Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Salma Mohamed Mwassa

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Spika, kwanza kwa masikitiko makubwa sana niungane na Wabunge wenzangu kutoa pole kwa msiba huu tulioupata wa kupoteza watoto wetu hawa ambao walikuwa na ndoto kubwa za kulipeleka Taifa letu mbele. Wanafunzi 32 ni msiba mkubwa mno, hilo darasa sijui watakuwa wamebaki wanafunzi wangapi na mtihani wao wa kitaifa utakuwaje. Kwa hiyo, nahuzunika sana kwa msiba huu.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nijielekeze kuchangia Wizara hii ya Habari, Utamaduni na Michezo. Kwanza kabisa nichangie kuhusu kulinda utamaduni wa Taifa letu. Katika kulinda utamaduni wa Taifa letu kuna mambo mengi ya kuangalia kama uvaaji wetu na mengine mengi. Kuna tabia ya uvaaji wa nusu uchi hasa kwa jinsia ya kike, wanawake wengi wanavaa uchi yaani nusu uchi kabisa. Ukiangalia maigizo unakuta wanaume wamevaa vizuri kabisa lakini wanawake wapo nusu uchi. Sijui Serikali ina mpango gani katika suala hili au hamlioni? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano Mashindano ya Miss Tanzania, hivi ni lazima uwe uchi ndiyo ushinde Miss Tanzania? Kwa kiwango kikubwa ukiwaangalia Ma-miss wanavaa nusu uchi kabisa na hiyo nafikiri ndiyo imeleta ugumu hata kumchangia yule Miss Tanzania aliyekuja hapa watu wanaona kwamba hii tasnia ni kama ya kuaibisha fulani yaani siyo utamaduni wetu kama Waafrika au Watanzania, mwanamke uvae uchi. Unakuta kabisa nguo zao asilimia 80 ya mwili wake uko uchi amevaa sehemu ndogo tu. Mimi niulize ni nini hasa kinachofanya iwe hivyo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi mtu huwezi kuwa covered kabisa kwenye vazi lako la kibantu ukawa Miss Tanzania? Hata ukienda huko kwenye mashindano ya Miss World ukivaa full itajulikana kabisa hivi ndivyo Watanzania wanavyovaa, lakini ukiangalia modern culture unavaa nusu uchi unaenda huko worldwide unavaa totally uchi, Watanzania huwa hatuvai uchi na hatuna kabila lolote ambalo linalovaa vazi lake uchi, sasa sielewi utamaduni huu wa kuvaa uchi umetoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwenye maigizo wanaume wamevaa lakini wanawake wako uchi, nusu uchi. Hata kwenye sanaa mbalimbali iko hivyo yaani mwanamke kuwa uchi imeonekana kama ni kivutio, hilo silikubali kabisa. Mheshimiwa Waziri anavyokuja kihitimisha hapa atueleze ana mpango gani na huu uvaaji wa nusu uchi kwa wanawake? Maana inaonekana mwanamke kuvaa uchi ni kivutio, akiwa covered …

MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Spika, nafikiri huyo mtani wangu Mngoni naye haelewi Kiswahili vilevile, kwanza hawa siyo Watanzania. Wangoni toka lini wakawa Watanzania hawa wametoka South Africa tumewapokea tu, kwanza hapa wakae kwa passport na muwe na permit kabisa Wangoni toka lini mkawa Watanzania nyie. (Kicheko)

TAARIFA...

MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Spika, siipokei taarifa hiyo. Namaanisha kuvaa nguo nusu uchi, simaanishi uchi, kwa maana baadhi ya sehemu sensitive za mwili wa mwanamke zinakuwa uchi, ndiyo ninachomaanisha siyo kwamba ni kuvaa nusu uchi, asilimia 80 watu wanakuwa uchi.

Mheshimiwa Spika, pia napenda kuongelea suala la waandishi kuwekewa mazingira magumu au kuvamiwa wanapofanya kazi zao. Waandishi wa habari mara nyingi wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao hasa kwenye mikutano ya vyama vya upinzani wanakuwa wakivamiwa, wanakuwa hawana uhuru kabisa wa kuandika zile habari au vinginevyo.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano tukio lililotokea Vina Hotel Dar es Salaam, waandishi wamevamiwa, wamepigwa mpaka sasa hivi hatujui ripoti imekaaje, lakini mimi nasema kwamba Serikali iwalinde waandishi wanapotekeleza majukumu yao. Waandishi ni kioo cha jamii, wanatakiwa waandike habari zote kutuhabarisha umma aidha habari za vyama vya upinzani au chama tawala wawe huru kote. Sasa hivi inavyoonekana wanapata hofu sana kuja hata kwenye mikutano ya vyama vya upinzani kwa sababu mara nyingi wanavamiwa lakini haionekani kama suala hili linachukuliwa in a sensitive way. Kwa hiyo, niombe Serikali iwalinde waandishi wa habari.

Mheshimiwa Spika, vilevile niende kwenye Vazi la Taifa, ukiangalia tuna Wimbo wa Taifa, Bendera ya Taifa lakini hatuna Vazi la Taifa, kwa nini? Lazima tuwe na Vazi la Taifa, tujivunie utaifa wetu kama Tanzania, lakini miaka kama mitano iliyopita Vazi la Taifa linaongelewa, sasa Waziri atuambie kabisa hapa taratibu za utafutaji wa Vazi la Taifa imeishia wapi au kikwazo ni nini. Naomba Waziri atueleze wazi Vazi la Taifa tunalipata lini hapa Tanzania ili na sisi tuwe na Vazi la Taifa.

Mheshimiwa Spika, vilevile niongelee suala la uchakavu wa mitambo TBC. Kwenye hotuba ya Waziri ameeleza kabisa kwamba amewatengea bajeti ya maendeleo ya shilingi bilioni moja kuhusu usikivu wa TBC, lakini nimtaarifa Mheshimiwa Waziri kwamba bajeti hiyo haifai kitu kabisa kwani TBC ina mitambo chakavu hamna mfano. TBC ni mtoto wa Serikali na kama ni mtoto wako usimfanye wa kufikia, mbona hana competition na vyombo vingine vya habari. Mitambo yote ni chakavu, haisikiki sehemu nyingi kwa mfano ukiangalia wilaya za vijijini huko kwa mtani wangu Mngoni huko Ruvuma kote haisikiki, aseme hapa kama inasikika, hakuna, Ruvuma na sehemu nyingine kote haisikiki kutokana na uchakavu wa mitambo.

Mheshimiwa Spika, ninachomshauri Waziri aendelee kutafuta pesa, hiyo bajeti ya shilingi bilioni moja ni ndogo hawawezi kufanya kitu chochote pale kwa sababu mitambo yao ni chakavu kabisa. Nashauri muwatengenezee mitambo ile ili kionekane kweli ni chombo cha Taifa. Hata wafanyakazi maana sasa hivi wafanyakazi wenyewe wa TBC wanaona aibu hata kujitambulisha wao ni wafanyakazi wa TBC kutokana na watu wasivyoipenda kwa sababu ya kutosikika vizuri. Kwa hiyo, kama huyu ni mtoto wa Serikali inabidi aendelezwe vizuri, Waziri atafute pesa kwani hii shilingi bilioni moja haitoshi kabisa.

Mheshimiwa Spika, pia niongelee kuwaandaa vijana wetu kimichezo. Katika shule zetu za msingi kuna wanafunzi wenye taaluma mbalimbali naona sasa wakati umefika kuibua vipaji vya wanafunzi hawa tusisitize michezo ifundishwe kabisa mashuleni kama ilivyokuwa mwanzo. Mwanzo kulikuwa na UMISETA na michezo mbalimbali sasa hivi naona kabisa imefifia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia katika English Medium hizi shule za private michezo hawana kabisa, nashauri Waziri afuatilie ili nao wao wawe na mashindano kama ilivyo katika shule za Serikali. Ukiangalia English Medium zote watoto hawana michezo yoyote wapowapo tu, hamna mchakamchaka yaani hawaeleweki. Naomba Waziri wa Elimu aangalie hizi shule binafsi wawe na mazingira ya watoto kucheza, wanakuwa dormant, hawajielewi na wakati tuna watoto wengi kule ambao wangeweza kuwa ile timu yetu ya Serengeti Boys. Ile timu yetu Taifa Stars wale wanaendelea kuzeeka, kwa hiyo tunatakiwa tuendelee kuandaa vijana wengine huku toka kwenye shule zetu. Kwa hiyo, nashauri tuendelee kuandaa vijana katika mtiririko unaoeleweka.

Mheshimiwa Spika, ahsante.