavyoiendesha nchi hii. Wapo ndugu zetu walikuwa wanapiga kelele za ufisadi, ufisadi, amewafungulia Mahakama ya Ufisadi. Wale waliokuwa wanasema kwamba huyu fulani fisadi wamewachukua, tuleteeni kwenye Mahakama ya Ufisadi tuwashughulikie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua nafasi hii kuunga mkono hoja ya Wizara ya Maji. Nataka niwakumbushe Wabunge wenzangu Kanuni zetu zinasema Kamati Ndogo ya Bunge ya Kudumu inapofanya kazi ni sawasawa na Spika amekaa anaendesha Bunge. Bajeti tuliyoletewa hapa imefanyiwa kazi na wenzetu wa Kamati inayohusika na suala la maji. Kwa hiyo, unapokuja hapa tu ghafla bin vuu ukasema tufumue, turudishe, tufanyeje, mbona mnawadharau Wajumbe wenzetu wa Kamati waliofanya kazi hii?

Mimi naungana na wenzangu wanaosema tutafute namna ya kuboresha Mfuko wa Maji, yale mawazo yanakaribishwa, lakini wewe unasema tufumue, tuikatae, darasa hilo sisi wanafunzi tunalikataa, darasa la kukataa bajeti sisi tunalikataa, bajeti hii itapita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nataka nianze kwa kuwapongeza wapigakura wangu wa Jimbo la Newala. Kule kwetu Newala tuna ustaarabu wa kuvuna maji ya mvua, kila nyumba ya bati utakayoona ina kisima kimechimbwa na kwa sababu kule kwetu water table iko very low tunachimba mpaka futi 14, tunajenga kwa zege, tunajenga kwa tofali, tunakinga maji ya mvua ya kutosha familiaile mwaka mzima. Ndiyo maana hali ya maji Newala unafuu upo kidogo, si kwa sababu ya maji ya bomba ya Serikali, hapana, tunakinga maji ya mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tusingekinga maji ya mvua hali yetu ingekuwa mbaya sana. Nataka nitoe mfano na hili mimi nataka niiseme Serikali yangu, mnapofanya vizuri nawapongeza, mnapoharibu nawasema. Hivi mradi wa maji wa Makonde kwa muda wa miezi miwili mmewakatia umeme, watu wa Newala tupate wapi maji ya bomba ya kunywa?

Nimeambiwa umeme juzi umerudi, naomba jambo hili lisirudiwe tena. Mheshimiwa Rais aliposema kata umeme amewahimiza Maafisa wa Serikali mnaotakiwa kulipa maana yake mlipe kwa wakati siyo mnazembea kulipa halafu wanakwenda kuadhibiwa wananchi ambao kila mwezi mkiwapelekea ankara wanalipa. (Makofi)

MHE. KEPT. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa pili ule hata ukawaelimishe namna gani, huyo anayeongea…
Mheshimiwa Naibu Spika, huyo anayeongea alituhamasisha humu tuikatae bajeti, mimi sikukubaliana naye lakini nilikaa kimya, ndiyo ustaarabu wa humu ndani. Ndiyo maana tunawaambia nchi hii CCM itatawala ninyi mtabaki tu kama mnyama fulani anaona mkono wa binadamu unatembea anasema unadondoka kesho, unadondoka kesho, ndiyo mlivyo, tunakamata Serikali kesho, kesho, kama mwendo wenu ni huo hampati kushika nchi hii. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nataka wale ambao hamuifahamu Newala, Waziri anaifahamu, Naibu Waziri anaifahamu, sisi tunaishi mahali kunaitwa Makonde Plateau. Wale wanaokumbuka geography Makonde Plateau definition yake wanasema a raised flat piece of land (kipande cha ardhi kilichonyanyuka), ukiwa kwenye plateau maana yake umekaa kwenye meza, ndivyo ilivyo Newala na Tandahimba. Tuko juu kwa hiyo water table iko chini sana, hakuna mahali tunapoweza kuchimba tukapata maji na ndiyo maana tunategemea sana maji ya bomba na ndiyo maana kwenye miaka ya 1950 watu wa Newala wenyewe tukaanzisha Kampuni inaitwa Makonde Water Corporation, tukakopa hela Uingereza tukaanzisha mradi wa maji Makonde, tukawa tunauza maji, tunatengeneza pesa, watu wanapata maji ya kunywa. Serikali baada ya uhuru ikatuhurumia, ikauchukua ule mradi ikaufanya mradi wa maji wa kitaifa. Nakuomba ndugu yangu Wenje, aah nakuombandugu yangu Lwenge… (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu Wabunge ni yale yale ya kutokujua, mimi nilidhani upande wa pili wanaelewa kwamba ulimi hauna mfupa kumbe hawajui. Mimi nimewasamehe maana tumefundishwa, baba uwasamehe maana hawajui watendalo, mimi nimewasamehe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kampuni ile ya Makondeko ilichukuliwa na Serikali, ukafanywa ndiyo mradi mkubwa wa kitaifa. Mheshimiwa Naibu Waziri, mradi wetu ule wa kitaifa unasuasua kwa sababu upatikanaji wa maji siyo mzuri, miundombinu imechakaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu upande wa Wizara yale mambo ambayo nilitaka kuyamalizia nitawaandikia, mimi naunga mkono hoja.