Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Dr. Raphael Masunga Chegeni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba ya bajeti ya Wizara hii na napongeza sana jitihada ambazo Waziri na timu yake wanafanya katika kutekeleza majukumu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, Busega ni Wilaya changa sana haina Hospitali ya Wilaya na watendaji wa kada ya afya wenye sifa na kwa mujibu wa mahitaji. Naomba Wizara isaidie kupatikana fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya Hospitali ya Wilaya zikiwemo wodi, maabara, theatre na miundombinu stahiki ili wananchi waweze kupata huduma ya tiba. Pia tupewe kipaumbele katika suala la upatikanaji wa watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa kuwa baadhi ya watumishi yaani kada ya Clinical Officers (AMOs et cetera) wana wajibu wa kuwa wasimamizi wakuu wa vituo na zahanati, lakini unakuta kuna Wauguzi kwa ngazi ya shahada (degree) wanafanya kazi chini yao na pia mshahara hulipwa chini ya hao COs. Je, Wizara ina mpango gani wa ku- rationalize hizi kada kuondoa mkanganyiko wa maslahi kwa watumishi hawa? Naomba Wizara ichanganue kada hizi na maslahi stahiki yatolewe kwa watumishi hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, kwa kuwa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na hasa Busega unaweza kuchukua muda mrefu kukamilika; na kwa kuwa uwepo wa DDH husaidia sana kutoa huduma kwa wananchi ndani ya mkataba, Busega tulishaomba Mkula Hospital iwe DDH na Mheshimiwa Waziri alitembelea na kuahidi kutekeleza kauli hiyo ndani ya miezi mitatu ambayo ilishapita muda mrefu. Hivi sasa imesababisha wananchi walioahidiwa na Mheshimiwa Waziri kwenye mkutano wa hadhara kuona ahadi ya Waziri ilikuwa ni uongo. Je, Serikali kwa nini isiharakishe au kusaidia mchakato wa kukamilisha suala hili? Naomba Wizara kupitia kwa Waziri itimize ahadi ambayo imekuwa kero kubwa sana kwa wananchi hata kama kuna upungufu basi Wizara isaidie mchakato huo ili kuwezesha wananchi wa Busega na wa jirani wapate huduma hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, kwa kuwa Mhula Hospital kuna Chuo cha Nursing, je, Serikali haioni umuhimu wa kukisaidia ili kiweze kupanuliwa na kutoa mafunzo kwa kada hii muhimu na hasa Mkoa wa Simiyu? Naomba Serikali isaidie upatikanaji wa fedha na watumishi watakaoweza kusaidia chuo hiki muhimu na pia Wizara isaidie namna ya kuboresha badala ya kubeza na kutokutoa ushirikiano unaotakiwa. Ikiwa hoja hizi hazipati majibu stahiki nitashawishika kuomba maelezo zaidi yatakayopelekea nikalale na mshahara wa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kwa nafasi ya pekee namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuwa karibu na wananchi wa Busega na hasa katika ziara yake wakati wa uzinduzi wa nyumba za watumishi zilizojengwa kwa hisani na Taasisi ya Mheshimiwa Benjamini Mkapa Foundation. Ahadi yake ya kufanya ziara rasmi bado tunaisubiri kwa hamu. Nawapongeza Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara. Tunashukuru pia kwa msaada wa ambulance.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.