Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya ya kuweza kusimama ndani ya Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea, kwa vile ni mara yangu ya kwanza kuzungumza katika Bunge hili la Kumi na Moja, napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru kwa moyo wangu wa dhati kabisa wanawake wa Mkoa wa Kigoma kwa kunirejesha Bungeni kwa mara nyingine na mimi nasema sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa ushindi mnono alioupata. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri wengine kwa kuteuliwa ku wa Mawaziri katika Baraza la Mawaziri la mwaka 2016. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kuendelea kuishukuru Serikali kwa moyo wangu wa dhati kwa kuendelea kufanya mambo mazuri katika Mkoa wa Kigoma. Naishukuru sana na naendelea kuwapongeza viongozi wa Awamu ya Nne walioweza kuufungua Mkoa wa Kigoma. Daima tutamkumbuka Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuweza kuufungua Mkoa wa Kigoma, lakini na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi ambaye kwa sasa ni Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa waliyoifanya ndani ya Mkoa wa Kigoma. Walitujengea barabara, wakatujengea Daraja la Mto Malagarasi maarufu kwa jina la Kikwete, daraja kubwa ambalo ni mfano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi cha mwaka 2015 niliwahi kusimama nikasema wananchi wameona na kwa vile wameona hawatatuangusha. Wakati ule tulikuwa tukiitwa sisi ni wapinzani lakini tuliufuta upinzani sisi ni Chama Tawala. Naomba nimshukuru Katibu Mkuu na aliyekuwa Katibu Mwenezi kwa kazi kubwa waliyofanya ya kuwaelimisha wananchi wa Mkoa wa Kigoma Ilani ya Chama cha Mapinduzi ilivyokuwa ikitekelezeka na hatimaye tukaweza kurejesha Majimbo yaliyokuwa yamepotea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa barabara zile ambazo hazikukamilika ikiwepo barabara ya Kigoma – Kasulu – Nyakanazi iweze kujengwa. Pesa zilizotengwa zipelekwe ili barabara ile iweze kukamilika. Pia kipo kipande cha kutoka Uvinza - Malagarasi kilometa 48 kwenda kwenye Daraja la Mto Malagarasi kwenye Daraja la Kikwete, naomba kilometa hizo ziweze kujengwa kusudi wananchi waweze kupata manufaa kupitia barabara hiyo. Kipo kipande kingine kutoka Chagu - Usinge - Kaliua, nacho naomba kiweze kukamilishwa kutuunganisha na Mkoa wa Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 43 kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, amezungumzia kuhusu reli. Reli katika Mkoa wa Kigoma, Tabora na Ukanda wa Ziwa ni kilio kikubwa sana. Kabla reli nyingine haijajengwa tunaomba reli ya kati iweze kujengwa kwa sababu itakuwa ni mkombozi kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma, Tabora na Kanda ya Ziwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi huu wa reli tunaomba uwe ni wa kutekelezeka isiwe ni ahadi isiyotekelezeka kwa sababu kwa muda mrefu tumekuwa tukisema kwamba reli itajengwa, lakini haijengwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kwa wakati huu iwe ahadi ya kutekelezeka, isiwe ni ahadi isiyotekelezeka kwa sababu reli inaboresha uchumi. Reli ikijengwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma pamoja na Tabora wataweza kunufaika na uchumi wao utaweza kuimarika. Reli itaweza kufungua fursa ya kibiashara kati ya nchi jirani na Kigoma itakuwa ni kitovu cha biashara. Watu wa Burundi, DRC wataweza kusafirisha mizigo yao kwa kupitia Mkoa wa Kigoma na reli hiyo ya kati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwa muda mrefu kabisa wananchi wa Mkoa wa Kigoma mpaka sasa hivi barabara hazijaweza kukamilika vizuri na kwa sababu hiyo reli ndiyo usafiri wa bei nafuu. Kwa sababu sasa hivi mtu akitoka Kigoma kuja Dar es Salaam anatumia shilingi 70,000 hapo hajapata chakula njiani, kwa kutumia basi anaweza kufika Dar es Salaam kwa shilingi 100,000 lakini reli ikikamilika itawapunguzia gharama ya usafiri wananchi wataweza kusafiri kwa bei nafuu na wataweza kusafirisha mizigo yao kwa bei nafuu lakini gharama za maisha nazo zitashuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, sasa hivi mfuko wa cement Dar es Salaam shilingi 13,000 mpaka shilingi 14,000, lakini Kigoma shilingi 19,500. Tunaomba reli ikamilike ili wananchi wanaotumia reli waweze kunufaika lakini hivyo hivyo kwa kupitia reli uchumi uweze kukua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sasa kuzungumzia kuhusu elimu. Kwanza naomba niipongeze Serikali kwa kuondoa ada kwa wanafunzi. Watoto wengine wa shule walikuwa wanafichwa kwa sababu ya ada lakini kwa sababu ada imeondolewa wanafunzi sasa wamepelekwa shuleni kwa wingi. Darasa la kwanza mwaka huu tumeona wameanza kwa wingi na ninaamini wataendelea hivyo hivyo ni kwa sababu Serikali imeondoa ada kwa wanafunzi. Naomba ada hii isiwe tangu darasa la kwanza mpaka form four iendelee mpaka form six ili watoto waweze kusoma kwa wingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuondoa ada tuangalie sasa ni jinsi gani tunawekeza katika elimu. Ninaamini watoto watakaomaliza form four watakuwa wengi, wengine watabahatika kuendelea na wengine wengi hawataendelea watarudi kukaa vijijini. Kwa hiyo, naomba kabisa Serikali iwekeze katika kujenga vyuo vya VETA ili watoto wanaomaliza kidato cha nne na pengine form six waweze kwenda kusomea VETA, hatimaye wajiajiri katika shughuli za mikono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba niwasemee walimu ambao wanadai stahiki zao nyingi. Wapo walimu ambao wamepandishwa madaraja na wamestaafu na walikiri kupanda daraja lakini mpaka wanastaafu mishahara yao haijaweza kurekebishwa. Nilitaka kuuliza, je, Serikali itafanya marekebisho kwa kutumia mishahara yao pale walipopanda madaraja? Kama si hivyo, naomba Waziri anayehusika wale ambao watakuwa na malalamiko wamepanda daraja mishahara haijarekebishwa waweze kurekebishiwa mishahara yao kusudi wanapotapa pesheni zao iendane na mishahara yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie maji. Maji ni afya, maji ni uhai. Kwa muda mrefu wanawake wa Tanzania wameendelea kuteseka kwa kukosa maji. Sisi Tanzania tumejaliwa kuwa vyanzo vingi vya maji, tumejaliwa kuwa na bahari, maziwa, mito mikubwa na modogo.
Kwa hiyo basi, naomba Serikali ijipange kutumia vyanzo hivyo ili kuweza kufikisha maji vijijini na kuwaondolea adha wanawake ambao wamekuwa wakipata shida kufuata maji kwa umbali mrefu na kukosa muda wa kufanya shughuli za kuwaletea maendeleo na kuinua kipato chao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Kasulu ipo miradi iliyoanzishwa lakini miradi hiyo haijaweza kukamilika kwa sababu fedha zimekuwa hazipelekwi. Naomba sasa katika bajeti hii fedha zipelekwe ili miradi iliyoanzishwa katika Wilaya ya Kasulu iweze kukamilika. Ipo miradi ya Kasangezi, Ahsante Nyerere, Helushingo na Nyarugusu.
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umemalizika.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.