Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Hawa Mchafu Chakoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu.
Awali ya yote, nipende kumshukuru Mwenye Mungu, mwingi wa rehema na mwenye kurehemu, lakini pia nipende kuwashukuru wanawake wa Mkoa wa Pwani kwa kuniamini niweze kuja kuwawakilisha. Sambamba na hilo, napenda niwashukuru wanawake wa CCM Taifa na Chama changu cha Mapinduzi kwa kuniteua Mbunge wa Viti Maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati naelekea kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu, napenda kutoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na timu yake ya Baraza la Mawaziri inayoongozwa na Jemedari Mkuu, Waziri wetu Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kwa kazi nzuri wanayoifanya ambayo inavutia moyoni mwa Watanzania, kwa kazi nzuri wanayoifanya ambayo inaleta furaha katika macho ya Watanzania. Hakika Mungu mbariki Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza lake la Mawaziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu kwa kuanza ukurasa wa saba. Katika ukurasa wa saba hotuba hii inajielekeza katika namna ya kuchukua hatua kuhakikisha wanaongeza mapato na wanabana mianya ya ukwepaji kodi. Mimi nipende kuunga mkono jitihada hizi, ni jambo jema sana na I believe for sure kama tuna uwezo wa kukusanya hata zaidi ya shilingi trilioni 1.3 endapo TRA itajizatiti kweli kweli lakini pia kila Mtanzania atimize wajibu wake, anayepaswa kulipa kodi alipe kodi, tudai risiti tunapofanya manunuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuelekea kuongeza mapato kama ambavyo Serikali imedhamiria tuna shida moja, EFD mashine bado kuzungumkuti. Suala zima la EFD mashine ni tatizo. Nimeshashuhudia nimepata risiti za aina tatu tofauti pale unapofanya manunuzi. Kuna risiti ambayo unakuta ina maelezo ambayo kwa mtazamo wangu mimi naweza kusema yamejitosheleza. Kuna TIN namba pale, utakuta jina la ile kampuni ama kile kituo cha kufanyia biashara, kuna VRN pale lakini pia utakuta jumla ya amount uliyonunua, muda, tarehe pamoja na ile amount inayokuwa deducted kwenda Serikalini, lakini zipo risiti nyingine zinazotoka katika hii mashine unakuta zina lack hizo details. Kwa hiyo, naomba sana hili suala la EFD mashine tuliangalie vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia baadhi ya wafanya biashara hawana hizi mashine, wanaendelea kutumia risiti za kuandika. Niseme kwamba hizi risiti siyo afya sana katika ongezeka la ukusanyaji wa mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimewahi kwenda petrol station kuweka mafuta, nimeweka saa tatu asubuhi lakini risiti inaniandikia nimeweka saa tano usiku. Kwa hiyo, inaonekana kwamba hizi mashine watu wanaweza kucheza nazo. Kwa sababu hiyo, nasisitiza tena tuziangalie mashine hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwenye petrol station kuna matatizo makubwa sana ndiyo maana nasisitiza TRA inabidi ijizatiti au ifanye kazi kweli kwenye hili suala la ongezeko la mapato. Utakuta kuna visima viwili, cha dizeli na petroli, vya dizeli viwili na vya petroli viwili, kimoja ni cha risiti ya kuandika na kingine ni cha risiti ya TRA. Kwa hiyo, naomba sana katika suala hilo mnaohusika mliangalie kwa ukaribu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mchango wangu mwingine uko katika ukurasa wa 16 ambao unazungumzia shilingi milioni 50 katika kila kijiji lakini pia umeelezea maandalizi ya namna fedha hizi zitakavyowafikia walengwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha vikundi vya kiuchumi vinavyokidhi vigezo. Hii ni ahadi ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo unaikuta katika Ibara ya 57(d) kwa ruhusa yako naomba nikisome na kinasema; “kutenga kiasi cha shilingi milioni 50 katika kila kijiji kama mfuko wa mzunguko (revolving fund) kwa ajili ya kukopesha vikundi vya wajasiriamali kupitia ushirika wa kuweka na kukopa (SACCOS) katika vijiji husika.” (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha kampeni kilichokuwa kinawavuta Watanzania wengi ni pamoja na kifungu hiki cha 57(d) cha shilingi milioni 50 katika kila kijiji. Ukiangalia muktadha wa hiki kifungu hizi shilingi milioni 50 siyo kwamba watu watagawiwa, watakopeshwa then watarudisha. Wakati wa ziara yangu ya kushukuru wapiga kura wa Mkoa wa Pwani nilipata maswali kutokana na kifungu hiki, wazee wanauliza wao watanufaika vipi na kifungu hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi wazee ambao wameshafika umri wa kushindwa hata kufanya kazi huoni moja kwa moja kama kinaweza kuwanufaisha. Isipokuwa naomba Serikali masuala mazima ya mapendekezo ya universal pension, pension kwa wazee wote yaweze kufanyiwa kazi kwa haraka ili yaende sambamba na hii shilingi milioni 50. Wakati watu wenye nguvu zao wananufaika na hii shilingi milioni 50 kukopa na kufanya biashara ama ujasiriamali basi wazee waweze kunufaika na pension ya wazee wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine uko ukurasa wa 23 ambao unazungumzia suala zima la kazi na hifadhi ya jamii. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambayo inaelezea mwelekeo wa shughuli za Serikali, nilitarajia kuuona hapa Mfuko wa Fidia (Workers Compensation Fund – WCF). Sikukuu ya Mei Mosi mwaka jana kati ya mambo ambayo Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi alifafanua na kueleza kwamba kati ya mafanikio ya Serikali yake basi ni pamoja na kuanzishwa kwa Workers Compensation Fund.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nipende kusema na niwe mkweli na utakubaliana na mimi kabisa kati ya kitu ambacho Serikali ya Awamu ya Nne imefanya kwa wafanyakazi wa Taifa hili basi ni pamoja na kuanzisha Mfuko wa Fidia Kazini. Ikumbukwe hapo awali ilikuwa inatumika sheria ya zamani, Sheria ya Fidia, Sura Na.263 ambapo mtumishi akiumia kazini, akipoteza kiungo alikuwa analipwa shilingi 108,000 kwa upande wa wafanyakazi wa private lakini kwa upande wa wafanyakazi wa public sector ilikuwa inatumia Sheria ya Public Service Act ambayo mtumishi akiumia ama akipoteza kiungo ama ulemavu wa maisha alikuwa anapewa shilingi milioni 12 na yenyewe ilikuwa inatolewa once.
Kwa hiyo, naomba sana Waziri Mkuu na Waziri mwenye dhamana ya kazi na hifadhi ya jamii kuuangalia mfuko huu kwani umeelezea namna njema ya kuwafidia wafanyakazi wetu wanapoumia ama kupoteza viungo sehemu yao ya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitapenda tena kujikita ukurasa wa tano wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambao unazungumzia uwajibikaji na maadili ya viongozi wa utumishi wa umma. Baadhi ya watumishi wa umma walifika mahali walijisahau sana, lakini pia baadhi ya watumishi wa umma wasiokuwa waadilifu hao ndiyo walikuwa wameigharimu Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Hata hivyo, Serikali yetu ya Awamu ya Tano imeamua kuchukua hatua ku-deal na hawa watu ambao walikuwa hawana uadilifu wametumia madaraka yao vibaya ama wametumia nafasi zao vibaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, cha kushangaza wenzetu hawa hawa waliokuwa wanapigia kelele kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inachelewa kuchukua hatua leo wamekuwa mstari wa mbele kutetea wabadhirifu, wamekuwa mstari wa mbele kutetea mafisadi, wamekuwa mstari wa mbele kutetea watumishi ambao hawana maadili. Wamekuwa vigeugeu, ni wao ndiyo waliokuwa wanasema tunaenda taratibu, sasa tunaondoka na supersonic speed, wanatoka tena mbele na kuanza kuwatetea wale watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine…
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Hawa Chakoma naomba ukae, Mheshimiwa Cecilia Paresso...
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema kwamba taarifa yake siipokei nimei-shred, lakini pia nipende kumkumbusha anaweza akaenda YouTube akaona Mwenyekiti wao Mbowe analalamika watumishi wa umma ambao wanasimamishwa anataka wahojiwe kwanza, tayari TAKUKURU imeshatoa ushahidi, anahojiwa kitu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naenda ukurasa wa tisa unaozungumzia kukua na kuimarika kwa demokrasia. Nchini Tanzania demokrasia imekuwa na ndiyo maana kuna uwepo wa vyama vingi. Pia niseme tunatambua uwepo wa upinzani nchini, tunatambua uwepo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na tunatambua chama kikuu cha upinzani. Wakati tunaelekea kwenye mustakabali wa kuwafanya Watanzania wawe na maisha bora, ukiacha kazi nzuri inayofanywa na Chama Tawala ama na Serikali, pia tunahitaji mchango makini kutoka kwa chama cha upinzani ama Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Kama tunakuwa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambayo kwanza haiko makini, mbili inaendeshwa na mihemko, tatu inaendeshwa na sintofahamu, hatuwezi kufika mahali kokote.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Hawa Chakoma umemaliza muda wako.