Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba na mimi nianze na pongezi. Naipongeza hotuba hii nzuri ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imesheheni mambo mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana ya Mkoa wa Katavi naomba nianze na eneo la afya. Mkoa wetu ni mpya, najua zipo jitihada za maksudi za kuusaidia Mkoa ule kwa maana ya kupata hospitali ya Mkoa. Rai yangu ni kwamba kama kwa kila mwaka tunatengewa shilingi bilioni moja na mpango mzima unakusudia bilioni 27 maana yake kuna miaka 27 kuweza kuijenga hospitali hiyo. Ninaomba Serikali yangu sikivu tupaone hapo kwamba watu wale kwa namna yoyote ile wasaidiwe ili kuhakikisha hospitali ya Mkoa inapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la maji niendelee kuishukuru Serikali hii, tulikuwa na mradi wa Ikolongo sasa hivi tunakusudia kuwa na mradi wa Ikolongo II. Mipango yote ya kuhakikisha mradi huo wa Ikolongo Na. II inaendelea kukamilika. Naendelea kuiomba Serikali maji haya ni msaada kwa wananchi wetu, pamoja na kwamba siyo wote wanaofikiwa na maji haya naendelea kuamini, utakapokuja mradi huu wa Ikolongo Na. II uwezekano wa eneo kubwa la Mji wa Mpanda kupata maji utakuwa umekamilika pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu eneo la barabara, mara ya mwisho tarehe 8 Aprili, kulikuwa na uzinduzi wa barabara Tabora – Koga - Mpanda kwa kiwango cha lami, mradi huo umeenda sambamba na watu wa Mbinga - Mbamba bay. Mimi nishukuru kwa jitihada hizo, lakini niendelee kuomba tena kwa maana ya barabara ya kutoka Sumbawanga - Mpanda na hiyo kama haitoshi kutoka Mpanda kwenda Kigoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni muhimu mno kwa watu wetu, siku zote naendelea kusema sioni kama ni sahihi kuwaita wale watu ni watu wa wapembezoni maanake hata Dar es Salaam yenyewe iko pembezoni, lakini suala tu la kuwezesha miundombinu itapelekea kufanya maeneo yale yasisomeke kama ya pembezoni.
Mkuu wangu wa Mkoa nilimpenda siku moja, alisema badala ya kuita ni mikoa ya pembezoni ni bora ikaitwa mikoa ya mipakani maana yake pembezoni inafanya watu wajione kuwa wanyonge na hawana sababu ya kuwa wanyonge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la madini. Mkoa wetu una bahati ya kuwa na madini mengi. Kuna dhahabu, kuna shaba, kuna garena, ni rai yangu na bahati nzuri ndugu zangu wa madini wapo hapa, kwanza nitakuwa mtu wa ajabu nisiposhukuru jitihada za makusudi zinazofanywa hasa kuwawezesha wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachokiomba, kuna maeneo ya Ibindi, maeneo ya Kapanda, maeneo ya Dirifu, maeneo haya kwanza kuna vijiji kuna makazi lakini maeneo pia ambapo wachimbaji wadogo wamekuwa wakijipatia riziki zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo maeneo mengine ya wachimbaji wadogo kutengewa maeneo, ninaomba Serikali hii sikivu iendelee kuyatenga maeneo hayo yawe rasmi kwa ajili ya wachimbaji wadogo, ili watu wao waendelee kukidhi shida zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la uvuvi, Mkoa wetu wa Katavi kwa ujumla wake upande mwingine tuna Ziwa Tanganyika. Tunapozungumzia uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kama ambavyo tumekuwa tukisaidia wananchi wetu kuwapa taarifa mbalimbali za hali ya hewa, kwamba kutakuwa na mvua kali, kutakuwa na mawingu, kutakuwa na nini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Serikali iende mbali zaidi, kama tutashindwa kuwa na vifaa vya uvuvi vya kisasa, walau basi iwepo na centre ya taarifa sahihi zinazogusa masuala ya kiuvuvi ili kuwasaidia wavuvi hawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yangu ni nini? Kama kuna taarifa zilizotoka kwa wataalam wetu kwamba kama Jumatano, Alhamis, Ijumaa mtakusudia kwenda Ziwani kuvua, uelekeo wa samaki utakuwa eneo la Kaskazini, uelekeo wa samaki utakuwa eneo la Kusini, kwa hiyo, mvuvi badala ya kwenda Kaskazini akaachana na samaki wako Kusini, kwa taarifa hizi zitamfanya avue uvuvi wenye tija. Lakini zaidi ya hapo ni kuwa na vifaa vya uvuvi vya kisasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, naomba nizungumzie suala la bandari. Najua jitihada zinazofanywa na nchi hii na kwa kweli niombe sana, siyo dhambi kuwa hapa tulipo na kusomeka ni nchi ambayo inazungukwa na maji pande zote, tuitumie hii kama ni fursa. Sisi kule kwa maana ya Ziwa Tanganyika tuna bandari ya Kalema, ni bandari ambayo ikifanyiwa kazi vizuri itaendelea kuibua fursa mbalimbali za watu na mali zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoke hapo nije kwenye eneo la misitu. Mkoa wangu wa Katavi kwa sehemu kubwa una misitu mizito. Nilichokuwa naiomba Serikali hii sisi kuwa na misitu isiwe dhambi. Nimeona vyombo vingine vya Kimataifa vinatoa fedha kwa ajili ya watu kuendelea kupanda miti na vitu vingine vya namna hiyo ikisaidia dunia hii kama maeneo ya mapumulio na kuachana na suala la hewa ukaa. Kwa hiyo, sisi ambao kwa bahati nzuri tumeendelea kutunza misitu hii isiwe dhambi sisi kuwa kwenye maeneo ya misitu. Serikali iendelee kuona kwamba watu hawa kwa kutunza mazingira na kwa kuwa na misitu mikubwa wanaendelea kuwasadia watu wa maeneo mengine, kwa hiyo tule nafasi ya sisi kutunza maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo niende eneo la utalii. Tuna mbuga nzuri ya Katavi nilisema mahali pengine na nitarudia tena. Tabia ya watalii kama hana kitu kipya cha kuona hana sababu ya kuja. Kwa hiyo, kwa nchi hii kuna maeneo mengine ambapo watalii wamekuwa wakiyatembelea miaka nenda miaka rudi. Sasa tusiwapoteze watalii hao kwa ajili ya kwenda maeneo ambayo wamekwishaona kwa zaidi ya miaka 15, tuibue fursa nyingine ndani ya nchi hii. Kwa hiyo, mtalii huyo badala ya kuikimbia Tanzania atakuja kwa kwenda eneo lingine, naomba sana tuinue eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kilimo najua kuna suala la pembejeo, lakini niombe sana habari ya matumizi ya mbegu ambazo hazina uhakika tutaendelea kuwafanya watu wetu wasitoke kwenye mduara wa umaskini. Kwa sababu kama anapanda halafu hana uhakika wa kuvuna huyu mkulima tunamtoaje hapo? Ataendelea kuzunguka kwenye mduara wa umaskini. Kwa hiyo, niombe sana, sambamba na pembejeo lakini tuendelee kuangalia suala hilo la mbegu bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la uwanja wa ndege, sikatai maeneo mengine kujengwa viwanja vya ndege lakini kupanga ni kuchagua. Kama kuna viwanja vilikwishajengwa na vingine havikukamilika kwa nini tunakwenda kuanza na vitu vingine vipya? Uwanja wa ndege wa Katavi pale Mpanda ni mzuri, umebakiza mambo machache ili ukamilike na ndege ziweze kufika pale, leo siuoni ukizungumzwa popote pale. Kama tatizo ni route za ndege, Serikali yangu sikivu ifanye hilo kwa makusudi kuhakikisha kama ni shirika letu hili ambalo lengo lake ni kutoa huduma kwa watu wote wapangiwe route, wakienda mara moja wakiona idadi ya wateja inapatikana wao wenyewe ndiyo watajikita katika kuongeza idadi ya route za kwenda huko. Nalisema hilo kwa sababu wananchi wengi wa Katavi wakitamani huduma ya ndege ama wakaipandie Mbeya ama wakapandie Kigoma sometimes wakapandie Mwanza na uwanja uko pale. Nilikuwa naliomba sana hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, reli niendelee kushukuru lakini tukisema tafsiri ya reli ya kati ni kutoka Dar es Salaam kwenda mpaka Kigoma, hiyo inayokwenda Mwanza lakini bila kusahau matawi ya Kaliua, Mpanda na Kalema. Tukilifanya hili lina tija, si kwamba watu tunatamani kulisema hilo, hapana, ni kwa maana ya tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala zima la vijana na mikopo niendelee kushukuru Serikali sikivu. Tukiendelea kuwawezesha vijana wao wenyewe ndiyo wataendelea kuibua miradi mbalimbali ya maendeleo. Kundi hili la vijana ambao wakati fulani wameonekana kama wamesahaulika tukiwajengea uwezo watatoka hapo walipo. Mimi nina mifano hai nikizungumzia kwa mfano wachimbaji wadogo wadogo ambao ni kundi la vijana, vijana hawa…
NAIBU SPIKA: Muda wako umeisha Mheshimiwa.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante.