Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Halima Abdallah Bulembo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa juhudi zake kubwa anazozifanya za kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata maendeleo. Vilevile naomba kuwapongeza ndugu zangu Wazanzibar kwa kumaliza uchaguzi salama, kwa kurudi na amani, sasa ni kazi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajielekeza kwenye hoja yangu, naomba sana kumshukuru Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo kwa suala zima alilosimamia kuhusu kuonekana kwa Bunge live. Napata shida sana pale watu wanapong’ang’ania kuonekana kwenye tv at least ningekuwa nasimama mimi Mbunge mpya, mdogo niseme nionekane lakini kuna watu wana majina, nina mdogo wangu ana miaka sita anamjua Mbowe ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, sasa anang’ang’ania kuonekana kwenye tv ili iweje? Tukiachilia mbali hilo, tumeona sasa hivi Wabunge wa Upinzani wakisema hoja zao zikisikika. Kwa hiyo, naomba sana kumpongeza Mheshimiwa Nape.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, naomba kuzungumzia bajeti ya Waziri Mkuu na naomba nijielekeze kuzungumzia mustakabali wa vijana katika nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Waziri Mkuu inasema utafiti wa mwaka jana vijana ni asilimia 59 hii inaonesha vijana ni kundi kubwa. Vijana hawa wanatakiwa kuwekewa mazingira mazuri, mazingira bora kwa sababu ndiyo nguvu kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vijana ambao wamegawanyika katika makundi matatu, kuna kundi la vijana ambao wanamaliza elimu ya msingi wanashindwa kuendelea na elimu, hawapewi vitu vya kufanya na mbaya zaidi Wabunge wengi au watu wengi ndiyo wanaowachukua kuwafanya wafanyakazi wa ndani, hii inaumiza. Unajua suala la ajira inabidi tuliongelee kutoka moyoni, wewe unamuona ni binti ana miaka 13 anakuja kukuomba kazi za ndani unamwajiri na umesimama hapa Mbunge unasema ajira kwa vijana huu ni unyanyasaji. Tunapozungumzia ajira inabidi sisi wenyewe tuonekane kwamba suala hili sisi wenyewe halitufurahishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kuna suala linaniudhi sana, vijana wengi sasa hivi wanamaliza chuo kikuu mashallah unamkuta mtu amemaliza degree yake ya kwanza anaenda kusoma masters anafika hadi Ph.D, linapokuja suala la kupata ajira anaambiwa awe na experience, experience inatoka wapi. Usiponipa ajira ili nifanye kazi experience nitaitoa wapi? Suala hili linaumiza na naomba Wizara husika ilitilie maanani. Tunamwona Mheshimiwa Rais kawateua Wabunge ambao hawakuwepo katika mrengo wa kisiasa, wameteuliwa kuwa Wabunge wamekuwa Mawaziri na wanafanya kazi nzuri kwa nini hawa vijana tusiwape nafasi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Kamati yangu nilikuwa nazunguka sana naona wanakuja mainjinia, mimi ninamdadisi tu, baba shikamoo, hivi una muda gani hapa, mwanangu niko muda mrefu nina miaka 40 wakati kuna watu wamemaliza chuo, wanaweza, ni vijana wadogo hawapewi nafasi, wanawaacha tu walewale wa siku zote wanang’ang’ania zile nafasi. Si jambo zuri tuwape vijana nafasi waonyeshe uwezo wao.
Naomba Wizara iseme kama kila mwaka tunaajiri watu labda 500 katika hao asilimia 20 wawe ni vijana waliotoka vyuoni ili na wao waweze kupata nafasi, bila kuwapa nafasi hatuwezi kuona nguvu kazi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho nataka kuzungumzia ni vijana wajasiriamali wapewe mikopo. Juzi nimeuliza swali Mheshimiwa Waziri kanijibu, lakini hawa vijana wajasiriamali ndiyo wengi wamejiajiri lakini mitaji yao ni midogo. Naomba bajeti ya Wizara ione inaweza kuwasaidia vipi vijana wajasiriamali. Kama nilivyotangulia kusema awali niliomba hifadhi za jamii ziweze kujengewa uwezo ili vijana waweze kwenda kukopa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine Mheshimiwa Rais aliagiza vijana wanaocheza pool table wachukuliwe na watafutiwe sehemu ya kupelekwa, hii imekuwa ni shida. Mheshimiwa Rais hakusema wale vijana wachukuliwe wapelekwe Polisi au watishiwe maisha maana sasa imekuwa tafrani. Lengo la Mheshimiwa Rais lilikuwa zuri kwani alisema vijana wale wachukuliwe watafutiwe kazi za kufanya kwenye mashamba makubwa ambayo watu wanayahodhi. Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya watumie zile fursa wakimkuta kijana anacheza pool table wamchukue wamwambie heka yako moja hii hapa lima nyanya, naamini kijana umemfundisha analima, amepata faida shilingi milioni mbili hawezi kurudi kucheza pool table. Kinachoshangaza Maaskari wanawachukua wanawafunga na kwa kuwa ni agizo la Mheshimiwa Rais anamwambia nipe hela nikuachie, wamefanya kama ni mtaji, kwa hiyo hili suala Wakuu wa Wilaya na Mikoa walisikilize. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna hili suala linaitwa betting maarufu kama mkeka sijui mnalijua suala hili, siyo vijana tu hata watu wazima wanaenda kucheza lakini hii ni kamari na hili ni bomu linalokuja kulipuka, likija kulipuka tutakuwa tumechelewa. Kijana kama mimi saa mbili asubuhi anaenda kucheza betting. Hao watu wa betting wanaenda kuomba leseni Halmashauri na wanapewa wanasema ni biashara, si biashara inaua nguvu kazi za vijana. Naomba wahusika walifuatilie kwani siyo suala zuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kwamba kila Halmashauri huwa zinatenga asilimia tano kwa ajili ya vijana. Halmashauri nyingi hazitengi asilimia hiyo. Nilikuwa nashauri Serikali iwape hati chafu kila Halmashauri ambayo haitatekeleza jambo hili ili kuwalazimisha kufanya kile kinachotakiwa kupeleka asilimia tano kwa vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuomba Wizara katika bajeti hii Mfuko wa Maendeleo ya Vijana uongezewe uwezo. Kwa kufanya hivyo itarahisa pesa kufika kwa vijana kiurahisi zaidi na kuwawezesha kupata maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho kabisa naomba kuzungumzia hili agizo tena la Mheshimiwa Rais kwa Serikali za Mitaa kutenga maeneo maalum yaani hili suala mimi linanikera.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimewashuhudia Mapolisi wanawakuta vijana wengine wamekaa tu mtaani wanakamatwa, Mheshimiwa Rais kaagiza watu hawatakiwi kuonekana, Mheshimiwa Rais tusimchonganishe na wananchi, tusimchonganishe na vijana. Wakuu wa Mikoa na viongozi wengine yale mashamba wanayohodhi wao kama wao watumie fursa zile kuwapa vijana ili waweze kupata mafanikio.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru na naunga mkono hoja.