Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumpongeza Waziri, Mheshimiwa Ummy Mwalimu; Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla na Watendaji wote wa Wizara kwa kuwasilisha vizuri hotuba yao hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya afya ni moja kati ya sekta nyeti Tanzania inayosimamiwa na Wizara ya Afya pamoja na hospitali zote za rufaa, hospitali za wilaya pamoja na vituo vya afya na zahanati zilizopo chini ya Serikali za Mitaa (Manispaa na Mitaa). Hizi zipo chini ya Wizara ya TAMISEMI pamoja na kwamba zote zinapata miongozo ya kiutendaji kutoka Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na umuhimu wa Idara hii ya Afya, Mkoa wetu wa Iringa unakabiliwa na changamoto zifuatazo:-

(i) Kukosekana kwa chumba cha uangalizi wa wagonjwa wa nje wa dharura OPD (Casuality/Emergence) hivyo kusababisha msongamano mkubwa wodini kwa zile huduma zinazohitaji uangalizi wa muda mfupi;

(ii) Uwiano mdogo wa daktari kwa mgonjwa, hivyo kufanya kuwa na msongamano mkubwa katika vyumba vya Madaktari wachache wanaokuwa zamu na kuongeza workload kwa Madaktari;

(iii) Kuna wodi nzuri za watoto zilizojengwa kwa ufadhili wa Hospitali ya Vicensa ya Italia na mzalendo mmoja, familia ya ASAS, lakini hakuna Daktari Bingwa wa watoto (pediatrician) pamoja na idadi kubwa ya watoto wanaolazwa hospitalini hapo;

(iv) Hakuna Kitengo cha ENT (sikio, pua na koo) wala Daktari wa ENT hivyo, case zote za ENT lazima zipewe rufaa au kusubiri visiting doctor ambapo ni kero kwa wagonjwa wenye matatizo hayo;

(v) Vitendea kazi muhimu wodini ni vichache kama vile oxygen cylinder na oxygen concentrators, pulsometor za kupimia kiwango cha oxygen kwa wagonjwa, BP machines hazina uwiano unaostahili kwa ugonjwa (wodi nzima inaweza kuwa na mashine moja tu) na vipimo vya sukari kwa wagonjwa wa sukari waliopo wodini wanaohitaji uangalizi wa kina;

(vi) Kitengo cha Afya ya Akili hakikidhi haja na mahitaji ya wagonjwa wa afya ya akili kwa sababu kina vyumba vinne yaani viwili kwa wanaume na viwili kwa wanawake vyenye uwezo wa kukaa na wagonjwa wawili kila chumba. Hivyo, uwezo wa hospitali kuhudumia wagonjwa wa akili ni wagonjwa nane tu ambayo ni hatari kwa hospitali yenye kiwango cha Hospitali ya Mkoa ya Rufaa;

(vii) Wagonjwa wanaohitaji msamaha hawapati huduma za dawa kama inavyostahili kutokana na dawa nyingi kutokuwepo hospitalini. Hali hii husababisha shida zaidi kwa wagonjwa wasio na uwezo, wazee na wenye magonjwa ya kudumu (sukari, akili, TB na HIV);

(viii) Nyumba za Madaktari, zaidi ya 85% ya Madaktari na wahudumu wengine wa afya wanakaa maeneo ya mbali na hospitali kutokana na kukosekana nyumba. Hii ni changamoto hasa inapohitajika huduma ya dharura kwa mgonjwa hasa nyakati za usiku;

(ix) Kukosekana kwa huduma nyingine za msingi kama CT Scan, MRI, ECG, ECHO katika Hospitali ya Mkoa na kusababisha rufaa nyingine zisizokuwa na lazima ambapo ni kero kwa wananchi wanaohitaji huduma hizo;

(x) Kukosekana kwa mifumo ya kielektroniki inayowezesha daktari kupata majibu ya mgonjwa kutoka maabara na taarifa nyingine za mgonjwa kwa haraka kama ilivyo hospitali nyingine za private;

(xi) Kila wakati kukosekana kwa dawa muhimu hospitalini na kusababisha wagonjwa kuhangaika kwenda kutafuta dawa kwenye maduka ya watu binafsi na kero zaidi inakuwa wakati wa usiku ambapo na hayo maduka binafsi yanapokuwa yamefungwa, inaweza kuhatarisha maisha ya mgonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu Benki ya Wanawake. Niipongeze Serikali kwa kuweka dirisha la kuweza kuhudumia wananchi wa Mkoa wa Iringa. Hata hivyo, niiombe Serikali itoe mtaji wa kutosha ili ile dhamira ya kusaidia benki hii kwa ajili ya wanawake ipate kutimia. Pia nashauri kuwepo na mobile agency kwa ajili ya huduma hii kufikishwa mpaka vijijini kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu vituo vinavyolelea watoto yatima. Pamoja na wamiliki wa vituo hivi vya watoto yatima kuisaidia Serikali katika wimbi hili la watoto yatima na watoto wa mtaani lakini kuna changamoto nyingi zilizopo katika vituo hivi, kuna vituo havina hata uwezo wa kuwatibu watoto hawa wanapougua au kupata ajali. Hivyo, ni vema Serikali ikaweka utaratibu wa kusaidia vituo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.