Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Andrew John Chenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii nami niweze kuchangia kwenye hoja hii. Nitamke naunga mkono hoja hii mia kwa mia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Naibu wake na timu yake kwa kuandaa hotuba nzuri, ina taarifa nyingi za manufaa kwa maendeleo ya nchi yetu. Mnyonge mnyongeni lakini haki tuwape. Hii Wizara inajitahidi sana Waheshimiwa, kwa nchi nzima tunaona sura hiyo lakini ni kwa saabu ya rasilimali fedha ambalo ndilo linalotusumbua wengi hapa, lakini tunawapongeza wanafanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mkoa wa Simiyu, naendelea kuishukuru Serikali kupitia hotuba hii kwa mradi mkubwa ambao ni wa kihistoria kwa Mkoa wa Simiyu kutoka Ziwa Victoria ambao utahusisha Wilaya zote tano za mkoa huo. Lakini nitakuwa mchoyo sana wa fadhila nisipotambua kazi kubwa iliyofanywa na Rais mstaafu Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete, maana yeye tangu mwaka 2005 alipoingia madarakani ndio amehangaika sana na mradi huu kwa kutambua hali halisi ya ukame katika Mkoa wa Simiyu. Mimi naamini mbele ya safari mradi huu utakapokamilika hata katika awamu ya kwanza wamkumbuke angalau awepo katika uzinduzi wa mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nirudie tena kumshukuru sana Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, juzi alipokuwa Bariadi aliusemea mradi huu kwa nguvu na akamaliza kabisa akakata mzizi wa fitna kuhusiana na mradi huu ambao ulikuwa umeanza kuoneshwa kuhusu wapi matenki ya maji yakae na alisema bila kumung’unya maneno mradi huu utatekelezwa na matenki ya maji yatakaa palepale kwenye Mlima wa Ngasamo, tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utekelezaji, mimi ningependa tu Waziri labda kesho anapohitimisha anithibitishie, kwa sababu mradi huu umesanifiwa kwa kutambua hali halisi ya mkoa huo, kwamba yatakuwepo mabomba makubwa mawili, bomba moja la maji ambayo hayakutiwa dawa (raw water) na bomba lingine ndiyo la maji safi ambayo ndiyo yatatumika kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lile la maji ambayo hayakusafishwa, hayakutiwa dawa ni kusaidia kurejesha hali ya uoto wa asili katika maeneo hayo lakini pia kwa mifugo; na ndiyo maana hoja kubwa ya mradi huu ilikuwa ni kuangalia hali nzima ya mkoa huo ili mifugo hii isiende maeneo mengine kwenda kuharibu mazingira. Kwa hiyo ningependa hiyo confirmation tuipate, kwamba bado dhana ni ile ile katika usanifu wa mradi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali, nimeona pesa ambazo zimetengwa kwa Mji wa Bariadi ambao ni makao makuu ya Mkoa wa Simiyu. Mahitaji ya maji ni makubwa, idadi ya watu inazidi kuongezeka Bariadi na viunga vyake, tunahitaji hizo pampu tano kwa sababu visima vile vitano vimechimbwa mwaka juzi na viko pale. Sasa tungependa tupate umeme, ziunganishwe, tuongeze uzalishaji wa maji na tusambaze kwa matumizi ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye Jedwali Namba 5A, pesa ambayo imetengwa kwa kutekeleza miradi ya maji vijijini. Nina vijiji vitatu ambavyo tumepata maji tangu mwaka 2012; vijiji hivyo ni Igegu, Masewa na Sengerema katika kata ya Dutwa, kata ya Sapiwi na kata ya Masewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wananchi hawa wanajua kuna maji, wanafahamu, waliyaona wakati wanachimba visima hivi, ningependa sasa zile pesa ambazo nimeziona angalau zikatumika katika kusambaza mabomba ili maji yatoke chini yawafikie wananchi hawa kwa matumizi ya maendeleo yao. Naendelea kushukuru Serikali, nimepata maji ya msaada wa Serikali ya Misri, kisima kirefu pale Kololo lakini nazidi kuomba tena kwa Ngulyati, Mhango na Kasoli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu skimu ya umwagiliaji, nimeona ya Mwasubuya, lakini tuna eneo kubwa ambalo tunaamini Kasoli tukiweza kujenga bwawa kubwa tukafanya shughuli ya umwagiliaji sehemu kubwa ya eneo la Simiyu tutaweza kujitosheleza kabisa kwa mahitaji yetu ya chakula, kwa hiyo, naiomba Serikali ione hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije sasa mwisho, kwamba niliposema mnyonge mnyongeni. Waheshimiwa Wabunge na mimi nakubaliana na walionitangulia kwa kusema kwamba tutafute njia nzuri ya kuishauri Serikali ituongezee pesa katika Wizara hii na njia nzuri ni hii ambayo kesho Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha hoja hii, tujaribu kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, naona nia njema ya Serikali, lakini tukifuata Kanuni zetu suala hili likarejeshwa kwenye Kamati ya Bajeti tuweze kufanya uchambuzi wa kina, njia ambayo naiona ya haraka ambayo hata kwenye ukurasa wa 13 wa hotuba hii mnaona, iliyonyanyua bajeti hii ni tozo ya shilingi 50. Asilimia 52.7 ya pesa ambazo zimefika zimetokana na tozo hii. Sasa hivi kwa wastani tunaingiza lita bilioni 1.8 za dizeli na lita bilioni 1.2 za petroli. Tukiangalia kwa suara hiyo uwezekano wa kupata fedha tukaongeza kwa asilimia 100 tena yaani shilingi 50 na tukipiga mahesabu tunaweza tukaongeza shilingi 100. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unafahamu maendeleo lazima tuyatolee jasho na ninawaomba sana Waheshimiwa Wabunge safari hii hii lugha ya kusema kwamba tutaongeza mfumuko wa bei, tulikatae kwa sababu sio hoja ya msingi. Hii inawezekana tukayafanya haya, mahitaji ya maji kwa watu wetu ni makubwa na tunaona, sasa tukiendelea namna hii hatutafika kokote, mimi ndiyo ushauri wangu na inawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii.