Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kabla sijatoa hoja yangu ya kuunga mkono niwape pole wakazi wa Jimbo langu la Bunda kwa taabu kubwa waliyonayo ya upungufu mkubwa wa chakula na niwahakikishie kwamba Serikali kwa maelekezo yake hivi karibuni inaweza kuwasaidia kupunguza tatizo walilonalo.

Suala la pili, niwape pole wanavijiji wa barabara ya Bukama, Salamakati, Mihingo na Mgeta ambayo imevunjika daraja zake kwasababu ya mvua na mkandarasi wiki ijayo au wiki mbili zijazo atakuwa kwenye site, kwa hiyo wategemee watapata huduma, kwamba Serikali inawasaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niseme tu kwamba humu ndani pamoja na kwamba tupo Wabunge wengine wa miaka mingi lakini pia kuna wazee humu ndani, hili suala la bajeti ya maji tumelisema sana, watu wameonyesha njia, lakini iko hoja ya msingi kwamba sasa litakwenda kwenye Kamati ya Bajeti ambayo itakaa na kulitazama upya. Sasa kama hiyo ndiyo hoja basi hakuna haja ya kulipinga ni kuliunga mkono tu kwamba pengine katika ongezeko litakalokuja litatusaidia kufanya mambo.

Kwa hiyo, mimi nitaiunga mkono hii bajeti mkono kwa sababu itakwenda na itarudisha majibu ambayo yataleta neema. Mambo mengine haya ya kuota kwamba CCM itakufa lini, unaweza ukakaa miaka mingi tu hujapata jambo hilo kwa sababu CCM pia ni nembo ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kwenye hoja ya msingi ya Jimbo langu la Bunda. Haihitaji kusoma sana kujua kwmana asilimia 72.6 ya huduma ya maji inayopatikana vijijini haihitaji kwenda darasa la saba wala la ngapi. Hivi kwa mfano, kama asilimia 72.6 ndiyo huduma ya maji vijijini, kwa lugha nyingine ni kwamba kama una watu milioni moja maana yake watu 726,000 wanapata maji vijijini. Yaani kama tuna vijiji 1,000 ina maana vijiji 726 tu vinapata maji sasa jamani hivi ni kweli? Maana yake ni kwamba vijiji 274 ndivyo havipati huduma ya maji. Hivi Waziri, wazee wangu hawa mmetoka sijui engineer sijui nini inahitaji hilo kutuuliza? Hivi takwimu hizi tunazipata wapi? Waheshimiwa Wabunge sisi wote tuko humu ndani, kwanini usituambie kila Mbunge atuletee vijiji vyenye huduma ya maji na wewe ukaviona kwenye asilimia? Msikariri bajeti hizi kwa mambo ya kukariri kwenye vitabu jamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, wazee wangu nyie ndiyo mnamalizia hivi, mkishatoka hapa na uwaziri unaacha. Kwa hiyo naomba mjikite kutusaidia sisi. Mbona Waziri wa Nishati na Madini ametuambia leteni vijiji ambavyo havina umeme, tumempa na ameviona vijiji vinaonekana, ninyi kwa nini hamfanyi hivyo? Mnakariri bajeti sio wataalam? Mimi ninawaambia kumekucha hali si nzuri sana. Kwenye Jimbo la Bunda amezungumza mwenzangu hapo, lakini niseme tu nimeandika barua tarehe 26/10/2016, utata wa miradi ya Jimbo la Bunda nikataja mradi wa maji Mgeta-Nyangaranga. Nashukuru kwa sasa hivi mkandarasi yupo lakini bado anasuasua tu, anaweka leo bomba moja kesho haweki, hakuna kinachoendelea pale, mradi una miaka sita unahangaika tu, haiendi vizuri. Barua hii haikujibiwa; hata sikujibiwa mimi kama Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kupewa nilichoandika jamani ni sawa? Mheshjimiwa Waziri nimekuja kwako, Mheshimiwa Naibu Waziri nimekuja kwako, kwa Katibu nimeenda, sasa mnataka tuende wapi? Wazee wangu mnataka tuende wapi tuseme? Mradi wa Maji Mgeta matatizo, Mradi wa Nyamswa Salama Kati mmetenga shilingi 367,291,127, wanasema mradi umetengenezwa kwa asilimia 55 umekufa una miaka mitatu; mnataka twende wapi? Nimezungumza mkasema mtarekebisha miradi ya zamani iendelee, lakini hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Mradi wa Kilolei shilingi milioni 400, vijiji vya Nyabuzume, Kiloleni na Kambugu shilingi milioni 400, ile mnasema visima kumi. Nimewaambia ofisini hakuna kinachoendelea, mnasema tuseme nini sasa kwenye hili? Ameandika Mhandisi wa Wilaya ya Bunda tarehe 1 Juni, 2016 miradi ya viporo vya madeni ya wakandarasi wa mradi wa maji Wilaya ya Bunda; mmeleta shilingi bilioni tano. Miradi karibu asilimia sabini na kitu asilimia haifanyi kazi, ninyi mkija kwenye asilimia hapa mnaandika maji yanapatikana Bunda, hayapo, hayapo Bunda.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ndugu zangu wamekuja watu wa JICA tumewapa taabu kubwa sana, tumewaambia watusaidie kwa sababu kwenye Jimbo langu la Bunda lina ukame mkubwa, wametuambia tufanye bajeti tumewapelekea bajeti ya dola 63,879 ya ukarabati ya marambo yaliyoingiliwa na magugu maji.

Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri mliwahi kujibu hapa Bungeni kwamba mwaka huu mtafanya ukarabati wa malambo sita, iko wapi mzee wangu? Sasa mnafikiria sisi Wabunge tufanyaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, JICA hawa hawa wamesema tutengeneze malambo, tumewapa bajeti ya dola 255,237.17 tusaidieni basi, tusaidieni kwenye JICA hawa ambao wametuona kwenye tatizo mtusaidie kutusemea watusaidie. Jimbo la Bunda lina ukame wa kutisha, Jimbo hilo hilo ndio lina tembo wanaokula mazao ya watu kila siku, lina watu wana taabu zao kule; tunaomba mtusaidie kwenye jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona mradi wa umwagiliaji Bunda. Mradi wa umwagiliaji maji wa Nyatwali hauko Jimbo la Bunda, haupo Wilaya ya Bunda uko Bunda Mjini. Bunda DC kuna mradi wa umwagiliaji wa Maji unaoitwa Mariwanda pamoja na mradi wa Kasugutwa wa Buramba, haiku kwenye bajeti yanu; na kwenye takwimu zenu mnaonesha kwamba Mradi upo Bunda DC lakini upo Bunda Mjini. Kwa hiyo, naomba mlirekebishe hili na mradi wetu wa Mariwanda muufanyike kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu hebu tusaidieni, kama mmepewa hiyo Wizara na hali ndio hii inaenda miaka miwili sasa inaenda miaka mitatu na ninyi wazee ma-engineer mpo hapo, watu wazima ambao tunawategemea mtusaidie na hamna plan mpya ya kukomboa mambo ya maji, tunakaa na ninyi humu kufanya biashara gani? Maana sasa lazima tuwaambie kwamba miaka mitatu ijayo mtuambie mmeingia humu ndani mmekomboa nini au ndiyo zile asilimia mnazoimba tu asilimia 72 wakati hazipo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri naomba nimeandika kwenu, nimewaleta, kwenye Jimbo langu mnasema kwamba miradi ya zamani iendelee kuwepo; na kwangu miradi ya zamani ipo, endeleeni kunisadia au mnampango wa kuniondoa huko ndani? Mniambie sasa mapema nijue.