Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Edwin Mgante Sannda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwanza kabisa naipongeza Wizara kwa kazi nzuri ambayo imeendelea kufanya chini ya Waziri wetu na timu yake yote. Kabla sijachangia yale ambayo ningependa kusema, ningependa nitoe maoni yangu ya ujumla kuhusiana na bajeti ya Wizara hii ambayo imewasilishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, sijui niombe ombi la tofauti kidogo? Tumwombe Chief Whip wetu anipatie dakika 15 kwa sababu, ninayo mengi hapa, ikiwezekana hiyo tukatengua Kanuni, itakuwa nzuri zaidi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza maoni yangu ya jumla, pamoja na mawazo ya wengi ambayo yamekuwepo kuhusiana na kuongeza bajeti hii, mimi nimejaribu kuitafakari. Mwaka 2015/2016, tulikuwa na karibu shilingi bilioni 130 halafu mwaka 2016/2017 tukaruka sana mpaka shilingi bilioni 900 mwaka huu 2017/2018 tumekwenda chini kidogo mpaka shilingi bilioni 600. Wengi wamedhani kwamba ni vizuri tungeweza kuongeza bajeti ifikie angalau lengo la mwaka jana. Mimi nafikiri tulipofanya maoteo ya shilingi bilioni 900 labda hatukuwa sahihi sana ndiyo maana hawa wenzetu wakarudi nyuma wakawa realistic zaidi na kurudi kwenye shilingi bilioni 600. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wenyewe Wabunge, tumekuwa tukisimama hapa kila siku tunasema bajeti za Serikali zije za uhalisia, leo wamerudi nyuma wamekuwa halisia, tunawaambia warudi kule. Nataka niwaambie, katika shilingi bilioni 900 plus, utekelezaji mpaka Machi ni shilingi milioni 181, kweli! Asilimia 19.8 halafu tunataka turudi kule?Tunawaambia Watanzania ukweli au tunataka kuwafurahisha? Kwa maoni yangu ya jumla, hapa ambapo mmepaweka ni sawa. Hatuna sababu ya kurudi kwenda kuibadilisha bajeti kwa sababu tunataka kuwa wahalisia zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye maoni yangu. Kwanza kabisa napenda niungane na wenzangu wengi ambao wamechangia kwamba tupate lile ongezeko la shilingi 50 kwenye Mfuko wa Maji ili tufikie shilingi 100, nina uhakika Mfuko wetu wa Maji utatusaidia sana. Kwa hiyo, nami naungana na wenzangu katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niongezee tena zaidi, pamoja na kwamba tunafikiria tuongeze shilingi 50 kwenye mafuta lakini hata kwenye masuala ya vinywaji tunaweza kufanya hivyo. Kuna mmoja wetu hapa alizungumza hili, tukizungumzia vinywaji na bidhaa nyingine ambazo tunatumia kama sigara na kadhalika tukaongeza pale kasenti, tutapata hela ya kwenda kwenye maji, maji mijini na vijijini yatapatikana. Katika kilio kikubwa kuliko vilio vyote, nafikiri hii Wizara ndiyo kilio kikubwa kwetu Wabunge wote. Kwa hiyo, napenda sana niungane na Waheshimiwa Wabunge wengine kuhusu Mfuko wa Maji tuutunishe zaidi uweze kusaidia kwenye suala hili la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye suala zima la umwagiliaji. Nimeangalia ile Tume ya Umwagiliaji ina shilingi bilioni 20 sijui kati ya hiyo shilingi bilioni 600. Tumesema tunataka Tanzania inayoelekea kwenye uchumi wa kati. Uchumi wa kati kwa mpango wetu utakwenda kufanikishwa na uchumi wa viwanda lakini uchumi wa viwanda unataka mapinduzi ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi mapinduzi ya kilimo tutayaleta kwa kutegemea mvua au kwa hii shilingi bilioni 20 iliyotengwa, kweli? Mapinduzi ya kilimo yatafanikiwa pale tu tutakapoamua kuwekeza zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji. Viwanda vyetu vitawezeshwa na malighafi za ndani. Malighafi za ndani zinalimwa hapa na ili zilimwe sawasawa ni lazima kilimo kiwe kilimo chenye tija, endelevu, cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya umwagiliaji kwa kweli hairidhishi. Hata ile Tume ya Umwagiliaji bajeti iliyotengewa Mheshimiwa Waziri pale hatupo sawa sana. Pale nitapenda sana kutofautiana na ninyi. Niombe anaporudi atuambie, maana shilingi bilioni 20 kwa shilingi bilioni 600 unazungumzia chini ya 10% ya bajeti yote inaenda kwenye infrastructure na mambo mengine yote kuhusiana na umwagiliaji, kweli hapa ndiyo tutapata mapinduzi ya kilimo? Haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze kidogo pia kuhusiana na suala zima la Jimboni kwangu. Suala la umwagiliaji tuliwahi kuwasilisha maombi muda mrefu kidogo ya Bwawa moja la Umwagiliaji la Mongoroma ambalo lina ekari 3,000. Ekari 3,000 kama tungeweza kuwekeza, hela iliyohitajika ni kama shilingi bilioni mbili, hela iliyohitajika ingeweza kuwekwa pale ni watu takribani 12,000 wangenufaika. Hebu niambie nimultiplication effect ya kiasi gani, ripple effect ya kiasi gani wananchi wangepata kiuchumi kutokana na kilimo cha umwagiliaji chenye uhakika kwa staili hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri na timu yake, naomba hii miradi ya umwagiliaji tuiangalie sana. Mabwawa kama Mongoroma yangeweza kutusaidia kweli. Nimeona kwenye ripoti ziko sehemu nyingi amezungumzia lakini hebu na kule kwetu mkutazame. Mongoroma andiko letu lina zaidi ya miaka mitatu na tija yake ni kubwa, hata uchumi baadaye ungeongezeka sana kule Kondoa, Warangi wangeanza kufurahi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye masuala hayahaya ya mabwawa, Bwawa la Munguri pale Kondoa ambalo kwa kiwango kikubwa lingeweza kusaidia kupunguza upungufu wa maji Kondoa Mjini na maeneo ya pembezoni lina muda mrefu tumelisemea, limeandikiwa, limefuatiliwa lakini inaonekana kama Serikali imekuwa na kigugumizi kuanza kufanya mchakato wa kushughulikia bwawa lile liweze kupata maji ili wananchi wa Kondoa wanufaike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, basi nashukuru kwa hayo. Nilitamani kumalizia kidogo, lakini naunga mkono hoja, naomba mzingatie hayo niliyoyaeleza.