Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kuchangia bajeti ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, napenda kumshukuru sana Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Napenda kumshukuru kwa jinsi alivyoanza kuendesha Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa nguvu, kwa kasi na kwa weledi mkubwa na kwa vitendo na sio blah blah. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia tukiwa na mipango mingi, miradi mingi, maneno mengi lakini sasa hivi tumepata mtu ambaye anaonesha vitendo. Rais ambaye anaonesha kitu gani ambacho kinatakiwa na sio kuzungumza blah blah. Kwa muda mrefu tumekuwa na sera nyingi lakini ndugu zangu mtakubaliana nami kwa kipindi kifupi mmeona vitendo ambavyo amefanya. Amechukua hela kutoka mafungu mbalimbali na kuyapeleka kwenye mambo muhimu ambayo yanawagusa wananchi wa kawaida kama mambo ya barabara, vitanda hospitalini, madeski ya shule na mambo kadha wa kadha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ndugu zangu nimefurahi sana na nashukuru kupata mtendaji wa aina hiyo. Nchi yetu sasa hivi inataka kiongozi wa aina hiyo anayeweza kutoa amri, kutekeleza na kufuatilia. Naamini kama Rais Magufuli angekuwa amechukua mafunzo ya komandoo basi miezi sita tu hii nchi ingeweza kuwa kwenye mstari ambao unatakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kupongeza uongozi mzima kwa jitihada kubwa ambazo zimefanyika hivi karibu mpaka tumepata mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Kampala na kuyaleta kule kwenye bandari ya Tanga. Mradi huo ni mkubwa na lazima uende sambamba na sehemu ambazo bomba hilo litapita kwa kuonesha wananchi watafaidika namna gani. Bandari ya Tanga kama mlivyosikia ina kina kirefu kuliko bandari zote na ndiyo moja ya sababu iliyofanya tupate mradi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningefurahi sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kama wangechambua sasa hivi hiyo bajeti ambayo ipo, wahakikishe kwamba wanaimarisha vitu vyote ambavyo vinahitajika kwenye bandari ya Tanga, kuna vifaa ambavyo ni vichakavu sana kwenye bandari ile. Vifaa vyote hivyo na mambo yote hayo ambayo yanatakiwa ni lazima tuhakikishe kwamba bandari hiyo inaimarika ili tuweze kukabiliana na huo mradi ambao unakuja.
Ningeshukuru sana kama reli ya Tanga na yenyewe ingewezwa kuimarishwa. Najua imewekwa kwenye bajeti lakini nitashukuru kama na yenyewe inaweza kuwa kwenye standard gauge ili iweze kuungana na reli ya kati iweze manufaa makubwa kwenye mradi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitashukuru pia kama kiwanja cha ndege cha Mkoa wa Tanga kitaimarishwa kwa sababu sasa hivi kutakuwa na watu wengi, wimbi litakuwa ni kubwa, kwa hiyo, tunaomba uwanja huo na wenyewe uweze kuwekwa kwenye mpango huu na kuweza kuimarishwa kwa kupanuliwa tayari kwa kupokea wageni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, sisi Muheza bomba hilo litapita, tunataka kutayarisha kituo cha matunda (center ya matunda) kuhakikisha kwamba kwa mradi huo panakuwa na additional value ili kuona tunafaidika vipi na mradi huo. Kwa hiyo, tumeshatayarisha sehemu za wawekezaji kuhakikisha kwamba tunatengeneza sehemu ya matunda, tunataka Mji wa Muheza uwe mji wa matunda. Matunda yote ya Mkoa wa Tanga yaweze kupatikana kutokea Muheza. Tumeshaanza kukaribisha wawekezaji na tungeomba Serikali ituunge mkono kwenye hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo lakini vitu hivyo vinakwenda na miundombinu, ni lazima tuhakikishe kwamba tunaziimarisha barabara, mkoa wa Tanga tuna barabara ya Muheza kwenye Jimbo langu, barabara ambayo Serikali imeahidi kuiweka lami, barabara ya Amani mpaka Muheza. Amani kutoa vitu chungu mzima, kuna viungo, karafuu, pilipili manga, kuna vitu vingi sana na wakulima wa kule wanapata taabu sana kuleta vitu hivyo mjini. Pamoja na kuweka kituo cha matunda tuna mpango tuweke viwanda vya kusafishia viungo ili kuhakikisha kwamba Muheza inakuwa ni Muheza kweli kweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, najua kuna tatizo la maji ambalo tumeanza kulishughulikia kwa kumuomba Waziri anayehusika lakini ningeomba liwekewe mkazo. Bila maji Muheza haiwezi kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia nichangie suala la utalii. Vivutio ambavyo tunavyo nchi hii haviendani na watalii waliopo. Hatuwezi kusema tunakadiria watalii milioni 1.2 wakati tuna National Parks karibu 15, uwiano wake haupo. Kuna nchi ambazo zina kivutio kimoja tu, mimi nilikuwa Zimbabwe wana Victoria Falls tu lakini wanaingiza watalii milioni 2.5 kwa mwaka, sasa ni kwa nini sisi tushindwe kufanya vitu kama hivyo? Naomba suala hilo liangaliwe na tuone tunaweza kufanya nini kuweza kuongeza watalii. Kuna sehemu nyingi sana za utalii, Amani kule Muheza ni sehemu mojawapo ya watalii ila wanashindwa kwenda vizuri kule kwa sababu ya barabara. Naamini tutakapoiweka lami ile barabara kutakuwa na ongezeko la watalii sehemu za Amani.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kilimo ni muhimu na linakwenda sambamba kabisa na sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ya viwanda. Bila kilimo, mazao na malighafi hatuwezi kufika. Tuchukue mifano ya nchi nyingine ambapo wanawawezesha wakulima, wanawakopesha pembejeo, wanawapa mbolea bure halafu baadaye wanakuja kuelewana na Serikali namna ya kuwakata. Kwa hiyo, naamini tukifanya hivyo tutaweza kuhakikisha kwamba wakulima wetu wanaweza kufaidika na kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, napenda kuunga mkono bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ahsante sana.