Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuinua Sekta ya Sanaa, Michezo pamoja na kusimamia mambo yote yanayohusu Wizara hii. Naomba kuchangia katika hotuba hii maeneo yafuatayo:-

Kuimarisha huduma na mitambo ya TBC; niungane na hotuba ya Kamati husika juu ya ushauri wao wa kuwekeza kiasi cha kutosha kwa Shirika letu la TBC kama ambavyo Kituo cha AZAM walivyofanya, naamini pamoja na majukumu mengi ya Serikali, lakini kuimarisha TBC ni muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, TBC ndio ambayo imetapakaa nchi nzima na Shirika la Taifa haiwezekani tuliache shirika letu litoe huduma dhaifu. Watu wengi sasa hawaangalii vipindi vingi vya TBC kutokana na ubora hafifu unaotolewa na TBC na hatimaye watazamaji kupendelea huduma za vituo vingine kama vile AZAM, ITV na kadhalika. Nashauri Serikali ichukue maoni ya Kamati na sisi Wabunge na yafanyiwe kazi.

Mheshimiwa Spika, Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF); Shirikisho letu la Mpira Tanzania (TFF) kwa kiasi kikubwa wanajitahidi kutekeleza wajibu wao wa kila siku mfano ni jinsi walivyosimamia timu yetu ya mpira iliyopo Gabon kwenye mashindano ya vijana chini ya miaka 17 .

Mheshimiwa Spika, kuna mambo ningependa nishauri juu ya Shirikisho letu la Mpira Tanzania (TFF), hivi kwa nini inajitokeza mara kwa mara Shirikisho letu limeingia katika mgogoro na vilabu vyote vya mpira? Mfano ni suala la klabu ya Kagera kunyang’anywa pointi tatu walipocheza na Simba, suala hili linalichafua sana Shirikisho letu la mpira. Hivi

TFF haina wataalam wa kutosha ambao wangeweza kushauri hili kumalizika kwa haraka na kutoa haki.

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana atoe majibu yenye kuridhisha kwa sababu TFF wapo chini ya Wizara yake.

Mheshimiwa Spika, Viwanja vya Mpira; viwanja vya mpira ni chachu ya maendeleo ya mpira nchini, tunavyo viwanja vichache vyenye hadhi, nishauri Serikali isimamie viwanja vilivyopo mikoani vifanyiwe ukarabati hususani maeneo ya kuchezea mpira. Inasikitisha kuona kwa takribani miaka 50 sasa tuna viwanja visivyozidi 10 vyenye hadhi ya Kimataifa. Nishauri Wizara hii kwa kushirikiana na TAMISEMI ihakikishe kila Wilaya inakuwa na kiwanja cha mpira ili kuleta maendeleo ya mpira nchini.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri asilimia 90 ya watangazaji na waandishi kukosa sifa stahiki ya taaluma ya uandishi wa habari na utangazaji. Jambo hili linasikitisha sana niombe sasa TCRA wahakikishe kuwa vituo vyote vya utangazaji vinazingatia sifa na vigezo ili huduma zitolewe na watu wenye sifa. Hivi inakuwaje vituo kuajiri watu wasiokuwa na sifa? Je ni hatua zipi zimechukuliwa kwa vituo vya utangazaji vilivyo na waandishi na watangazaji wasio na sifa?


Mheshimiwa Spika, nipongeze sana Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI kwa utaratibu wa kuandaa vijana na TFF kuandaa vituo vya Ufundi kila mkoa kwa madhumuni ya kulea vijana. Jambo hili ni zuri sana na kama litasimamiwa vema litaleta maendeleo ya dhati na ya kweli ya mpira nchini.

Mheshimiwa Spika, jambo hili linahitaji kuwa na rasilimali fedha, sijaona wapi Wizara imetenga fedha katika kutekeleza mpango huu. Vile vile napongeza ushauri wa sisi Waheshimiwa Wabunge kuanzisha vituo vya mfano huu katika maeneo yote ya Majimbo.