Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Issa Ali Abbas Mangungu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbagala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kupata nafasi hii kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha leo kusimama hapa nikiwa Mbunge wa Jimbo la Mbagala. Pili, nimpongeze na niwapongeze wote ambao wameshinda katika Uchaguzi Mkuu huu akiwemo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mama Samia Suluh Hassan, Mawaziri na Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuchangia moja kwa moja hotuba ya Waziri Mkuu katika eneo la ajira. Jimbo langu la Mbagala lina viwanda ambavyo vinachangia pato la Taifa, vinachangia kodi lakini kumekuwa na malalamiko na manung’uniko mengi ya wafanyakazi katika viwanda hivyo. Waajiri wamekuwa wananyanyasa wafanyakazi, wanawatumikisha zaidi ya miaka sita mpaka miaka nane hawawapi mikataba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilivyoingia nimekuwa nikilifuatilia jambo hili na namshukuru sana Mheshimiwa Mavunde amenipa ushirikiano mkubwa maana Wilaya yetu ilikuwa hata Afisa Kazi hakuna lakini ameniahidi na amekuwa akimpa maelekezo Afisa Kazi yule ili kuweza kuja kutatua matatizo haya. Kwa hiyo, naomba muendelee kutusaidia maana wananchi wetu wanapata tabu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili katika eneo hili, katika Jimbo langu kuna viwanda lakini wawekezaji wale wameleta wafanyakazi wenye asili ya kigeni. Watu wale wanafanya kazi ambazo zingeweza kufanywa na mwananchi wa kawaida lakini wanaachwa wanaishi kwenye ma-godown mle, hakuna Afisa Uhamiaji anayekwenda kukagua vibali vyao, hakuna Afisa Kazi, wananyanyasa Watanzania kumekuwa na matatizo ambayo yangeweza kuepukika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana eneo letu la viwanda Mbagala mfanye ukaguzi wa uhakika na wa umakini. Zile kazi ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania wa kawaida wazifanye na hao wageni watafutiwe maeneo mengine ya kuweza kufanya kazi. Japokuwa tunataka teknolojia na maendeleo lakini nchi yetu isiwe jalala la kufanya watu waje tu kufanya kazi ambazo hata Watanzania wa kawaida wanaweza kuzifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo nije vilevile kwenye ajira za Walimu. Katika suala hili la ajira za Walimu kuna malalamiko mengi. Malalamiko haya yanatokana na kutopandishwa vyeo kwa muda mrefu na wanapandishwa vyeo lakini hawalipwi stahiki zao. Leo asubuhi limeulizwa swali na Mheshimiwa Naibu Waziri amelijibu, imefika mahali Walimu wamefanya kazi ya kusahihisha mitihani hawajapewa malipo yao. Yametoka maelekezo mikoa ilete, imeleta mikoa tisa kwa mujibu wa Mheshimiwa Waziri lakini hao waliochelewesha kuleta hawakutumbuliwa majipu na wameongezewa muda mpaka Jumatatu kama nimemsikiliza vizuri Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, madai ya Walimu yako mengi, matatizo ya Walimu yako mengi na kero za Walimu ziko nyingi. Mheshimiwa Waziri Mkuu wewe ulikuwa Mwalimu unajua changamoto zinazowakabili Walimu nchi hii, jitahidi kuhakikisha Walimu wanapata stahiki zao kwa wakati, wale wanaostahili kupandishwa vyeo wapandishwe vyeo kwa wakati na vile vile malipo yao yafanyike kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile niipongeze Serikali hii, leo tuna Waziri anayeshughulikia ulemavu. Napenda kuipongeza Serikali kwa sababu hapo nyuma ilikuwa inaonekana walemavu ni kama watu walioshindwa maisha, wasiokuwa na mwelekeo, walikuwa wanatengwa lakini baada ya kuteuliwa tu Mheshimiwa Possi amefanya ziara kuangalia vyuo vya walemavu, amezunguka kuangalia changamoto na matatizo ya walemavu, nampongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana waendelee kuimarisha kambi zile za walemavu mfano kule Nunge Kigamboni na Mbagala eneo la Chamazi kuna kambi ya Muhimbili. Kambi ile ilikuwa inawaweka wale walemavu wa matatizo ya akili na mambo mengine, lakini sasa hivi haina huduma zozote, eneo lake limeanza kuvamiwa na matokeo yake inakuwa ni maficho ya wahalifu. Ningeomba sana Mheshimiwa Possi na hili alitazame.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kuchangia ni kwenye elimu, Jimbo langu ni jipya ambalo lina wakazi zaidi ya watu laki nane. Baada ya kuanzishwa elimu bure kuna mfumuko mkubwa wa wanafunzi. Nitatolea mfano Shule ya Msingi Mbande iliyoko Kata ya Chamazi tuna wanafunzi wa darasa la kwanza 1,375; Shule ya Msingi Majimatitu nina wanafunzi elfu moja na mia mbili kadhaa. Juhudi zimekuwa zikifanywa na Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya lakini tunaomba Ofisi ya Waziri Mkuu itutazame kwa jicho la huruma sana. Jimbo la Mbagala limeelemewa na idadi kubwa ya wanafunzi na halmashauri ile uwezo wake ni mdogo. Kwa hiyo, naomba sana ndugu zangu Ofisi ya Waziri Mkuu mtuangalie kwa jicho la huruma kwa kutuongezea ruzuku, ushauri na ufundi na kwa jinsi mtakavyoweza kutusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoke hapo niende kwenye suala la maji. Nimesikia programu nyingi sana za maji lakini hakuna hata moja iliyogusa Jimbo la Mbagala na Wilaya ya Temeke. Ukisikia programu Ruvu Juu inakwenda Kimara, Changanyikeni na maeneo mengine. Kulikuwa na mradi wa Kipera, Mkuranga na mradi wa Kimbiji, huu sasa ni mwaka wa nane haujatekelezwa na hatujapata maji hayo yanayotoka katika vyanzo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukisema hapa kuna Mto Rufiji unao uwezo wa kuchangia upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengi ambayo mradi huu wa maji unaweza ukapita kama ukiwekewa msisitizo. Mfano ukitoa maji Mto Rufiji yatapita Ikwiriri, Kibiti, Bungu, Jaribu, Njopeka, Kimanzichana, Mkuranga yenyewe, Vikindu, Kongowe, Mbagala, Temeke na maeneo mengine ya Jiji la Dar es Salaam. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri wa Maji hebu angalia jinsi gani unavyoweza ukaanza mchakato wa kutuletea maji kupitia Mto Rufiji na vile vile mradi huo wa Kipera, Kimbiji nao utekelezwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine naomba Mbagala sasa hivi ina wakazi karibu laki nane, maji ni ya kisima. Mbagala ina viwanda, maji ni ya visima, je, mnatuweka katika kundi gani? Maana walioko pembezoni ya nchi wanasema wamesahauliwa, jamani Mbagala iko Dar es Salaam, tumekosa nini kule hatuna maji safi na salama? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niingie kwenye suala la ulinzi na usalama. Mbagala sasa hivi imekuwa wilaya lakini Kituo cha Polisi kinachotumika kama wilaya hata Police Post haistahili lakini Askari wetu kule sasa hivi wanatafuta bodaboda kwenye mitaa na mitutu ya bunduki, usiku wamelala, uhalifu unafanyika sana usiku hakuna misako, hakuna doria.
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Siku hizi Tigo wamekuwa kazi yao kukamata pikipiki mpaka mitaani zamani walianzia jijini katikati kule sasa wamekuja kwenye maeneo yetu ya mitaa. Kama kuna matatizo na maelekezo wapeni madereva wajielewe na waelewe, kama kuna elimu wapeni, wapewe leseni wafuate utaratibu, hawajakataa kufuata utaratibu lakini haya yamekuwa ni manyanyaso na kero kubwa. Naomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu hili nalo ulitazame na utoe maelekezo mahsusi juu ya madereva wa bodaboda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wastaafu nao jamani wamelalamika sana nchi hii. Kila tukija kwenye Bunge kuna kero za wastaafu, hebu tumalize na hili nalo ni jipu, walipwe stahiki zao. Juzi Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumza vizuri, kuna mchakato wa kuwaongezea zile pesa zao laki moja kutoka elfu hamsini lakini hata hiyo elfu hamsini maeneo mengine hazifiki, hebu angalieni jinsi gani ya kuwasaidia wastaafu hawa. Wapo wastaafu ambao wamestaafu jeshini, Walimu na watumishi wengine katika kada mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie mradi wa REA. Jimbo langu la Mbagala katika Kata ya Tuangoma, Chamazi na maeneo mengine yalipata mradi huu, nguzo sasa zimelala barabarani mwaka, miezi sita, waya hakuna, hakuna Mkandarasi, Wizara imekaa kimya na tunategemea Julai tunaanza mradi mpya, phase III, hebu hii phase II basi muisimamie maeneo yetu yapate umeme. Sambamba na hilo kuna low voltage. Mbagala ikifika saa 12 huwezi kuwasha fridge, kupiga pasi na kusikiliza redio na TV, umeme ni mdogo. Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini hebu tuangalie Mbagala kwa huruma, tuweze kupata umeme wa kutosha na wa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba niseme jambo moja. Hotuba hii ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu huna pa kuikosoa, imejielekeza katika kila eneo. Kwa hiyo, ninachoomba ni usimamizi ili yale ambayo tumeyakusudia yaweze kutekelezeka. Pili, wengi wanasema, Upinzani wanasema hivi, mimi sitaki kuwasema Upinzani, tulishasema toka kwenye kampeni tumejipanga na wataisoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mheshimiwa Majaliwa ametokea tangu Mwalimu, ametokea kwenye utumishi sasa ni Waziri Mkuu utamdanganya nini kwenye utumishi wa umma? Siyo hilo tu, Naibu Waziri, Mheshimiwa Mavunde alikuwa Mwenyekiti wa Vijana anawajua vijana na anajua mazingira ambayo anatakiwa ayatumikie, leo utasema nini na utamkosoa nini? Mheshimiwa Dkt. Possi ameshakuwa Mwalimu UDOM na maeneo mengine nje ya nchi amefundisha, leo ni Waziri anayeshughulikia walemavu utamdanganya nini, utamkosoa wapi? Mama Jenista Mhagama ninyi wenyewe mnamfahamu na mnamjua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme kwamba, tukijipanga vizuri siyo watasusia tu, watakuja kutaka ushauri kwetu na tunawakaribisha na tutawasikiliza ili tuweze kulipeleka mbele gurudumu la maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, juzi amefungua Daraja la Kigamboni, lakini pale pale baada ya kufungua daraja lile ameona kutakuwa na changamoto ya foleni. Kwa hiyo, amesema kabisa zijengwe njia sita kutoka Rangi Tatu mpaka Gerezani. Niombe sana Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi ahadi ile ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa pale isimamiwe kwa haraka ili kupunguza kero ya foleni kutoka Mbagala kuingia katikati ya mji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kuna barabara inayotoka Charambe kwenda Chamazi mpaka Msongola. Barabara ile iliwahi kuleta kashfa katika Serikali ya Awamu ya Pili na baadhi ya Mawaziri wa Awamu ya Tatu wakaenda Mahakamani, lakini mpaka leo haina marekebisho hasa kipande cha kutoka Kwa Mbiku mpaka Mbande haipitiki kabisa. Naomba sana Waziri wa Ujenzi katika majumuisho yake atujibu hili, imekuwa ni kero na ni tatizo kubwa. Ile barabara haina vituo vya basi, haifanyiwi matengenezo na imekuwa ni mahandaki matupu. Naomba sana Mheshimiwa Waziri ututazame kwa jicho la huruma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nipongeze sana Chama chama Mapinduzi kwa Ilani nzuri inayotekelezeka na inayoeleweka. Huwa wanasema Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi mnaahidi hamtekelezi, wameahidi Daraja la Kigamboni juzi tumefungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine, labda uelewa wangu mdogo. Mheshimiwa Rais alifuta Sherehe za Uhuru akasema pesa hizi ziende kutengeneza barabara ile ya Mwenge. Leo watu wanasema anatumia pesa vibaya, pesa zile hazijaidhinishwa, kwani jamani Wapinzani wamekuwa CAG wa nchi hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Bunge limetoa pesa kwa ajili ya utengenezaji wa madawati, ooh allocation ya ile pesa imeidhinishwa na nani, CAG atasema, kama kuna misallocation atasema jamani mlichofanya siyo. Leo wameanza wao kukosoa, si kwamba wanakosoa wanaona sasa hivi foleni hakuna kabisa barabara ya Mwenge kwenda katikati ya mji, kwa hiyo, hawana cha kusema na kama hawana cha kusema tutatafuta mengine ya kusema na tutawapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni demokrasia na utawala bora. Wanajua leo sisi tuna Awamu ya Tano ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, tumetoka tangu Awamu ya Kwanza ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wao wana awamu ngapi hata ya uongozi wa kwenye chama? Kwa hiyo, chama chetu kina demokrasia na tunakubali kukosolewa, tunajikosoa, tunasonga mbele na tutaendelea kusonga mbele Watanzania wanatuamini na wanakiheshimu Chama cha Mapinduzi kimekuwa chama cha mfano wa kuigwa Barani Afrika na dunia kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nichukue fursa hii kuunga mkono hoja na niwapongeze sana Mawaziri kwa ushirikiano wanaotupa, hakuna matabaka, wamekuwa wasikivu na tutaendelea kuwaombea Mungu mfanye kazi zenu ili nchi yetu isonge mbele. Matatizo na changamoto zipo, naamini kwa Serikali hii ilivyojipanga tutayatatua na tutakwenda tunapopahitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ahsante sana na naunga mkono hoja.