Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii jioni ya leo ili na mimi niweze kusema machache juu ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri pale. Pengine nianze tu kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi kubwa wanayoifanya katika Wizara yetu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa pongezi hizo, sitakuwa na maneno mengi sana, nitajikita kwenye maeneo matatu. Kwanza nitaanza na Shirika letu la Utangazaji (TBC). Inasikitisha sana kuona kwamba TBC haifanyi vizuri hata Kamati yetu imesema kwamba TBC waongezewe pesa, TBC haifiki maeneo mengi nchini hivi, tatizo liko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri, TBC ndiyo wanatusaidia sisi hapa wakati wa kampeni TBC, ndiyo inasikika kila eneo. Kuna baadhi ya TV hazifanyi coverage kabisa hasa kwa upande wetu wa Chama cha Mapinduzi, hebu tuone sasa wakati umefika tuwekeze TBC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa kwenye kitabu hiki kwamba Azam TV wametumia dola milioni 40 takribani shilingi bilioni 90 tunashindwa nini kuwekeza kwenye TBC? Biashara ni ushindani kwa sababu hata ukipita mtaani unaona watu hawangalii TBC wanaangalia tv nyingine wakati hili ni Shirika kubwa la Taifa, tatizo liko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe wakati Mheshimiwa Waziri ana-wind tupeleke kwenye Kamati yetu ya Bajeti suala hili ili tuwawekee pesa TBC. Hili haliwezekani kwa sababu TBC ni shirika la wananchi, linatakiwa lifike kila kona ya Tanzania hii. Mimi nasikitika sana kwa sababu kama michango yetu haitazingatiwa maana yake TBC itakufa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sasa naomba nijikite kwenye TFF (Shirikisho la Mpira Tanzania). Sote tunakumbuka enzi ya Ndolanga wadau wa mpira ilikuwa kila siku ni mahakamani mpaka ikafika FIFA. Alipokuja Tenga nchi hii ilitulia na mpira ukaanza kwenda. Leo hii tunashuhudia Rais wa TFF kila siku ni migogoro. Tumeshuhudia migogoro imeanzia kwenye chaguzi za mikoa, kila siku unasikia huyu hana sifa, huyu hana personality, TFF imejaa Usimba na Uyanga. Tunashuhudia Kamati za TFF unakuta mtu ni Mwenyekiti/Rais wa Simba au Yanga huyo huyo unamkuta ni mshiriki wa TFF, tutafika wapi? Tunazungumzia mpira kwa sababu mpira ni biashara na ni ajira sasa tutafikaje kama tuna migogoro kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mzungumzaji wa mwanzo leo Mheshimiwa Juma Nkamia alisema kwamba FIFA wanaruhusu Serikali ku-interfere, mimi najua hairuhusiwi. Mimi naomba mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi tuhakikishe kwamba tunachagua viongozi ambao watasimamia maendeleo ya mpira ya nchi hii. Tuache habari ya Simba na Yanga. Hebu Rais wa TFF nenda kajifunze kwa wenzetu wa West Africa wanafanya nini, kwa nini wanafika mbele? Inasikitisha leo Tanzania yenye zaidi ya watu milioni 50 tuna mchezaji mmoja ambaye anacheza Europe, Mbwana Samatta, hivi imefikia hapa? Hebu tujiulize tumekosea wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine hatuna viwanja vya kutosha. Uwanja mzuri upo Dar es Salaam mikoani kote hakuna viwanja, sisi Chama cha Mapinduzi tuna viwanja vingi tu. Tunaomba Wizara husika ianze kukarabati viwanja vile tusitegemee tu ufadhili. Tuangalie namna gani ambavyo tunaweza kukarabati viwanja vile ili mpira uweze kuchezwa pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba nimeona kwamba Wizara itaanza kushirikiana na TAMISEMI kwa ajili ya kujenga vituo vya michezo mikoani. Ni jambo la kupongeza sana Mheshimiwa Waziri na mkashauri Waheshimiwa Wabunge pia waanzishe vituo katika majimbo yao, nadhani litakuwa ni jambo la busara sana. Nashauri Wahemishiwa Wabunge wachukue ushauri uliotolewa kwenye hotuba hii kwani una tija na manufaa kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 20 amezungumzia kwamba takribani asilimia 90 ya watumishi ambao wanafanya kazi katika vyombo vyetu vya habari hawana weledi au ujuzi wa mambo ya habari, hili jambo ni la kusikitisha sana. Hivi inawezekanaje mwandishi wa habari awe hana weledi wa kufanya kazi hii? Ndiyo maana yanazungumzwa mambo mengi kwamba hata utangazaji hauendi sawa, maneno yanayotamkwa siyo sahihi kwa sababu hawazingatii weledi. Nimwombe Mheshimiwa Waziri kupitia TCRA hebu angalieni weledi wa wafanyakazi hawa katika vyombo vyetu vya habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo maneno machache, naomba nikushukuru na naunga mkono hoja.